Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Spika alimuokoa Karume’
Spika alimuokoa Karume’
By Habari Tanzania | Published  08/4/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Spika alimuokoa Karume’
 
-Waziri Kivuli adai alinasa vielelezo nyeti
-Adai vigogo Wizara ya Fedha wabadhirifu
-Amsifu Spika kwa kunusa makombora yake
-Kificho asema Baraza si jukwaa la siasa ng’o
 
 
Na Mwandishi Wetu
 
KAMBI ya Upinzani Zanzibar imedai kwamba, kitendo cha Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho kumzuia Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Abas Muhunzi kuwasilisha hotuba yake, kililenga kumlinda Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume dhidi ya kashfa.
 
Akizungumza juzi jioni, Muhunzi alisema hotuba yake ilibeba mambo matatu mazito, yanayohusu ubadhirifu katika Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar, ambayo ipo chini ya Rais Karume, ikisimamiwa na waziri wa nchi.
 
Muhunzi alisema kwamba, baada ya kufanywa utafiti wa kina imebainika suala la malipo ya wafanyakazi hewa serikalini pamoja na wastaafu, linawahusu baadhi ya watendaji wakuu katika Wizara ya Fedha na Uchumi Makao Makuu na kusababisha serikali kupoteza kiasi kikubwa cha fedha.
 
Alisema kwamba amebahatika kunasa ushahidi wa hundi za malipo ya wastaafu hewa kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na kusababisha serikali kupoteza milioni 140 kila mwezi.
 
Aidha, alisema kwamba hotuba yake ililenga kumtaka Waziri wa Nchi Afisi ya Rais anayeshughulikia fedha na uchumi kueleza vitendo vya kulipwa wafanyakazi hewa 1,400 na kuisababishia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hasara ya sh bilioni moja kila mwaka, vimeanza kufanyika kuanzia lini na pia alikuwa ahoji malipo ya wastaafu.
 
Alisema hoja ya tatu ni kuitaka Wizara ya Fedha na Uchumi itafutiwe waziri wake, badala ya kuendelea kufanya kazi chini ya Rais wa Zanzibar, ili kuwapo na uhuru wa kuhoji mambo mbalimbali kwa maslahi ya Wazanzibari.
 
“Spika alinusa vizuri hotuba yangu, kwani ilikuwa na mambo mazito na yenye maslahi kwa nchi na kutaka Wizara ya Fedha na Uchumi iondoshwe Ikulu. Haiwezekani wizara kama hii waziri afanye kazi kwa niaba ya mtu,” alishauri.
 
Kwa Muhunzi, hii ni mara ya pili kukumbwa na misukosuko, ambapo mara ya kwanza alitimuliwa barazani kwa mwaka mzima, baada ya kumhusisha Rais Karume na mchezo mchafu katika biashara ya mafuta Zanzibar.
 
Katika sakata hilo la kwanza, Baraza liliunda kamati ya uchunguzi na kueleza katika ripoti yake kwamba, vielelezo alivyotoa Muhunzi vilikuwa vyepesi na havikuweza kuthibitisha kuhusika kwa rais katika mchezo huo mchafu.
 
Katika mkutano mwingine wa juzi na waandishi wa habari, Kiongozi wa Upinzani, Abubakar Khamis Bakar, alisema msimamo wa mawaziri wao vivuli utaendelea kubakia pale pale, kutowasilisha hotuba zao kuhaririwa kwanza na Spika.
 
Alisema kwamba kufanya hivyo ni sawa na wapinzani kukosekana barazani, kwa vile uhuru wa kuikosoa serikali na kufichua maovu utakuwa unapotea.
 
Alieleza kwamba, utaratibu huo uliotangazwa na Spika haujawahi kutumiwa na Bunge lolote duniani, na unavuruga mgawanyo wa madaraka wa mihimili mitatu ya serikali; yaani Bunge, Mahakama na Utawala.
 
Abubakar alisema tangu kuanza kwa Kikao cha Bajeti, Spika amekuwa mstari wa mbele kuungana na serikali katika kupinga hoja za wapinzani za kutaka kuundwa kamati za kuchunguza vitendo vya ubadhirifu katika taasisi za umma.
 
Alitoa mfano kwamba, wajumbe walipendekeza kuundwa kamati ya kuchunguzwa Shirika la Umeme Zanzibar, Shirika la Meli na sakata la wafanyakazi hewa, lakini zote zimekataliwa.
 
Alisema kwamba ibara ya 92 (5) ya kanuni za Baraza hilo imeweka utaratibu waziri kivuli apewe hotuba ya serikali saa 24 kabla ya kuwasilishwa barazani, lakini wamekuwa wakipewa usiku wa kuamkia kikao, ili wasipate nafasi ya kuichambua na kuikosoa serikali katika mambo ya msingi.
 
Naye Spika Kificho alisema, alilazimika kuchukua hatua ya kumzuia waziri kivuli asiwasilishe hotuba yake kwa vile alishindwa kuzingatia utaratibu aliouweka kutaka azipitie kwanza hotuba za mawaziri vivuli.
 
Alieleza kwamba, kwa mujibu wa ibara ya 151 ya kanuni za baraza hilo, mambo ambayo kanuni zimekaa kimya bila ya kueleza kitu, Spika huwa mlezi wa kanuni hizo, ingawa zinakuwa ni mali ya wajumbe wote.
 
Alisema kwamba Baraza ni chombo cha wananchi, hivyo hatakubali kuona fedha za wananchi zinatumika kuwalipa watu wanaokwenda kusema mambo ambayo hayawafai wananchi wenyewe.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.