SERIKALI imezua mgogoro mwingine na madaktari kwa kufuta madaktari bingwa.
Tayari Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa tamko kwamba imefuta cheo hicho na haiwatambui, lakini wao wameilalamikia serikali kwa hatua hiyo.
Baada ya hatua hiyo ya serikali, wengi wao wako njia panda, huku wengine wakitafakari upya kuendelea na nafasi walizo nazo.
Katika waraka wa madaktari hao, ambao gazeti hili unao nakala yake, wanasema wana masikitiko makubwa juu ya hatua hiyo, hasa wakiwa wazalendo.
“Cha kushangaza zaidi ni kwamba, wizara imekuwa ikilidanganya bunge na wananchi kuwa, inasomesha madaktari bingwa ambao baada ya kumaliza masomo yao, wizara hiyo hiyo hubadilisha usemi na kuwaeleza kuwa haikitambui cheo hicho,” walisema.
Kinachogomba katika hili, ni madaktari ambao walitakiwa kuitwa mabingwa baada ya kusota darasani kwa miaka mitatu, kuishia kuitwa ‘waandamizi’, wakiunganishwa na wengine ambao hawakusomea shahada ya uzamili, bali wanapata uandamizi huo kutokana na uzoefu kazini.
Barua ya Wizara ya Afya ya Januari 17, mwaka huu, kwenda kwa mmoja wa madaktari waliokuwa wakitaka kubadilishiwa cheo, baada ya kupata sifa za kuwa daktari bingwa, ilieleza bayana kwamba cheo hicho kimefutwa.
“Nakiri kupokea barua yako ya tarehe 27 Desemba 2005 kuhusu somo tajwa hapo juu (kubadilishiwa mshahara). Kwa mujibu wa Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Na. 23 wa mwaka 2002, cheo cha daktari bingwa kimefutwa, hivyo hutabadilishwa cheo kuwa daktari bingwa, badala yake utapewa nyongeza mbili za mshahara wako wa sasa baada ya kuleta cheti chako cha kuhitimu shahada ya uzamili,” ilisema barua hiyo iliyosainiwa na N. Tawale, kwa niaba ya Katibu Mkuu.
Madaktari hao wanalalamika kwamba, wamelihangaikia suala hilo kwa muda mrefu, na baada ya ufuatiliaji huo, ndipo wakaambiwa cheo hicho kilifutwa.
Kabla ya mabadiliko hayo, daktari mwenye digrii ya kwanza alikuwa anasoma digrii ya uzamili (clinical) kwa miaka mitatu, kisha anatambulika kama daktari bingwa, halafu anapandishwa ngazi tatu za mshahara (vertical increase), kwa mfano, kutoka TGS 8 hadi TGS 11.
“Lakini baada ya mabadiliko hayo, daktari huyo haitwi daktari bingwa, bali anaitwa daktari mwandamizi (senior medical officer), cheo ambacho hata daktari ambaye hakusoma shahada ya uzamili ya miaka mitatu au zaidi hukipata kwa kukaa muda mrefu kazini.
“Tunaomba ieleweke kuwa, daktari bingwa ana ujuzi wa ziada ambao ameupata kutokana na masomo aliyosoma, ujuzi ambao hauwezi kupatikana kwa uzoefu kazini. Kwa sasa, daktari aliyekuwa akiitwa bingwa, hupewa nyongeza ya mshahara ya ngazi mbili na atasubiri nafasi ya daktari mwandamizi ikitangazwa, ndio aombe na kusailiwa na ngazi husika. Kama atafaulu usaili, ndio atapata hicho cheo.
“Tunao ushahidi kuonyesha kuwa, daktari huyo hukaa zaidi ya miaka mitatu bila kupewa cheo hicho, licha ya kufanya kazi kama daktari bingwa. Huu ni wizi wa taaluma na akili ya daktari na inakatisha tamaa kusomea udaktari bingwa, kwani hata tusiposoma tutakifikia hicho cheo tu.
“Taaluma ya udaktari yaweza kufananishwa na vyeo vya kijeshi, kwamba kuna masharti maalum ya kufikia cheo fulani. Kwa mfano, ili upate nyota moja lazima uwe na elimu fulani, na ni lazima upitie masomo yasiyopungua miaka mitatu ili uweze kuwa bingwa katika fani husika. Haiingii akilini kuona kuwa daktari anadhulumiwa haki hiyo, swali ni je, kuna haja ya kusomea fani hii wakati haitambuliki?” walihoji.
Muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu, madaktari waligoma, wakitaka waongezwe maslahi, ili yalingane na unyeti wa kazi wanayofanya, mazingira magumu ya kazi na mafunzo ya muda mrefu wanayosoma. Serikali haikukubaliana nao, ikaamua kuwasimamisha, kisha baadhi wakafukuzwa na wengine wakarejeshwa kwa karipio kali.
Wanaleta malalamiko hayo, wakati Rais Jakaya Kikwete ndiyo kwanza ametoa msamaha kwa madaktari mahiri 29 waliokuwa wamefutwa kazi kutokana na mgomo huo.
Madaktari hao walisema kwamba, katika utafiti waliofanya kujua kwanini cheo hicho kimefutwa, waligundua kuwa serikali iliipa kila wizara wasaa wa kurekebisha muundo wa utumishi wa idara zinazoangukia chini yake. Kwa kutumia wataalamu wake, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilipeleka mapendekezo Utumishi, yakaridhiwa na serikali.
“Tuligundua kuwa wataalamu wengi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii si madaktari bingwa, bali wengi wao wana Shahada ya Uzamili ya Afya ya Jamii (MPH) ambayo husomwa kwa mwaka mmoja. Kabla ya mabadiliko haya, hawakuwa wanatambuliwa kama madaktari bingwa, bali walikuwa wanapewa nyongeza mbili za mishahara (horizontal increase) na walikuwa wanalalamika kwa nini nao wasitambuliwe na kupewa nyongeza kama wenzao waliokuwa wanasoma kwa miaka mitatu au zaidi.
“Tunalazimika kuamini kuwa, kwa sababu wao ndio washauri wa wizara, walifanya mabadiliko haya kwa sababu binafsi na si kwa maslahi ya wadau wa sekta ya afya. Cha kushangaza zaidi, wakati serikali inasema haitambui cheo cha daktari bingwa, ukienda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), cheo hiki kinatambulika na wanalipwa na serikali hiyo hiyo. Tena mshahara wa daktari mliyemaliza wote (siku moja) masomo, akiajiriwa Muhimbili anapokea takriban sh 300,000, zaidi ya zile utakazolipwa wewe uliyeajiriwa na Wizara ya Afya.
“Hii ni dhahiri kuwa, madaktari watafanya kila linalowezekana kuajiriwa MNH kwa ajili ya maslahi zaidi. Pia serikali iliamua kuwapandisha mshahara waganga wakuu wa wilaya, ambao kitaaluma aidha ni madaktari wasaidizi (AMO), madaktari wenye digrii moja au wenye MPH, kwa sababu ni wakuu wa idara (watawala). Mishahara yao ni zaidi ya sh 150,000 ukilinganishwa na huyu daktari bingwa anayenyanyaswa.
“Hii inatupa hisia kuwa, madaktari tusomee utawala ili tulipwe vizuri kuliko kusomea kutibu wagonjwa! Je, wananchi wa mikoani watatibiwa na nani? Au madaktari wakikimbilia nchi za nje kutafuta maslahi, bado watalaumiwa kwa kukosa uzalendo?
“Hebu tuangalie suala la maslahi. Wenzetu wenye shahada ya uzamili ya afya ya jamii, wao ni watawala, wakuu wa miradi, wakuu wa vitengo, husafiri mara kwa mara ndani na nje ya nchi na kujipatia masurufu mengi. Huyu daktari mwenye shahada ya uzamili (clinical) ndiye hukutana na wagonjwa moja kwa moja, hana masurufu yoyote na anapunjwa hata hicho kidogo anachostahili.
“Hivi kuna madaktari bingwa wangapi huko mikoani ukiondoa Dar es Salaam? Kwa nini serikali isiwatambue madaktari hawa bingwa na kuwalipa kama inavyowalipa wenzao wa Muhimbili?
“Ni suala jepesi sana kutambua kuwa iwapo madaktari hawa hawatatambuliwa na kulipwa vizuri, aidha watakimbilia kuajiriwa Muhimbili au watakimbilia nchi zinazowatambua na kuwalipa vizuri. Tutabaki kila siku kulalamika hatuna wataalamu wa afya, kumbe tunao wengi, lakini hatuwajali na tunawatumia vibaya.
“Daktari huyu anakesha wodini, chumba cha upasuaji akihudumia wananchi kwa taaluma hiyo serikali isiyoitambua, ni uzalendo gani serikali inataka madaktari waonyeshe?
“Machungu haya ndiyo hupelekea kudai haki zetu kwa migomo. Tumechoka kugoma, tunaamini Waziri wa Afya ambaye pia ni daktari bingwa atacheza midundo ya ari mpya na kasi mpya kurekebsha kasoro hizi,” walisema madaktari hao.
Tanzania Daima ilifika wizarani zaidi ya mara tatu jana, lakini awali wahusika hawakuwapo, lakini baadaye ofisa uhusiano aliyepatikana, alisema maswali haya yanahitaji ofisa mwandamizi au Katibu Mkuu, ambaye jana alikuwa bungeni, katika mkutano unaoendelea wa bajeti