CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kitafanya mabadiliko makubwa ya kimfumo na katiba yake mwezi huu.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa, aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam jana kuwa, lengo ni kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
“Mabadiliko ya kimuundo yanayotarajiwa kufanyika yanalenga kupitisha muundo wa chama ambao utakiwezesha CHADEMA kujipanga vizuri zaidi katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya kuendelea kutetea mabadiliko na kushinda katika chaguzi zijazo.
“Mabadiliko ya wajibu wa wanachama yanalenga kukiweka zaidi chama mikononi mwa wanachama, hususan katika ngazi za chini na kuweza kuwaunganisha zaidi Watanzania katika kufanya mabadiliko ya kisiasa pamoja na kuchochea maendeleo.
“Pia mabadiliko mengine ambayo yatajadiliwa ikiwamo alama za CHADEMA, mathalan kadi na bendera, pia yanatarajiwa kujadiliwa. Mkutano huo pia unatarajiwa kupitisha programu ya miaka mitano ya chama,” alisema Dk. Slaa.
Alifafanua kuwa, muundo wa chama utabadilishwa kuanzia ngazi ya taifa hadi kwenye matawi. “Watanzania watarajie vitu vipya,” alisema, Dk. Slaa na kuongeza kuwa ukimya wa chama hicho baada ya uchaguzi utakwisha kwa makakati huu utakaotangazwa hivi karibuni.
Alisema nia ni kujenga heshima na kuonyesha Watanzania nafasi ya mfumo wa vyama vingi katika jamii. Kwa maelezo yake, mchakato wa maoni ya mabadiliko yatakayotangazwa Agosti 13, ulianza Januari, mwaka huu kwa utafiti uliohusisha wilaya 65 na hojaji zilitumwa kwa makao makuu ya mikoa yote. Sera ya Majimbo sasa itaingizwa rasmi kwenye Katiba ya CHADEMA.
Dk. Slaa alisema kwa sasa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatekeleza Sera ya Majimbo ya CHADEMA bila kujua, kwani inatumia utaratibu wa kugawa maendeleo kwa kanda, na hayo ndiyo majimbo. “Tunachotaka kufanya sisi si kuleta ukabila kama wanavyodai wasioelewa, bali ni kupanua wigo wa maamuzi kwa watu wa kawaida chini ya Sera ya Majimbo,” aliongeza.
Uzinduzi utafanyika Dar es Salaam saa 12 siku ya mkutano na alifafanua kuwa chama hicho kilikwishazinduliwa kilipoanzishwa isipokuwa sasa kinazinduliwa upya. Mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe 600 na waalikwa karibu 100 kutoka vyama vya siasa, mabalozi, taasisi za dini, NGOs, vyama vya wafanyakazi, nchi marafiki ikiwamo wanachama wa Democratic Union of Africa (DUA) na International Democratic Union (IDU).
Alisema vyama rafiki vilivyopo chini ya IDU na DUA baadhi vimeshinda uchaguzi kutokea kwenye upinzani, na vinatawala katika nchi kama Marekani, Australia, Ghana, Liberia na Ujerumani.
Dk. Slaa aliongeza kuwa, CHADEMA ndicho chama chenye mwelekeo na nguvu kwa sasa nchini na ndiyo maana kimeamua kufanya mabadiliko makubwa na kukipeleka chama kwa wananchi kwa nia ya kutoa ushindani wa kweli mwaka 2010 na hivyo kuongeza idadi ya wabunge na madiwani.