WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameitaka serikali kuwa makini na mikataba ya uwekezaji wa mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na mradi wa chuma wa Liganga.
Walieleza hofu yao kwamba, hatimaye mikataba itakayofikiwa inaweza kulitia hasara taifa kama ilivyo kuwa kwa mikataba ya IPTL, Meremeta, SONGAS na mingine.
Wabunge hao walitoa tahadhari hiyo jana wakati wakichangia hotuba ya makadirio ya matumizi na mapato iliyowasilishwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Nazir Karamagi.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Lucy Owenya (CHADEMA), alisema miradi hiyo ni muhimu kwa taifa, hivyo serikali inatakiwa kuwa macho na uwekezeaji wake, kukwepa kuingia mkenge kama ilivyotokea kwenye baadhi ya mikataba ya miradi ya uwekezaji nchini.
Owenya alisema kambi ya upinzani imepokea taarifa nyingi za uwekezaji wa miradi ya Mchuchuma na Liganga, lakini serikali inapaswa kuwa makini ili kuliepusha taifa kwenye hasara kubwa kama ilivyokuwa kwenye miradi mingine ya uwekezaji nchini.
Aliitaja baadhi ya mikataba ya uwekezaji iliyoingia serikali na kusababisha hasara kubwa kwa taifa kuwa ni pamojana mkataba wa IPTL, SONGAS, KIA, Meremeta, Mwananchi Gold na TvT, ambayo alidai imeliingizia taifa hasara kubwa kutokana na kuingia mikataba hiyo kiholela.
Ili kuingia mikataba katika mradi wa Mchuchuma na Liganga, Owenya aliitaka serikali kuzingatia uwazi katika kuitisha na kuteua mwekezaji, uwezo wa kitaalamu wa kuweza kuchimba na kuchenjua madini ya aina mbalimbali, uwezo wa kifedha na uzoefu katika kufanya shughuli hiyo.
“Bila kufuata misingi hiyo, tutalipeleka suala hili kwa wananchi kwa nguvu zetu zote, kwani Watanzania wamechoshwa kubebeshwa gharama za mikataba potofu kama IPTL, SONGAS, KIA, Meremeta, Mwananchi Gold, TvT na migodi mingine ya dhahabu na almasi,” alisema Owenya.
Akiliwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, Msemaji wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, Herbert Mntangi, alisema miradi ya Mchuchuma na Liganga ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya Watanzania.
“Tunaipongeza serikali kwa jitihada inazofanya kupitia Shirika lake la Maendeleo la Taifa (NDC) ili kufanikisha miradi ya madini ya chuma Liganga na makaa
ya mawe ya Mchuchuma.
“Miradi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa taifa hili. Kamati inaishauri serikali kuchukua hatua thabiti na kwa uwazi zaidi ili kuendeleza miradi hiyo muhimu haraka iwezekanavyo,” alisema Mntangi
Naye Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), akichangia suala la uwekezaji wa Mchuchuma na Liganga, alisema kuna taarifa za serikali kumbeba mwekezaji mmoja bila kujali uwezo wake, na kuonya kuwa hali hiyo inaweza kuliingiza taifa katika hasara nyingine ya mikataba potofu.
“Naomba serikali izingatie uwezo, hasa wa teknolojia na kifedha na tuache dhana kwamba huyu ni mwenzetu, ana uhusiano wa karibu na viongozi,” alisema Kabwe.
Katika hatua nyingine, Owenya alisema Kambi ya Upinzani inataka kupewa taarifa juu ya Kampuni ya Tanzania Container Terminal, ambayo alisema ndiyo iliyokodishiwa Container Terminal katika Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema kuna malalamiko kwamba kampuni hiyo imeongezewa muda wa mkataba kwa miaka mingine 15, bila kufuata utaratibu wa kisheria uliowekwa, kama zabuni kutotangazwa kwa utaratibu ulio wazi.
Alisema kipindi hicho ni kirefu, akasema wanataka majibu ya kina, kwa nini mkataba huo wa ukodishaji umeongezwa bila zabuni kutangazwa na kufanywa kinyemela.
“Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuliarifu Bunge hili, wamiliki na wakurugenzi wa kampuni hii ni kina nani hasa, ili kuondoa minong’ono ya ‘conflict of interest’ ambayo sasa inatembea wazi mitaani.
“Kambi ya Upinzani inaitaka serikali iwasilishe kwa Kamati ya Viwanda na Uwekezaji hati za usajili wa kampuni hii, na hatimaye Bunge liarifiwe rasmi,” alisema Owenya.
Aidha, Owenya alisema wabunge wa Upinzani, wanaitaka serikali itoe majibu ya kina ya ni nani mmliki wa Kampuni ya Mwananchi Gold Mines Ltd, na kama wapo wengi, ni kina nani, na wana hisa ngapi katika kampuni hiyo kila mmoja.
Alisema serikali imetoa kauli kuwa Kampuni ya Meremeta imefilisika na imeeleza kuwa sasa wako kwenye hatua ya hitimisho, ikiwa na maana kuwa taratibu zote za ufilisi zimekamilika na ni hatua zenye usiri, hali inayowafanya wabunge wengi kudai taarifa hizo ili wajue kilichopo.
“Pamoja na hilo, tunataka kujua je, wadai ni kina nani na wanadai kiasi gani hadi kampuni iweze kufilisika, na mfilisi alichaguliwa kwa utaratibu gani?” alihoji
Owenya.
Suala jingine lililojadiliwa na Owenya ni madai kuwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limeteua mashirika binafsi nchini Dubai kukagua magari yanayonunuliwa na Watanzania kwenye soko la magari Dubai kwa dola za Marekani 150 (sh 187,500) kwa kila gari.
“Kama madai hayo ni kweli, basi ninaomba majibu ya kina, taratibu za serikali zilizotumika na sababu zilizofanya uongozi wa TBS uruhusu uamuzi huo na
kuwatoza Watanzania fedha nyingi kiasi hicho kwa kila gari wakati nchi nyingine za Afrika Mashariki hazitozi kodi hiyo,” alihoji Owenya.
Katika hotuba yake ya bajeti, Waziri Karamagi, aliomba kuidhinishiwa sh bilioni 15.7, kati ya hizo sh bilioni 9.5 ni kwa ajili ya taasisi zilizo chini ya wizara yake, na sh bilioni 6.1 ni kwa ajili ya idara zilizo katika wizara hiyo