Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  MISHAHARA YA WAFANYAKAZI VIWANDANI MIDOGO –KIKWETE
MISHAHARA YA WAFANYAKAZI VIWANDANI MIDOGO –KIKWETE
By Habari Tanzania | Published  08/5/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Na Mwandishi Maalum
 
Rais Jakaya Kikwete amewataka wenye viwanda hapa nchini kupitia upya viwango vya mishahara wanavyowalipa wafanyakazi wao.
 
Alisema amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa viwandani wakielezea namna wanavyolipwa mishahara ambayo haiendani  na hali halisi ya maisha.
 
Rais ametoa wito huo leo wakati walipokuwa akizungumza na uongozi wa kiwanda cha nguo kilichopo mkoani Mwanza (MWATEX) wakati alipokitembelea  Kiwanda hivyo kukagua shughuli za uzalishaji. Hata hivyo hakuweza kujionea shughuli hizo kutokana na kukatika kwa umeme kulikotokea wakati  akiwa kiwandani hapo.
 
 “Kuhusu wafanyakazi,   ninaguswa sana na mishahara wanayolipwa, ni midogo sana, kwa kweli hili linanigusa sana, hebu liangalieni hili, ili nao waweze kuishi maisha mazuri” alisema Rais
 
Na kuongeza  kuwa amekuwa akipokea  malalamiko mengi, tena mengine yakielezea kuwa bado kuna viwanda vinalipa shillingi 26,000 kwa mwezi.kiwango alichosema  hiki ni kidogo sana kwa kweli na hakilingani na hali halisi ya maisha na kinawafanya waishi maisha ya kukopa.
 
Na kuongeza kwamba ni vema wenye  viwanda wakakaa chini na kupitia upya mishahara wanayowalipa wafanyakazi wao.
 
Alipendekeza kuwa njia moja wapo ambayo wenye viwanda wanaweza kuitumia katika kuboresha mishahara ya wafanyakazi, ni kwa wenye viwanda kutumia teknolojia za kisasa ambazo zitapunguza gharama za uzalishaji na hivyo kutoa mishahara mizuri  kwa wafanyakazi wao.
 
Alisema “Ukimlipa mfanyakazi mshahara  mdogo na huku analinda mali yenye thamani ya mamilioni hata ari yake ya kufanya kazi inakuwa chini, hawezi kujituma na yuko tayari kiwanda kife kwa kuwa hana uchungu nacho,  kwani hana anachofaidika nacho. Lakini  ukimlipa vizuri , anajituma zaidi katika kufanya kazi, kwani anakuwa ni sehemu ya kiwanda kile,” Alisisitiza Rais.
 
Akizungumzia kuhusu sekta ya nguo kwa ujumla, Rais alisema kuwa serikali ya awamu ya nne imeamua kutoa mkazo wa pekee katika ufufuaji na uendelezaji wa viwanda vya nguo hapa nchini kwa kuwa viwanda hivyo vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuongeza ajira.
 
Na alishukuru kwamba angalau viwanda vingi vya nguo vimefufuliwa na  viko katika mwelekeo mzuri.
 
 Alisema  “Sekta ya nguo ni eneo mojawapo ambalo nina interest nalo sana, ni eneo ambalo nimeazimia kuona kuwa mambo yake yanawekwa  sawa .  Kutokana  na umuhimu wake natarajia kuitisha mkutano wa sekta hiyo mwezi Septemba ambapo nitakaa na wadau wote na kuijadili kwa kina sekta hii” alibainisha.
 
Kutokana na umuhimu wa sekta ya nguo katika uchumi wa taifa, Rais alisema  anawashangaa sana watendaji serikalini ambao hawatatoa ushirikiano kwa wenye viwanda vya nguo na viwanda vingine hapa nchini.
 
Alisema Rais “Nitamshangaa sana mtu wa serikali ambaye hatasaidia  viwanda viweze kujiendesha,  mapato ya serikali yanatokana na kodi na ushuru mbalimbali unaotokana na sekta ya viwanda.
 
Kiwanda hicho cha MWATEX ambacho kilianza kufanya kazi miaka minne iliyopita tangu kiliposimama miaka tisa iliyopita, hivi sasa kinatoa kwa serikali shilingi bilioni nne kwa mwaka kama mchango wake wa kodi.
 
Katika mzungumzo hayo na uongozi wa MWATEX, Rais aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kujielekeza katika uzalishaji wa bidhaa zinazoelenga soko la nje.
 
Alibainisha  ukuaji wa uchumi utakuwa wa kasi zaidi ikiwa viwanda hapa nchini vikiwamo vile vya nguo vitajielekeza katika uzalishaji wa bidhaa zinazolenga soko la nje.
 
Akaupongeza uongozi wa kiwanda hicho ambao kabla ya mwisho wa mwaka huu wataanza kusafirisha nje nyuzi zenye ubora wa kimataifa.
 
Akitoa maelezo mafupi kuhusu maendeleo ya kiwanda hicho, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bw. Amini Radhan alisema kuwa  pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa za kukifufua kiwanda hicho ambacho walikikuta katika hali mbaya, kiwanda kinakabiliwa na ukosefu mkubwa sana wa wataalamu katika idara ya ufumaji (Weavers).
 
Alisema kuwa tatizo la wataalamu wa ufumaji si la kiwanda hicho peke yake bali ni la viwanda vyote vya nguo hapa nchini.
 
Alimweleza Rais kwamba kutokana na uhaba wa wataalamu hao kiwanda hicho hakiwezi kufikia malengo ya uzalishaji kwa kuwa idara ya ufumaji ndio idara tegemezi.
 
Bw. Radhani, aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kufufua chuo kilichokuwa kikitoa mafunzo wa wataalamu wa ufumaji, ambako katika miaka ya huko nyuma yalikuwa yalitolewa na  kampuni ya viwanda  vya nguo Tanzania, TEXCO.
 
Hata hivyo alisema uongozi wa kiwanda hicho umekuwa ukijadiliana na VETA kuangalia uwezekano wa kuanzisha mafunzo hayo. Jambo lililoungwa mkono na Rais.
 
Akielezea zaidi kuhusu uboreshaji wa kiwanda tangu kilipobinafshiwa kwao, Mkurugenzi huyo alisema kuwa  ukarabati na urekebishaji wa mitambo katika idara za usokotaji, ufumaji, na rangi umefikia asilimia 70.
 
Jumla ya wafanyakazi 1,300 wakiwamo vibarua wameajariwa katika kiwanda hicho.
 
Akielezea kuhusu mipango ya baadaye ya kiwanda hicho,  Mkurugenzi huyo, alisema kuwa kiwanda kimefunga mitambo ya kisasa katika idara ya usokotaji, itakayokiwezesha kiwanda  kutengeneza  nyuzi zenye ubora wa soko  la kimatifa zitakazouzwa nje.
 
Aidha   kutokana na uzalishaji wa nyuzi zenye ubora, kiwanda pia kitatumia nyuzi hizo kutengeneza cotton sanforized twill materials kwa ajili ya kuuza soko la kimataifa.
 
Kwa upande wa soko la AGOA, kiwanda cha MWATEX kinatarajia kuanzia msimu ujao wa pamba wa 2007/08  kiwanda kina mpango wa kuanzisha kiwanda cha knitting kwa ajili ya kuzalisha T-Shirts ambazo zitaweza kuingia katika soko la AGOA.
 
 Baadhi ya matatizo yanayokikabili kiwanda hicho ni ukatikaji wa mara kwa mara wa umeme, uhaba wa maji na gharama za mafuta.
 
Kuhusu gharama za mafuta, Mkurugenzi wa MWATEX alisema kiwanda  kimeanza kutafuta nishati mbadala ambayo ni matumizi ya mabaki ya mazao kama pumba za pamba, mpunga na mahindi kwa ajili ya kuendesha Boiler badala ya mafuta ya Furnace.
 
Kuhusu uhifadhi wa mazingira, kiwanda kimejenga kitivo cha kisasa cha uchambuzi wa rangi na madawa  chenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi zaidi ya mara kumi  ikilinganishwa na kivito kilichokuwapo.
 
Kuhusu tatizo la maji, kiwanda ina mpango wa kuvuta maji kutoka ziwa Victoria.
 
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amewataka wakurungenzi wa mipango miji, kuhakikisha kuwa wanatenga maeneo kwa ajili ya viwanda.
 
Alisema kuwa hivi sasa mkazo umekuwa katika utengaji wa maeneo ya viwanja vya makazi na kusahau kabisa kutenga maeneo ya viwanda.
 
Alisisitiza kuwa maeneo hayo yakishatengwa, ni lazima  wahusika wahakikishwe kuwa yanalindwa ili yasivamiwe na wananchi kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchi.
 
Alisema kuwa hivi sasa kumejitokeza tabia ya wananchi kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wenye viwanda, na kisha kuleta malumbano pale wenye viwanda wanapotaka kuendeleza maeneo yao.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.