Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Ya Zombe yaanikwa
Ya Zombe yaanikwa
By Habari Tanzania | Published  08/5/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Maelezo ya awali yaanza kusomwa kortini
Adaiwa kuwaeleza mashahidi wangeuawa
Hapakuwa na majibizano ya risasi Sinza
Matundu yadaiwa kutobolewa kwa bisibisi
Yaelezwa gari la marehemu lilivyosachiwa
Kisha wakafungwa pingu, wakatoweshwa
 
Asha Bani na Denis Nduala
 
HATIMAYE maelezo ya awali yenye ushahidi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake 13 wanaotuhumiwa kwa mauaji ya wafanyabiashara wanne, yameanza kusomwa mahakamani.
 
Wakili wa Serikali, William Magoma, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Sivangilwa Mwangesi, alisoma maelezo ya mashahidi 21, kati ya 42 waliokwishaandika.
 
“Baada ya kuwatambua marehemu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ghafla tulikamatwa na polisi waliokuwa hospitalini wakilinda miili ya marehemu, tukapelekwa kwa aliyekuwa Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe,” alisema Wakili Magoma aliposoma maelezo ya Emmanuel Ikonga atakayekuwa shahidi.
 
Wakili huyo aliendelea kusoma maelezo ya Ikonga: “Baada ya kupelekwa kwa Zombe akatuambia kuwa, lazima tuuawe kwa kuwa alidai tulikuwa pamoja na wale marehemu wanne waliouawa na polisi.”
 
Ikonga ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ni mjomba wa Ephraim Chigumbi na Sabinus Chigambi au Jongo, ambao ni kati ya marehemu wanne waliouawa na polisi, wakidai kwamba ni majambazi.
 
Katika maelezo yake, Ikonga alidai kuwa, Zombe aliwaamuru askari waliowakamata akisema; “yaweke ndani majambazi, wakatuweka rumande hadi siku ya Januari 16 saa 4:00, akaja askari mmoja na kutufungulia huku akisema kuwa tulikuwa si majambazi.”
 
Naye Rashid Ally Rashid, aliyepangwa kuwa shahidi wa 12, ni muuza maji wa Sinza, ambaye katika maelezo yake, anasema kwamba, huko Sinza walipodai kulikuwa na majibizano ya risasi kati ya askari na majambazi usiku wa Januari 15, ilikuwa si kweli, kwa kuwa kulikuwa na ukuta wa nyumba isiyoisha ambao ulikuwa umewekwa alama ya chaki na kutobolewa na kitu kama bisibisi na wala si risasi kama ilivyodaiwa. “Usiku huo hatukusikia milio yoyote ya risasi,” amenukuliwa akisema shahidi huyo.
 
Bernadeta Lyimo, anayekuwa shahidi wa pili, ameandika maelezo kwamba, siku ya tukio alikuwa nyumbani kwake na shemeji zake ambao ni marehemu, na kwamba walimpelekea fedha za matumizi, mara likatokea gari la polisi, aina ya Toyota Stout rangi ya kijani, likiwa limebeba askari wanne akiwamo askari wa kike mmoja.
 
“Kati ya hao askari, kulikuwa na askari ambao waliwasimamisha marehemu (enzi za uhai wao) wakiwa kwenye teksi ambayo ilikuwa inaendeshwa na dereva wa teksi Juma Ndugu, wakaanza kuwasachi na kusachi gari nyuma ya buti la gari, wakatoa mkoba ambao ulikuwa na pesa nyingi sijui kiasi gani,” maelezo ya Lyimo yanasema.
 
Lyimo alisema kuwa, baada ya hapo, polisi walichukua mkoba huo na kumkabidhi askari wa kike ambaye aliingia nao kwenye gari, huku marehemu wakiwa wamefungwa pingu wawili wawili, wakielekea barabara ya Sam Nujoma.
 
Lyimo anaendelea kusimulia: “Siku inayofuata tukasikia kuwa wameuawa kwa kudai kuwa ni majambazi wakati si kweli, walikuwa ni wafanyabiashara wa madini wilayani Mahenge.”
 
Naye mtunza ghala la silaha katika Kituo cha Oysterbay, Koplo Sajo Kajela mwenye namba 07521, ameeleza kwamba, ilikuwa zamu yake ya kutunza silaha na aliwapa askari wa zamu silaha ambao Januari 15, baadhi walirudisha silaha zikiwa na risasi ambazo zimetumika.
 
Kati ya watuhumiwa ambao ilidaiwa na Koplo Sajo walirudisha silaha na risasi zilizotumika ni Rashid Lema aliyekabidhiwa silaha yenye risasi 30 na kutumia tatu kwa madai kuwa, alifanya mashambulizi dhidi ya majambazi usiku wa Januari 14.
 
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Zombe, Chiristopher Bageni, Ahmed Makele, Noel Leonard, Jane Andrew na Koplo Nyangelela Morris.
 
Wengine ni Koplo Emanuel Mabula, E.6712 Felix Sandys Cedrick, Koplo Michale, D.2300 Abeneth, DC Rashid Mahmoud Lema, D/CPL. Rajabu Hamis Bakari, Koplo Festus Philipo Bwabisabi, wote kwa pamoja wanaendelea kusota mahabusu ya Ukonga.
 
Watuhumiwa wanadaiwa kuwa, Januari 14 mwaka huu maeneo ya Pande kwenye msitu wa Mbezi Louis, waliwauwa ndugu watatu ambao ni wafanyabiashara wa madini wa Mahenge na dereva teksi mmoja. Washtakiwa wanatetewa na mawakili Jerome Msemwa na Fatuma Karume.
 
Waliouawa ni Mathias Lunkombe, Sabinus Chigumbi au Jongo, Ephaim Sabinus Chigumbi ambao walizikwa wilayani Mahenge na Juma Ndugu. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Ijumaa ijayo, ambako maelezo ya ushahidi yataendelea kusomwa.
 
Kesi hiyo ya mauaji, itasikilizwa na Mahakama Kuu, kwa kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za aina hiyo

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.