Sambamba na hilo, upinzani umeitaka serikali itunge sheria mpya ya uhuru wa habari nchini, ili kulinda uhuru wa kuwasiliana, kusambaza na kupokea habari miongoni mwa Watanzania, kwa mujibu wa katiba ya nchi.
“Kuna baadhi ya sheria zinazoongoza sekta ya habari ambazo zimepigiwa kelele sana tangu serikali ya awamu ya pili, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa aidha, kuzifanyia marekebisho sheria hizi au kutunga sheria mpya kwa ajili ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari,” alisema Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni na Michezo, Grace Kiwelu jana alipowasilisha hotuba ya kambi ya upinzani bungeni.
Alizitaja baadhi ya sheria mbaya kuwa ni: Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976; Sheria ya Magereza ya mwaka 1967; Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970; Film and Stage Plays Act, 1976; na Sheria ya Mamlaka ya Mapato ya mwaka 1995.
Kiwelu alibeza mamlaka ya ‘kimungu’ ambayo sheria ya magazeti inampatia waziri mwenye dhamana ya habari, akasema serikali inaficha nia yake mbaya ya kudhibiti vyombo vya habari nyuma ya dhana ya ‘usalama wa umma.’
“Chini ya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, waziri anayehusika na habari na msajili wa vyombo vya habari (magazeti) wamepewa mamlaka ya juu sana kudhibiti vyombo vya habari kila anapohisi kwamba maslahi ya umma yako hatarini. Lakini pamoja na uzuri wa neno hilo ‘maslahi ya umma’, jamii ya Watanzania imekuwa ikishuhudia watawala wakiyafungia magazeti kwa hofu ya kuhatarisha maslahi ya umma ambayo hayakutafsiriwa.
“Hivi nani anayetoa tafsiri ya maslahi ya umma, anaweza kuachiwa tu mtu mmoja kazi hiyo bila hata kushauriwa na chombo chochote? Maamuzi mengine yanatia shaka kubwa kama kweli ni maslahi ya umma au kwa vile hakuna vigezo vilivyowekwa na wala vilivyo wazi. Ni dhahiri kuwa sheria hii hailindi maslahi ya umma bali kuficha uovu, huku serikali mara kwa mara ikivitisha vyombo vya habari kuwa vitafungiwa. Lakini serikali inasahau kuwa imeshikilia mpini wakati vyombo vya habari vimeshikilia makali,” alisema.
Kiwelu aliwatetea waandishi, akisema nia mbaya ya serikali ya kutorekebisha sheria ya magereza ndiyo ilisababisha waandishi na wapiga picha kupigwa, kwani kwa mujibu wa sheria hiyo, ni marufuku mtu yeyote kupiga picha maeneo ya magereza, au mfungwa, au kukaribiana nao mahali walipo.
“Kibaya zaidi sheria hii imetafsiri magereza kuwa ni popote alipo mfungwa. Kwa hiyo, hata mfungwa akitoroka akavamia maeneo ya watu, kwa mujibu wa sheria hii, hakuna anayeruhusiwa kujihusisha naye kumpiga picha wala kumhoji. Au askari akikutwa akimdhalilisha mfungwa hata mbele ya wapiga picha, wasichukuliwe picha? Hii ni kuifanya serikali ishiriki katika udhalilishaji na uovu. Sheria hii ni mbaya na inahitaji kufanyiwa marekebisho haraka sana.
“Ni kwa mujibu wa sheria hii, baadhi ya wanahabari walishambuliwa na kuumizwa vibaya na askari magereza waliotumia wafungwa kuwapiga mwaka jana. Katika hali iliyoonyesha utovu wa nidhamu na ukatili wa hali ya juu, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, aliwakebehi wanahabari kwa kipigo walichopata. Je, habari na manyanyaso ya mfungwa hayapaswi kujulikana kwa umma wa Watanzania?
“Kuonyesha kuwa sheria hizi hazifai. Ipo sheria ambayo sasa inavunjwa kila kukicha na imepoteza maana yake. Sheria hii inasisitiza kuwa, kupiga picha za aina yoyote kuhusu tukio lolote ni lazima mpiga picha apate kibali cha maandishi cha waziri anayehusika. Hakuna anayeruhusiwa kupiga picha za kumbukumbu yoyote ya kifamilia au tukio lolote la jamii bila kibali hiki. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 1976.
“Ni wangapi miongoni mwetu tumepiga picha hizo katika sherehe za kipaimara cha watoto, ubatizo au ndoa? Ni wangapi tumekuwa tunapiga picha kuweka kumbukumbu hata ya ushindi baada ya uchaguzi? Ni nani kati ya hao walifanya hivyo kwa kibali cha waziri anayehusika kama sheria inavyosema? Mheshimiwa Spika, sheria hii ipo na hata kwa utambuzi wa kawaida tu inaonyesha kuwa sheria hii haina maana kuendelea kuwepo,” alisema.
Alimtaka Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib, alieleze Bunge ni lini atawasilisha bungeni marekebisho ya sheria hizo ambazo zimepitwa na wakati na zinapingana na mantiki.
Kauli ya Kiwelu ni kilio cha siku nyingi cha wadau wa habari nchini, ambao kwa zaidi ya muongo mzima wamekuwa wakivutana na serikali juu ya umuhimu wa kufuta sheria hizo na kutunga nyingine mpya.
Kwa miaka kadhaa sasa, wanaharakati wa habari wameshirikiana na Tume ya Kurekebisha Sheria kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria alizozitaja Kiwelu, na kupendekeza kwa serikali, lakini serikali imekalia mapendekezo hayo.
Baadhi yao wamekuwa na matumaini makubwa kwa serikali ya sasa ya awamu ya nne, ambayo imekuwa ikijitambulisha na ukaribu wake kwa wanahabari, lakini wanasema sifa tu kwa wanahabari bila kuondoa mazingira magumu ya kazi yao, si ufumbuzi wa kero na kilio chao cha muda mrefu