Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Diallo aanika uozo Wizara ya Maliasili
Diallo aanika uozo Wizara ya Maliasili
By Habari Tanzania | Published  05/9/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Asema baadhi ya maofisa wanasafirisha magogo, Kwamba makontena 15 husafirishwa kila wiki
Wanahujumu amri ya serikali kuzuia biashara hiyo
 
JITIHADA za serikali kuzuia biashara ya magogo kusafirishwa nje zinagonga mwamba kwa sababu baadhi ya maofisa ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii wamo kwenye mtandao wa biashara hiyo, ambapo makontena l5 husafirishwa kila wiki.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Antony Diallo, ambaye aliweka hadharani uozo wa baadhi ya maofisa wa Wizara yake kwamba wanahusika na usafirishaji wa magogo nje ya nchi.
 
Alisema tayari ofisa mmoja wa Idara ya Misitu amegundulika akiwa na kampuni sita za kusafirisha magogo nje ya nchi, wakati ofisa mwingine aligundulika kumpa mkewe kampuni kubwa inayofanya biashara hiyo hiyo.
 
Waziri alisema jitihada za serikali kuzuia biashara hiyo zinagonga mwamba kutokana na kuwepo mtandao unaosaidiwa na baadhi ya maofisa na kwamba serikali imeishaunasa mtandao huo.
 
Diallo alisema hayo mbele ya waandishi wa habari alipokutana nao ofisini kwake kufafanua sababu za kuendelea biashara hiyo, licha ya kuzuiwa, kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2002.
 
“Serikali imegundua kwamba baadhi ya wafanyakazi wa idara ya misitu, wameunda mtandao kati yao na wafanyabiashara wa magogo hapa nchini na nje ya nchi, jambo ambalo limefanya sheria ya kuzuia biashara hiyo kupata kikwazo hadi sasa,” alisema.
 
Pamoja na sheria ya 2002 kuzuia kabisa biashara ya magogo, na serikali kutoa matangazo kadhaa ya kuzuia biashara hiyo, kwa sasa inasemekana inafanywa kwa siri na kwamba wastani wa makontena 15 yanasafirishwa kila wiki.
 
Waziri hakutaka kuwataja majina maofisa hao, lakini alisema serikali inaendelea kuchunguza mtandao wa maofisa mbalimbali wanaotuhumiwa kushirikiana pia na baadhi ya maofisa wa bandari na wafanyakazi wa baadhi ya meli.
 
Alisema serikali inaendelea kuchunguza mtandao, na kwamba hata magogo yaliyokamatwa yatapigwa mnada baada ya utaratibu kutangazwa wiki ijayo.
 
Akielezea sababu za kushabikiwa kwa biashara ya magogo nje ya nchi, alisema wafanyao biashara hiyo wanaipenda kwa vile ina faida kubwa katika nchi za China, India na Singapore.
 
“Nchi hizo hazitozi ushuru magogo yanayoingia kwa vile yanatengeneza ajira kwa watu wao, lakini zinatoza ushuru mbao kwa vile haziongezi ajira,” alisema.
 
Waziri pia alizungumzia viwanda vya mbao vilivyopo Dar es Salaam kwamba havikidhi sheria ya kuitwa viwanda vya mbao na kwamba serikali itaangalia uwezekano wa kuvifunga hadi vitakaporekebisha kasoro.
 
Alitoa onyo kwa wenye viwanda vya mbao nchini kurekebisha kasoro kwa kuchana mbao na kuziuza nje na ndani ya nchi kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
 

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.