Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mpasuko CCM
Mpasuko CCM
By Habari Tanzania | Published  08/9/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Charles Mullinda

UMETOKEA mpasuko mkubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbarali, ambako Baraza la Wazee wa chama hicho, wameeleza kwamba, hawamtaki tena mbunge wao, Esterina Kilasi.


Wameandika barua kwa Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Yusuf Makamba, na nakala yake kupelekwa kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Naibu Katibu Mkuu, Kepteni aka Mwambi.


Wazee hao wanamwomba Katibu Mkuu amwajibishe mbunge huyo, kwa madai kwamba anakwenda kinyume cha CCM, na amekuwa akikutana na madiwani wa Upinzani na kula njama dhidi ya sera za CCM.


Waliojihusisha moja kwa moja na barua hiyo, ni Mwenyekiti Yusuph Mlwilo, Makamu Mwenyekiti Yasini Chekecheke na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Evance Minzi. Wameeleza wazi kwamba, chama hicho sasa kipo katika hali mbaya na ya hatari kisiasa.


Barua hiyo inamtuhumu Kilasi kwa mambo kadhaa na inamuelezea kuwa ni mbunge asiyeeleweka, ananadi ilani ya chama gani, kwa sababu michango anayoitoa ndani ya Bunge haiendani na maadili ya CCM.


Barua hiyo ya Julai 26, 2006, inaeleza kuwa Kilasi anapingana na zoezi lililofanyika la kubinafsisha mashamba ya Mbarali na Kapunga.


“Tumemsikia akipingana na ubinafsishaji wa mashamba ya Mbarali na Kapunga, zoezi ambalo lilifanyika kwa uwazi na kwa taratibu zote za ubinafsishaji kupitia Tume ya Rais (ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa) ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma.


“Anayoyafanya hayaendani na maadili ya chama chetu, amesikika akihoji juu ya wafugaji waliovamia Ihefu na kuharibu mazingira, eti waende wapi wakati anajua wengi wamekwishaondoka eneo hilo.


“Tunajua hao wakorofi na mabingwa wa kuhonga walifika nyumbani kwake usiku wa Alhamisi ya Julai 13 wakamlilia hali, kuwa hawajui waende wapi na wakampatia sh milioni 10. Aliporudi bungeni alipata nguvu ya kuuliza swali la kuwatetea waharibifu hao,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.


Tuhuma nyingine za Kilasi zilizoorodheshwa katika barua hiyo ni kuwatetea wana CCM waliohukumiwa na vikao vya tawi, kata na Wilaya ya Mbarali wachukuliwe hatua kali kwa kosa la kuwapa shida wanachama wenzao wakati wa kampeni za uchaguzi.
Wanachama hao wanadaiwa kucheza mchezo mchafu uliokuwa umelenga kuwakosesha ushindi wagombea udiwani wa CCM katika kata nane za Wilaya ya Mbarali.


“Kilasi alimshawishi Hawa Kiwele amkatie rufaa Grace Chalangwe katika kuwania nafasi ya viti maalumu ya udiwani, wakati jina la Chalangwe lilirudishwa na chama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, jambo hilo lilizua mtafaruku na mgongano ndani ya chama wilayani.


“Alifika mpaka mahakamani kupata nguvu ya kisheria, akaenda mpaka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya akihoji kwa nini limerudi jina la tatu wakati mwaka 2000 jina lake lilikuwa la tatu na ndilo likarudi.


“Anashirikiana na wapinzani kupinga sera za CCM kwa kuandaa mabango ya kupinga ubinafsishaji wa mashamba ya Mbarali na Kapunga na amekuwa akiandaa vikao kwa kushirikiana na madiwani wa TLP kupinga utekelezaji wa sera za CCM,” inasomeka barua hiyo.


Wazee hao waliendelea kueleza: “Siku ya ujio wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete Mbarali kuja kuomba kura, yeye akishirikiana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wakati huo, Ndg. Mateo Qaresi, waliandaa mabango ambayo yalikamatwa katika Kijiji cha Igawa yakisomeka; ‘Tunapinga mashamba ya Kapunga na Mbarali kubinafsishwa’, jambo ambalo hata Katibu wa Mkoa na RPC hawakuliafiki, kwani tulitegemea kuona mabango ya kuzidi kumpa moyo mgombea na kumuahidi kura nyingi siyo kumshirikisha matatizo kipindi kigumu kama hicho!


“Cha kushangaza, mama huyu na Qares walihoji kwa nini yamekamatwa, kwani yana ubaya gani! Ndipo tulipogundua kuwa wao ndio wahusika wa mabango hayo ya uchonganishi kati ya wapiga kura na mgombea wetu wa urais (ilikuwa ni njama na hujuma kwa CCM na mgombea wetu hasa wa urais,” wazee hao wameeleza.


Wana CCM hao wanaeleza katika barua hiyo kuwa, wanamuamini na kumtegemea Makamba kwamba anaweza kumshughulikia mbunge huyo na wanamuomba akutane na uongozi wa CCM wa Wilaya ya Mbarali, Baraza la Wazee, Mwenyekiti na Katibu wa CCM Wilaya, ili wampe picha ya hali halisi ilivyo mbaya ndani ya chama.


Wazee hao walihitimisha kwa kusema: “Tunaishia hapa, tukiamini tuliyoyasema ni sahihi kabisa, kupitia ahadi ya 8 (nane) ya mwana CCM isemayo ‘ nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko’. Tunakuomba wapinzani hao wasifanikiwe kabisa kutengua uamuzi sahihi uliofikiwa na Baraza la Mawaziri chini ya Mhe. Rais wa ubinafsishaji wa mashirika ya umma ambayo ni mzigo kwa serikali, ikiwa ni pamoja na mashamba haya.”


Alipozungumza na Tanzania Daima juzi kwa njia ya simu kutoka Dodoma, Kilasi alisema walioandika barua hiyo kwa Makamba ni wapinzani walio ndani ya chama hicho waliovaa kofia ya CCM, huku rohoni mwao wakiwa na damu iliyoiva upinzani.
“Najua wametumwa na mtu ili wanichafue, nahisi huyu anayewatuma hawa wapinzani waliomo ndani ya chama chetu ni mkuu wa wilaya wa zamani.


“Lakini ninachokitetea hata viongozi wangu wa CCM wanakijua, na wananiunga mkono kwamba ni bora shamba hilo libinafsishwe kwa wakulima wadogo wadogo kuliko kumpa mtu mmoja,” alisema Kilasi.


Mbunge huyo alisema hatishwi na maneno ya majungu yanayosambazwa na baadhi ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya Mbarali, kwa sababu tangu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, chama hicho kilikuwa kimegawanyika.


“Walianza zamani tangu wakati wa kampeni za uchaguzi. Mbarali kuna CCM A na CCM B, sasa mimi nipo hapo hapo katikati, sipo kundi A au B, lakini hali ya mambo inaharibiwa na hawa waliokuwa wakinipinga tangu mwanzo, wakitaka nisiwe mbunge,” alisema Kilasi.


Akizungumzia madai kwamba alipewa sh milioni 10 kama rushwa na watu waliotakiwa kuhama Ihefu, Kilasi alisema kwamba hao wanaodaiwa kumpa, hakuna hata mmoja mwenye uwezo wa kuwa na sh milioni 10, na kwamba siku ya Alhamisi ya Julai 13 hakuna mtu aliyefika kwake, bali ni majungu tu.


Kilasi alisema watu hao walioandika barua ni wazee wachache waliopewa fedha ili wamchafue. Alisema kwamba CCM wilayani Mbarali ina matatizo mengi, na atayaeleza baadaye.


Aidha, alieleza kuwa makundi yaliyoibuka wakati wa uchaguzi bado hayajavunjwa katika wilaya hiyo na ndio yanayoleta mitafaruku ya kila mara.


Ubinafsishaji wa mashamba ya Mbarali na Kapunga umezua mjadala mkubwa nchini, baadhi ya wananchi wakitaka yabinafsishwe kwa wakulima wadogo wadogo, badala ya kupewa mtu mmoja tu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.