Wabunge wa mkoa wa Mwanza wanaungana na wananchi wa mkoa wa Mwanza walioandamana kuonyesha imani yao, mshikamano na kuunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa mwisho wa mwezi wa Julai ikilaani maudhui ya filamu ya ”The Darwins Nightmare”.
Wabunge hao walitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki walipokutana kujadili hotuba ya Rais kuhusu filamu ya The Darwins ambayo wamedai kuwa ilikuwa na lengo la kushusha uchumi wa mkoa wa Mwanza.
Walisema waliipokea hotuba ya Rais kwa furaha wakati anaongea na wananchi wa mkoa wa Mwanza hususani alipotoa kauli yake ya kulaani na kukanusha maudhui ya filamu hiyo ambayo ilitengenezwa na matayarishaji wa kigeni Bw. Hubert Sauper, mwaka jana na kuwashirikisha Watanzania wachache katika filamu hiyo.
Aidha, wabunge hao walisema wakiwa kama wawakilishi wa wananchi wa mkoa wa Mwanza, hawakubali kamwe nchi ichezewe na kudhalilishwa na wageni wasioitakia mema nchi yao.
Walisema kuwa mkoa wa Mwanza umejaliwa rasilimali nyingi kama madini, ziwa, samaki, mifugo na mazao mbalimbali ya chakula na biashara ambapo walisema inawezekana mtayarishaji wa filamu hiyo alikuwa na lengo la kuvuruga uchumi wa mkoa wa Mwanza.
Walisema wanahisi mtayarishaji wa filamu hiyo ana mpango wa kuvuruga uchumi hasa katika biashara ya samaki ambayo ndio tegemeo kubwa la uchumi katika mkoa wa Mwanza.
Aidha, walisema kama wabunge wa mkoa wa Mwanza, hawatakubali kuona uchumi wa mkoa wao unavurugwa na wanaungana na wananchi wa mkoa wao kulaani filamu hiyo.
Wabunge hao walisema wananchi wa Mwanza wataendelea kuvua, kushiriki katika biashara na uzushi wa Bw. Saupre hautawarudisha nyuma wananchi wa Mwanza.
Walioomba serikali kumchukulia hatua za kisheria mtu huyo na kumpiga marufuku kuingia nchini