.Wahimiza uwekezaji katika elimu
Na Maura Mwingira, Washington
BENKI ya Dunia imeahidi kuendelea kuisaidia serikali ya awamu ya nne katika utekelezaji wa vipaumbele ilivyojiwekea, na kueleza kwamba ni jambo la msingi sana kuwekeza katika elimu.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais wa Benki ya Dunia, Paul Wolfowitz alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Rais Jakaya Kikwete, mjini Washington, Marekani.
Sambamba na kauli hiyo, watendaji wakuu wa taasisi za fedha za kimataifa, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha (IMF), walibainisha kuwa Tanzania bado ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo kuwa nchi ya mfano wa kuigwa barani Afrika.
Hayo yalibainshwa kwa nyakati tofauti na Rais wa Benki ya Dunia, Wolfowitz na Mkurugenzi Mtendaji IMF, Rodrigo de Rato, walipokutana na Rais Kikwete aliyetembelea makao makuu ya taasisi hizo, mjini Washington .
“Nitafurahi sana kusikia baada ya miaka mitano, jirani zenu na nchi nyingine katika Afrika, wakisema kama Tanzania wameweza, kwa nini wao wasiweze. Mna kila sababu na uwezo wa kufanya vizuri zaidi na kuwa nchi ya kupigiwa mfano,” alisema Rais wa Benki ya Dunia.
Rais Kikwete, ambaye yuko Marekani kwa ziara ya kikazi, alikwenda makao makuu ya taasisi hizo kwa lengo la kujitambulisha kwa watendaji wakuu wanaozisimamia na kuwaelezea mipango na mikakati anayotarajia kuifanya katika kipindi cha miaka mitano, changamoto zinazomkabili, kuelezea mtazamo wake kuhusu ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na taasisi hizo, na kuomba ushirikiano endelevu kutoka kwao.
Ikiwa hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kukutana ana kwa ana na watendaji hao tangu aliposhika madaraka ya kuongoza Tanzania, mwishoni mwa mwaka jana, Rais wa Benki ya Dunia alimweleza kuwa yeye binafsi amekuwa akifuatilia kwa karibu kila hatua ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambayo Tanzania inaendelea kupitia.
“Nimekuwa nikitafuta na kupata taarifa mbali mbali zinazohusu Tanzania kutoka vyanzo mbalimbali, na taarifa zote zimekuwa zikisifia namna ambavyo mmeweza kugeuka kutoka mfumo mmoja wa uchumi na kwenda mwingine katika kipindi kifupi, tena kwa mafanikio makubwa,” alisema.
Alisema kuwa mazingira ya amani na utawala unaozingatia sheria ni baadhi tu ya vigezo ambavyo vinatoa fursa ya kuendelea mbele zaidi.
Alibainisha kuwa katika mchakato wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano, uwekezaji katika sekta ya elimu ni jambo la msingi.
“Wenye mafuta watajidai na mafuta yao, mafuta ambayo kwa mtazamo wangu badala ya kuwa chanzo cha neema katika nchi hizo, kwa baadhi ya nchi yamekuwa laana. Na katika nchi kama yako ambayo huna mafuta, mafuta yako ni watu wako, wekezeni katika elimu, huo ndio urithi mkubwa kwa watu wako,” alisisitiza Wolfowitz na kuahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika kuendeleza sekta ya elimu.
Awali, Rais Kikwete katika mazungumzo yake alielezea changamoto zinazoikabili serikali katika sekta za elimu, ambazo ni ukosefu wa nyumba za walimu, uhaba wa walimu, na mchakato wa kuboresha mazingira ya utoaji elimu na ujenzi wa chuo kikuu kipya.
Wolfowitz alisema Benki ya Dunia inajivuna kuwa sehemu ya mafanikio yaliyopatikana Tanzania, na kwamba itakuwa tayari kuendelea kuisaidia serikali ya awamu ya nne katika utekelezaji wa vipaumbele vyake ilivyojiwekea.
Aliongeza kuwa Benki ya Dunia pia itakuwa tayari kuisaidia Tanzania kuandaa mapendekezo ya miradi ambayo Tanzania inatakiwa kuipeleka katika Millenium Challenge Corporation (MCC) ambayo ni taasisi ya Marekani, kwa utekelezaji.
Pia, akichangia hoja ya changamoto inayoikabili serikali ya kuibua ajira milioni moja katika kipindi cha miaka mitano, na ya kuongeza pato la mtu mmoja mmoja, Rais wa Benki ya Dunia alisema kuwa Tanzania inahitaji kuweka mikakati madhubuti ya kujenga na kuimarisha sekta za biashara za chini, za kati na za juu, ambazo alisema ndiyo hasa zitakazosaidia kuibua ajira.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisisitiza kuwa ili Tanzania iweze kujenga wajasirimali wadogo na wa kati inahitaji kuondoa urasimu usio wa lazima, urasimu ambao mtu anayetaka kuanzisha biashara humchukua siku zaidi ya 160 akihangaika kutafuta hati.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Rodrigo de Rato alisema kuwa IMF, kama ilivyo kwa Benki ya Dunia, inajivuna kuwa sehemu ya mafanikio ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.
Alisema kuwa IMF inafurahishwa zaidi kwa kuwa Tanzania sasa ina uwezo wa kujiamulia mambo yake na kumiliki kila hatua ya utekelezaji wa mambo mbalimbali yanayoihusu.
Rodrigo de Rato alisema IMF itaendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya nne katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Na katika kumdhihirishia Rais Kikwete kuwa IMF bado iko pamoja na Tanzania, Rato alimfahamisha kuwa katika siku chache zijazo wataalamu kutoka Shirika hilo na wa kutoka serikalini watakaa pamoja kujadiliana kuhusu miradi mipya ya Tanzania.
“Nataka nikuhakikishie kuwa tutaendelea kuwasaidia, na hasa katika uandaaji wa sera, na ili kukudhihirishia kuwa tuko nawe, siku chache zijazo, tutakaa kujadili miradi mipya,” alisema.
Pia, mkurugenzi huyo mtendaji wa IMF alisema kuwa shirika lake litashirikiana na serikali kukabili tatizo la nishati ya umeme.
Kwa upande wake, Rais Kikwete aliwashukuru watendaji hao kwa kumhakikishia kuwa watendelea kushirikiana naye.
Alisema kuwa yeye binafsi na serikali wamejiandaa vema kukabiliana na changamoto mbalimbali, kubwa zaidi ikiwa ya kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwawezesha pato lao kuongezeka.
Rais alisema anapokea ushauri aliopewa kutoka kwa watendaji hao kwa moyo mkunjufu, na kwamba kama walivyobainisha, hata yeye anaamini kuwa Tanzania bado ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi na kuwa nchi ya mfano.
Jana Rais alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kitabu kinachozungumzia utawala bora, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York.