Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wabunge ‘kumtafuna’ Waziri
Wabunge ‘kumtafuna’ Waziri
By Habari Tanzania | Published  08/6/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano, wametishia ‘kumtafuna’ Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nazir Karamagi, iwapo atawasilisha bungeni bajeti inayotetea ulaji, kesho.


Wengine wamefikia mahali pa kusema kuwa, kama watalazimishwa au watatishwa na wakubwa kuipitisha bajeti hiyo, huo utakuwa mwanzo wa mpasuko mkubwa ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani mambo yanayolindwa na waziri huyo ni machafu.


Baadhi yao, waliozungumza na gazeti hili jana kwa masharti ya kutotajwa majina, wamesema wako tayari kuibua kashfa zake na baadhi ya vigogo, iwapo wataona kwamba wakubwa wanamlinda apitishe bajeti yenye utata.


Wengi wa wabunge wa CCM, tayari wana shaka na bajeti itakayowasilishwa kesho.
Karamagi mwenyewe tayari ana wasiwasi, na ametumia muda mrefu wa juzi na jana kukutana na makundi ya wabunge wenye msimamo mkali, kuwashawishi wamuunge mkono.


Ijumaa wiki hii, aliwaalika wabunge wote wa Mkoa wa Iringa kwa chakula cha mchana, lakini baadhi yao walisema walichoitiwa kilikuwa zaidi ya chakula.
Mojawapo ya ujumbe ambao Karamagi amedaiwa kutoa kwa makundi kadhaa ya wabunge anaokutana nao, ni kuhusu mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma, na chuma cha Liganga, mkoani Iringa.


Habari kutoka miongoni mwa wabunge ni kwamba, yeye anampigia debe la wazi swaiba wake, Shubash Patel, mwenye Kampuni ya MMI, apewe miradi hiyo haraka iwezekanavyo.


Habari zinasema, ushawishi wa Karamagi kwa wabunge unakolezwa na kauli kwamba ‘Shubash anaungwa mkono na mzee,’ kauli ambayo imewaudhi wabunge wengi.
Katika kukabili upinzani dhidi ya jitihada zake, waziri huyo anasemekana kukutana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Biashara na Uwekezaji, iliyokwishatoa msimamo kwamba sheria na kanuni za uwekezaji zitumike kumpata mwekezaji anayefaa, na kwamba mradi huo usigawiwe kwa Patel kwa misingi ya urafiki.


Taarifa zilizolifikia gazeti hili, ni kwamba waziri ameweza kuwalainisha baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, na wameahidi kumsaidia kwa ama kunyamaza au kuwashawishi wabunge wenzao.


Lakini utafiti wa Tanzania Daima unaonyesha kwamba, robo tatu ya wabunge hawamwamini Karamagi. Baadhi yao wamesema anatumia vibaya jina la Rais Jakaya Kikwete kwa kudai kwamba ndiye anayembeba mwekezaji huyo kwa kusingizia misaada aliyotoa wakati wa kampeni za urais na ubunge katika majimbo kadhaa.
Kinachozungumzwa mno na wabunge ni kuhusika kwa Karamagi katika kashfa ya Bandari, ambapo mojawapo ya kampuni anazomiliki na kuendesha, TISCAN, imejiongezea mkataba wa miaka 15 utakaoisha mwaka 2025.


Awali, mkataba wa TISCAN ulipaswa kuisha mwaka 2010, lakini mara baada ya uchaguzi uliomweka Rais Kikwete madarakani na kumteua Karamagi, TISCAN iliongezewa mkataba wa miaka mingine 15 hata kabla ya muda wa mkataba wa awali kuisha.


“Njama hizi zimetuvunja moyo kwa kiwango kikubwa. Tunamshutumu kwa kuwa yeye ni mkurugenzi katika kampuni hiyo… kama amefanya hayo, kwa nini tumwamini katika suala la Mchuchuma?” alihoji mbunge mmoja.


Mwingine alisema: “Suala la Mchuchuma, jinsi anavyoliendesha, ni kwamba anatetea maslahi binafsi, si ya taifa. Na tunamtaka asimwingize mheshimiwa rais katika kashfa hizi.”


Wanasema Karamagi amekuwa akimtetea Patel kwa nguvu zote, hata kufikia kuunda kamati ya wataalamu wa wizara kuandaa ripoti tofauti na ya Kamati ya Bunge kuhusu vigezo vya kumpata mwekezaji anayefaa.


Baadhi ya wabunge wamesema kwa msisitizo kwamba baada ya kamati ya wataalamu kukamilisha kazi na kuungana na Kamati ya Bunge, waziri amefanya kila awezalo kupinda mapendekezo ili yampendelee Patel.


Katika mapendekezo ya awali yaliyotolewa na kamati ya wataalamu walioteuliwa na Karamagi kuhusu uchambuzi wa mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na mradi wa chuma wa Liganga, Mei mwaka huu, wataalamu walisema:


“Kwa kuwa miradi ya Mchuchuma na Liganga ni ya msingi na yenye maslahi makubwa kitaifa, kamati inapendekeza wawekezaji wa aina zote (wadogo kwa wakubwa) wanaotaka kushiriki katika kuendeleza na kuwekeza katika miradi hii, wafikiriwe baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina kibiashara, kisheria, kitaaluma… uchunguzi huu utasaidia katika kuthibitisha uwezo wao kifedha kitaaluma na uzoefu wa kutekeleza miradi ya aina hii.”


Hata hivyo, wabunge wanasema waziri aliomba mtaalamu mmojawapo (ambaye tayari ameshateuliwa kushika wadhifa mwingine) kuhariri ripoti hiyo kwa kuwa ilikuwa ‘haipendezi.’


Nakala ya ripoti ‘iliyorekebishwa’ inayopinga mapendekezo ya wabunge, inampendekeza Patel moja kwa moja. Katika mojawapo ya aya zake, inasomeka: “Kwa kuzingatia uzoefu wa MMI katika miradi kama hii, kamati inashauri Kampuni ya MMI iruhusiwe kuwekeza katika kichuguu kimoja (Liganga Hill) kati ya vichuguu vitano vya mradi wa Liganga…”


Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya uchimbaji na uchenjuaji chuma, wanasema huu ni ujanja wa kumpatia Patel mradi mzima, kwani madini ya chuma hayachimbwi kwa vitalu (vichuguu) kama dhahabu, vinginevyo hakuna mwekezaji anayeweza kukubali sharti hilo, kwani ili kupata faida, mwekezaji anapaswa kupata tani nyingi za chuma, tofauti na madini mengine yanayouzwa kwa kilo.


Habari zinasema, awali alikuwa akijenga hoja kwamba Patel anafaa kupewa mradi huo kwa kuwa ni mzalendo na yuko tayari kuanza. Lakini sasa ukweli ni kwamba wapo wazalendo wengine, Sub Sahara Resource NL & Crown Consortium Ltd, ambao nao wanaomba kupewa mradi huo, lakini hata walipotembelea Bunge kujitambulisha na kuwasilisha hoja yao kwa wabunge wiki chache zilizopita, waziri alikuwa ameshafanya uamuzi kwamba anayefaa kupewa ni Patel.


“Tunachotaka sisi, waziri aache upendeleo. Aendeshe mambo kwa haki, wanaotaka washindane; atakayeshinda apewe. Lakini hivi anavyopeleka mambo, anataka kutuburuza kubariki mchezo wake mchafu… sisi si wabunge wa kubariki michezo michafu ya mawaziri,” alionya mbunge mwingine.


Baadhi ya wabunge walifikia mahali pa kusema Patel hana sifa anazopewa na waziri, na kwamba akiachwa mwenyewe azitaje, hawezi kujitetea kama Karamagi anavyomtetea.


“We angalia nguvu anazotumia kutushawishi; mara anakutana na huyu, mara akutane na kundi fulani la wabunge… kuna nini? Kama mwekezaji wake hana teknolojia, kama hana uwezo wa kifedha, kwa nini tutumike kuhalalisha fedha walizopewa watu wengine kwenye uchaguzi mkuu? Kwa nini tufike mahali pa kutelekeza rasilimali za kitaifa kwa maslahi ya muda mfupi? Makosa yaliyofanywa na waliotangulia katika uwekezaji hayajamfunza lolote Karamagi?” alifoka mbunge mmoja.


“Patel amekuwa Patel… mara aseme rais anamtaka Patel; kuna ushahidi gani? Lakini hata kama angemtaka rais, si kazi yake kuwaburuza wabunge. Na kwa nini tuliletee taifa matatizo makubwa ya muda mrefu kwa kukimbilia faida ya muda mfupi?” alihoji mbunge mwingine.


Baadhi ya wabunge wameonyesha kutokuwa na imani na Patel na kutaka atimuliwe, lakini wizara ndiyo inayodaiwa kumlinda.


Baadhi ya wabunge walisema wamempania vilivyo Waziri Karamagi, na wakafikia mahali pa kusema “asipoangalia, anaweza kupoteza uwaziri kwa ajili ya Patel.”
Wakati Karamagi akikutana na wabunge, juzi alasiri Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alikutana na mawaziri wote na baadaye akakutana na wabunge wa CCM.


Tanzania Daima haikufanikiwa kujua kilichozungumzwa katika mkikutano yote miwili. Hata hivyo, inadhaniwa kwamba ilikuwa mikutano ya kuwekana sawa na kuwa na kauli moja ifikapo kesho.


Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema, inawezekana Lowassa ameamua kufanya mapema kuwawahi wabunge na kuwaandaa kisaikolojia kabla hawajalipuka kesho wakati wanachangia hoja katika bajeti ya Karamagi.


Wanasema inaweza kuwa mbinu mpya ya Lowassa ‘kuwabana’ wabunge, kwani huko nyuma alikuwa akiwaita baada ya kuona mjadala umekuwa mkali, lakini baada ya kushutumiwa kwa tabia hiyo, naye akakanusha, amebuni mbinu mpya ili kuondoa lawama.


Miradi ya Mchuchuma na Liganga imeleta msisimko wa pekee bungeni kutokana na kukosekana uwazi katika mchakato wa kumpata mwekezaji, huku ikiwa dhahiri kwamba Patel anabebwa na Waziri Karamagi.


Wabunge wanasema kinachokera ni kwamba Patel amejihusisha katika mazingira ya rushwa kwa madiwani, wabunge, viongozi waandamizi wilayani na mkoani Iringa.
Wanahoji sababu ya Patel ‘kupendwa’ hivi na Karamagi, na kwamba ni vema waziri afuate ushauri alipopewa na Kamati ya Bunge kama anataka kulinda heshima ya Serikali ya Jakaya Kikwete.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.