Na Mwandishi Wetu
Bahati Nasibu "Tajirika na Twiga" inayoendeshwa na kampuni ya Sigara Tanzania, TCC, kupitia sigara yake ya Safari, mwishoni mwa wiki iliwapata washindi wa droo yake ya pili iliyofanyika kwenye miji 16 nchini.
Jumla ya washindi 256 wamepata bahati ya kutajirishwa na bahati nasibu hiyo, ambao watagawana jumla ya shilingi mil.24, wa kwanza akiondoka na shilingi Nusu Milioni na wa mwisho atapata shilingi 50,000/-.
Hivyo kila mkoa ulizalisha washindi 16 wanaogawana shilingi 1.5, ambapo mshindi wa kwanza anapata shilingi laki tano, washindi watano wanapata shilingi laki moja kila mmoja huku washindi wengine kumi wakipata shilingi elfu 50,000/- kila mmoja.
Mkoani Arusha droo hiyo ilifanyika kwenye klabu ya Silk iliyopo mjini hapa. Iliendeshwa na Meneja wa Meneja Msaidizi wa Tawi la TCC mkoani hapa Bw Oswald Elia akisaidiwa na Meneja Mkoa wa Arusha, Bi Janet Doo, ikisimamiwa na Meneja Masoko wa TCC nchini, Bi Stela Urio.
Bw.Elia alimtangaza mshindi wa shilingi Nusu Milioni mkoani hapa kuwa ni John Timoth Makame ambaye pamoja na washindi wengine wa nchi nzima watakabidhiwa zawadi zao mara taratibu za kuthibitisha ushindi wao na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini zitakapokamilika.
Bw Elia aliwataja washindi watano wanaopata shilingi laki moja kila moja kuwa ni Hamis Lenge,Lugano Richard, Saadan Macha,Yunus Ramadhan na Joseph George.
Akiongea katika hafla hiyo, Bw Elia alisema washindi wa mkoa huo pamoja na wengine wa nchi nzima wanapaswa kuwasiliana na mameneja matawi wa TCC ili kuchukua zawadi zao katika kipindi kisichozidi siku 45.
"Lengo la Bahati Nasibu hiyo ni kuwazawadia wavutaji wa Safari pamoja na kuitangaza bidhaa hiyo mpya na bora kutoka TCC," alisema.
Aliongeza kuwa sigara ya Safari ina umri wa miezi mitatu tangu iingie sokoni lakini imejizolea umaarufu kila kukicha.
Alisema droo ya mwishoni mwa wiki ni ya pili kati ya droo tatu za bahati nasibu hiyo. Droo ya kwanza ilifanyika Julai 8 na ya mwisho ni Septemba 9 mwaka huu.
Alisema washindi wa droo hiyo nchi nzima watatangazwa magazetini wiki hii.Mbali na Arusha mikoa inayoshiriki bahati nasibu hiyo ni Arusha,Kilimanjaro, Tanga,Zanzibar,Mtwara,Morogoro,Mbeya,Iringa,Dodoma, Ruvuma,Mwanza,Kagera,Mara,Shinyanga na Kigoma.