Na Maura Mwingira,
Musoma
09/08/2206
Rais Jakaya Kikwete amesema ikiwa hata wanafunzi wanaohitimu mafunzo yao katika vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi staid (VETA) nao wanalalamika kukosa ajira, basi kuna tatizo mahali.
Na kwa sababu hiyo, Rais amezitaka mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa taatizo hilo ikiwa ni pamoja na kufundisha somo la ujasiriamali ili liweze kuwasaidia wahitimu kubuni miradi itakayowawezesha kujiajiri.
Ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na uognozi wa Chuo cha VETA Mkoani Mara, mara baada ya kukitembelea na kukagua mafunzo mbalimbali yanayotolewa chuoni hapo.
Alipokuwa akizungumza na wananfunzi na kubadilishana nao mawazo walimweleza kuwa mafunzo wanayoyapata ya ubora wa hali ya juu, walimu wanafundisha vizuri, lakini wanakosa ajira za kuajiriwa au wanashindwa kujiajiri kutokana na kukosa mitaji na vifaa.
“Mheshimiwa Rais, tunapenda sana kujiajiri, lakini tunashindwa kwa kuwa tukitoka hapa, tunakosa mitaji na vifaa lakini pia tunakosa nafasi za kuajiriwa” Akasema mwanafunzi Juliet Joseph Opasi.
Rais alisema “Hii ndiyo ninayoina mimi namna gani mnawawezesha vijana wanaomaliza mafunzo yao VETA nao wajiajiri. Maana kama hawa wanaohitimu nao wanalalamikia ajira, basi kuna tatizo mahali”.
Alisisitiza kuwa vijana wengi wanaomaliza mafunzo yao VETA au hata vyuo vikuu, wanashindwa kujiajiri aidha kwa sababu ya kukosa mitaji au kutojiamini kuwa wanaweza kuanzisha miradi na kuiendesha.
“Ningeshauri kuwa somo la ujasiriamali liwe somo mtambuka ili vijana wakitoka hapa wajue namna gani ya kuanzisha mradi na kuuendesha kwani wengi wao wanashindwa kwa sababu ya hofu tu. Wafundisheni watoke hapa na ABC ya ujasiriamali na kujitahidi kuwawezesha ili wajisaidie.”, alifafanua Rais Kikwete.
Alisema kuwa Serikali Kuu itaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuwawezesha vijana kujiajiri wenye ikiwa ni pamoja na kuwapatia mitaji itakayotolewa kwa wale ambao watakuwa wamejiunga katika vikundi lakini pia ikiwa wameanzisha shughuli zinazoeleweka
Aidha Rais alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wasomi waliohitimu katika fani mbalimbali, wajiunge katika vikundi vya kitaaluma na kuanzisha makampuni ya kujiajiri.
Alisema kuwa jambo hilo linawezekana na kutoa mfano wa baadhi ya wanasheria ambao wamejiunda na kuanzisha kampuni za uwakili na kusisitiza kuwa serikali iko tayari kuwawezesha kwa kuwapatia mitaji.
Aidha Rais aliahidi kuwa atatafuta muda mzuri wa kuishukuru OPEC kwa msaada wao kwa chuo hicho pamoja na kuwahimiza waendelee kusaidia vyuo vya ufundi hapa nchini.
Akitoa taarifa fupi ya chuo Hicho, Mwenyekiti wa Bodi wa VETA kanmda ya Ziwa Bw. Enock Bendera alisema kuwa Chuo hicho kilianza mwaka 1986 ikiwa na wanafunzi 64 na kutoa mafunzo katika fani nne.
Baada ya kufanyiwa ukarabati na kuongezwa kwa majengo, kwa msaada wa OPEC, Chuo hicho ambacho ni kati ya vyuo 124 iliyopo katika kanda ya ziwa, sasa kina uwezo wa kuchukua wananfunzi 204 na kuongeza idadi ya fani hadi kufikia 9. OPEC ilitoa zaidi ya shs. Mil. 340.0 katika kukikarabati chuo hicho na kwamba idadi itaongezeka hadi kufikia 320.
Akielezea changomoto ya chuo hicho. Bw. Bendera alisema kuwa kuna ukosefu wa mabweni hali inayofanya chuo kutochukua wanafunzi kutoka wilaya nyingine. Alielezea changomoto nyingi ni ukosefu wa ajira ambapo ni asilimia kati ya 15 hadi 20 ndiyo wanaopata ajira za kuajiriwa, asilimia 33 ndiyo wanaojiajiri na waliobaki wanakosa ajira.
Naye Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Gilbert Kibonge aliwataka wazazi kuachana na dhana potofu ya kudhani kuwaVETA ni mahali ambapo wanapelekwa watoto waliofanya vibaya katika masomo yao ya sekondari au msingi. Alisema kuwa mafunzo yanayotolewa na VETA yahitaji wanafunzi wenye akili timamu na siyo walifeli katika shule ya sekondari au msingi.
Kabla ya kutembelea chuo cha hicho cha VETA Rais Jakaya Kikwete ambaye amenza ziara yake ya siku sita mkoani Mara ikiwa amefuatana na Mama Salma Kikwete, aliitembelea Hospitali ya Mkoa na kufungua wadi mpya ya wazazi na watoto na kuwafariji wagonjwa.
Akitoa maelezo ya ujenzi wa wadi hizo, mganga mkuu mfawidhi wa hospitali hiyo alisema kuwa hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1932 na sasa ina umri wa miaka 73, alibainisha kuwa kutokana na umri na uchakavu wa majengo wa hospitali, imekuwa ikikabiliwa na mlundikano mkubwa wa wagonjwa hususan katika wadi za wazazi na watoto.
Akasema ni kutokana na msongamano huo na kwa msaada wa fedha kutoka serikalini, hospitali imeweza kujenga wadi mbili za watoto na wazazi na hivyo kupunguza msongamano.
Aidha alisema kutokana na kuongezeka kwa bajejti ya hospitali hiyo kutoka shs. Mil. 78.0 kwa mwaka hadi mil. 243.0 katika mwaka huu wa fedha, hospitali itaweza kuendelea na ujenzi wa majengo mengine pamoja na kukarabati wadi ambazo ni chakavu.
Aidha mganga huyo alisema hospitali hiyo ambayo ina vitanda 226, inakabiliwa na upungufuu mkubwa wa wataalam lakini hivi karibuni imeweza kuajiri watumishi wapya 14.
Akiushukuru uongozi wa hospitali hiyo, Rais alisema serikali itaendelea kuboresha huduma za afya hapa nchini na kuongeza bajeti katika hospitali za mikoa kama ilivyojitokeza katika bajeti ya mwaka huu.
Aliwahimiza kuendelea kuyahifadhi majengo hayo ikiwa ni pamoja na kutunza vifaa ili wananchi waweze kupata huduma nzuri na bora.
Rais Pia alitembelea Kiwanda cha MUTEX, na vile vile kuhutubia mkutano wa hadhara.
Katika hatua nyingine Rais Kikwete amechangia chama cha kuweka na kukopa (SACOS) ambapo wanachama wake ni watumishi wa hospitali hiyo shs. Mil 3.0 ili kuongezea mtaji wao wenye thamani ya shillingi milioni 17.0. SACOS hiyo ina wanachama 139 na imekwisha kutoa mikoa wenye thamani ya shs. Mil. 13.0 kwa wanachama 101.