UTATA mkubwa umegubika mchakato wa kuhesabu kura za uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi baada ya miaka 40, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Waangalizi wa kimataifa ambao awali waliusifu uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita kuwa ulikuwa wa amani, wamesema kuwa waliona kura zikiwa zimetupwa huku nyingine kutojumuishwa.
Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (HRW) lilisema kuwa waangalizi wa kimataifa kwenye eneo la mashariki la Ituri wamezuiwa kufanya kazi yao.
Watu zaidi ya milioni 25 walijisajili kupiga kura.
Wakati wa uchaguzi watu wengi walijitokeza na kulikuwa na matukio machache ya machafuko.
Kituo cha Marekani cha Carter Center na Umoja wa Mataifa waliusifu uchaguzi huo kuwa uliendeshwa kwa amani na kwa utaratibu.
Lakini katika siku za hivi karibuni hali ya utata imeibuka katika shughuli za kuhesabu kura.
Anneke van Woudenberg, wa HRW, alisema kuwa yeye mwenyewe amejionea kwa macho yake idadi kubwa ya karatasi za kupigia kura zikiwa zimetupwa nje ya ofisi za kuhesabu kura.
Kasoro nyingine pia ilikuwa idadi ya kura kutojumuishwa, ukosefu wa uthibitisho juu ya uhalisia wa katarasi za kupigia kura na kuongezeka kwa idadi ya kura bandia, alisema.
Alisema kuwa waangalizi wa kimataifa wakiwamo wa HRW, katika eneo la Ituri hawakujishughulisha sana katika shughuli za uangalizi, kutouliza maswali, kutoangalia karatasi za kupigia kura na kuwekewa ukomo wa uangalizi katika upigaji kura.
Colin Stewart wa Carter Centre, chombo huru cha uangalizi wa uchaguzi kilichoanzishwa na Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, alisema kuwa baadhi ya maofisa walikuwa wakisubiri kwa siku tatu kura zikusanywe na mwishoni waliamua kuzitupa kwenye malori.
“Hatuna uamuzi wa mwisho katika awamu hii, lakini kila siku tatizo jipya huibuka na kila tatizo lina nafasi ya kuharibu mchakato wa uchaguzi,” alisema.
Kutokana na ukubwa wa nchi hii, matokeo ya mwisho hayawezi kutolewa hadi baada ya wiki kadhaa.
Wagombea urais 32 akiwamo Rais Joseph Kabila, wanawania urais huku 9,000 wakiwania ubunge.
Wapiga kura walilindwa na askari 17,000 wa jeshi la kulinda amani la UN, wengi wao wakiwa katika eneo la mashariki mwa nchi.
BBC