SIKU moja tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kubeza filamu ya ‘Darwin’s Nightmare’, baadhi ya wakazi wa hapa wamesema maudhui yaliyomo hayapaswi kupuuzwa kwamba ni uongo.
Wamesema, hawamuungi mkono mtengenezaji wa filamu hiyo, Hubert Sauper, kwamba wakati mamilioni ya tani za minofu ya sangara zikiuzwa Ulaya, Watanzania wenye njaa hulazimika kula mabaki ya vichwa na mifupa, maarufu hapa kama mapanki; lakini wamemtaka Rais Kikwete achunguze kwa undani suala hilo, kwa kuwa lina ukweli mkubwa ndani yake.
“Kwa kuwa rais ameelewa jambo hili, akiwategemea walio chini yake watamwongoza vibaya. Tunaomba aanze kufanyia kazi uuzaji wa mapanki katika masoko tangu ya hapa jijini… mapanki yapo yananunuliwa na watu wengi; na si masikini wachache kama alivyosema rais… yapo Kabuhoro, Kirumba, Mabatini, Iloganzala, Ilemela na mahali pengine, yamezagaa sokoni, yanauzwa baada ya kuozea viwandani!” amesema mmoja wa wakazi hao.
Wakazi hao wameongeza kuwa, mamlaka zinazohusika hazikumwambia ukweli rais kuwa mapanki hayo huuzwa na wenye viwanda hata baada ya kuwa yameoza, na husafirishwa katika wilaya zote za Mwanza, na hata katika mikoa ya Mara na Kagera ambako wananchi huyatumia kama chakula na kitoweo kikuu.
Maoni hayo yamekuja, baada ya rais kusema juzi kuwa waliokutwa katika maeneo mbalimbali ya Mwanza wakikausha mabaki hayo ya sangara, walikuwa ‘waigizaji’ waliopewa ‘vijisenti’ na mtengenezaji wa filamu hiyo, miaka minne iliyopita.
“Kwa kuwa rais bado yuko Mwanza kwa mapumziko, ni vema akatembelea maeneo ya Nyamuhongolo, ajionee mwenyewe mapanki yanavyokaushwa tayari kuuzwa... na wala huu si uongo,” wamedai, wakitaka rais atumie mapumziko yake hapa Mwanza yanayoendelea hadi Jumapili kupata ukweli,” aliongeza mwingine.
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Nyamagana, wakati Sauper akiandaa filamu hiyo, Kapteni mstaafu Anasser Mkiwa, alipotakiwa na Tanzania Daima juzi kutoa maoni yake kuhusu hotuba ya rais, alisema: “Rais anataka tumpigie picha nyingine tumwonyeshe kuwa mapanki bado yanauzwa hapa katika masoko, na wala si masikini pekee wanaokula… Kwa kuwa ametuahidi maisha bora kwa kila Mtanzania, asiridhike kuwa ingawa hata Ulaya na Marekani kuna masikini, na Tanzania wawepo.
“Wawezeshwe kula hata dagaa badala ya mapanki; na serikali isijidai kukataa kila alichosema Sauper,” alisema Mkiwa.
Akizungumzia jinsi mauzo ya sangara yasivyowanufaisha wavuvi na wananchi wa Kanda ya Ziwa, alisema rais anapaswa kuanza kufanyia kazi tuhuma za mapato yanayotokana na kodi na tozo yasivyozinufaisha halmashauri.
“Hata Halmashauri ya Jiji la Mwanza inapata fedha kidogo mno kutokana na ushuru wa sh 7 kwa kila kilo moja ya samaki (landing fee); wahusika hawataki kuilipa halmashauri yetu ili imudu kuimarisha miundombinu yake au kuboresha maisha ya wakazi wake kiuchumi… watu bado ni fukara kwa sababu ya hujuma za wenye viwanda vya samaki,” Mkiwa alisema, huku akifananisha na hali ilivyo katika sekta ya madini, ambako pia wageni ndio wanaonufaika zaidi ya wazalendo.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi walipoulizwa na Tanzania Daima, kama viwanda vya samaki vilikuwa vimeuwezesha umma wa wakazi wa hapa kuondokana na umasikini, walisema kwa masharti ya kutotajwa majina, kuwa bado upo ubaguzi.
Wakati wageni hulipwa mishahara mikubwa na kupewa mikopo anuai, wazalendo wangali wakifanywa vibarua kwa miaka mingi viwandani humo, wakati mishahara yao haifiki hata nusu ya mishahara wanayolipwa wageni, hususan Waasia na Wazungu.
“Inawezekana kweli Sauper (mtunzi wa filamu hiyo) alipewa fedha na nchi za Scandinavia, ili kuharibu biashara ya sangara, lakini hata Nyamuhongoro mapanki yapo, na ni biashara za watu,” amesisitiza mwingine, huku akihoji: “Haya mambo hayapo? Suala la msingi tujiulize yapo kwa kiwango gani? Hawa si waigizaji.
Inawezekana rais ame - overreact baada ya viongozi wenzake wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kumuuliza mapanki… na wamemu - embarrass,” alisema Mkiwa.
Aliongeza kuwa, hata ukahaba unaosemwa, upo Makoroboi, Vitunguu (Soko Kuu), Barabara ya Posta na maeneo mengine, ingawa si sawa na Ulaya na Marekani. Tunaomba serikali iwaondoe machangudoa ambao hawafuati kanuni za kujikinga na UKIMWI, ikiwa ni pamoja na kupimwa mara kwa mara,” aliomba.
Rais Kikwete Jumapili alisema kwamba, madai ya wananchi kula mapanki na kuwapo ukahaba jijini Mwanza ni upuuzi na uzandiki. Na kwamba hata Ulaya na Marekani wapo wanaoimba barabarani “Change men! Change baby!” hata kiasi cha kuomba vijisenti vilivyobaki baada ya manunuzi kwa wanaume huku wakiwaita wanawake!
Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, mtu mmoja aliyemsaidia Sauper kutengeneza filamu hiyo, Jonathan Nathaniel (27) ameiambia Tanzania Daima kuwa anaomba Rais Kikwete “amkamate Sauper na kumrejesha nchini” ili awalipe fedha alizowaahidi kwa kazi waliyofanya.
Jonathan ni mtoto wa mitaani, ambaye sasa huishi kwa kuchora kadi za salamu na kuziuza kwa Wazungu. Katika fiamu hiyo, Jonathan anaonekana akielekeza jinsi watoto wa mitaani, hasa wa kike, wanavyovamiwa na wanaume nyakati za usiku na kubakwa.
“Mimi nilimfanyia kazi, lakini hakunilipa. Aliwanunulia watoto pipi na biskuti; kisha akapiga picha. Sikujua kuwa alitaka kwenda kutengeneza filamu ambayo angeiuza na kujipatia fedha nyingi hivi mgongoni kwetu,” alisema Jonathan.
Alidai kwamba, Sauper alipokuja nchini miaka takriban minne iliyopita, alijidai rafiki na kwamba angewasaidia, lakini wanasikia yupo Ufaransa na wakati mwingine Ubelgiji.
“Tunaomba akamatwe ili atulipe haki yetu, maana sisi tumeshiriki kama waigizaji, lazima tulipwe stahili zetu,” Jonathan alisema.
Juzi, wakati rais akihutubia, alisema alikutana na Sauper Ufaransa, lakini alitoweka bila kuaga baada ya rais kumtaka ushahidi wa kwamba ndege zinazochukua minofu na kuacha mapanki Mwanza, zinatumiwa kuingiza silaha kwa ajili ya kuvuruga nchi za Maziwa Makuu.
Suala la silaha kuingizwa nchini. Wengi waliohojiwa walisema haliwezekani kwani ndege zinapofika uwanjani huwa hazishushi nzigo wowote na badala yake hupakia samaki na kureja Ulaya.
“Wasichafue taifa letu. Ndege huwa zinatua na kuonadoka hatujaona mtu akishusha mzigo badala yake huwa wanapandisha samaki na kuondoka. Hilo hatulijui, ila la mapanki, Rais amechemka. Wasaidizi wake wamwambie ukwetu yaishe,” alisema mwingine.
Kwa Kanda ya Ziwa kula mapanki kimekuwa kilio cha miaka mingi na wavuvi wengi wamefilisika sasa kutokana na utaratibu wa watu wanaodai kuwa maafisa wa serikali kuwanyang’anya nyavu zao na kuzichoma moto wasivue sangara.
Wengine siku za nyuma zimekuwapo tuhuma kuwa wavuvi wamekuwa wakipigwa risasi kwa kukutwa wakivua samaki.
Huko Bukoba, inaelezwa kuna mtu anayeitwa Kayungi, amekuwa sawa na Mungu mtu. “Kayungi amefanya biashara ya samaki Bukoba ionekane kama biashara ya bangi. Watu siku hizi wanatumia mifuko miusi kubeba samaki kurejea majumbani mwao.
“Mtu huyu na wenzake wakikuta na samaki utafungwa kwenye gereza lao Kemondo, si chini ya miezi mitatu bila kupitia mahakamani. Nchi hii uhuru umepoteas, tumerejea nyuma katika haki za binadamu. Heri enzi za mkoloni hatukuzuiliwa kuvua samaki wetu,” alisema Rutashoba Rugahiyuluza aliyehojiwa kwa simu jana.
Alisema si aibu Rais kubaini kosa akalisahihisa, lakini kwa Bukoba mapanki yanakaribia kuwaua sasa na akaomba Kayungi atafutwe na kufanyiwa kazi kwani amekuwa Mungu mtu.