Kwa msingi huo, elimu ni kitu muhimu kwa mtu yeyote, ikiwa anahitaji maendeleo. Nchi zote zilizoendelea zimefika zilipo kutokana na elimu.
Pasipo elimu, katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia na utandawazi, asiyekuwa na elimu huachwa nyuma, huku wenye nayo wakichuma, wakionekana wajanja na wajinga wakibaki nyuma.
Tanzania nayo si kisiwa. Haiwezi kubaki pasipo elimu. Imekuwa katika mchakato wa kuwapatia raia wake elimu, lakini ukweli ni kwamba, kadiri muda unavyokwenda, elimu zaidi inahitajika, lakini pia uwezo wa kuipata unapungua kwa watu wengi.
Kama nchi, inatakiwa kuwaelimisha watu wake, ili waweze kushindana na wale wa jirani na hata wa mbali, katika ushindani mkubwa uliopo kwenye soko la ajira na pia la bidhaa.
Ukweli ni kwamba, bidhaa zinazotengenezwa kwa kutumia sayansi na teknolojia zaidi, hushika bei kubwa, tofauti na zilizotengenezwa kiujanja ujanja tu, pasipo elimu. Hata huduma zinazotolewa na walioelimika, ni za kuvutia, tofauti na za wasio na elimu.
Hayo yote yamewasukuma Watanzania kubuni mambo mengi, kwa ajili ya kuinua elimu, kupambana na adui ujinga, ambaye huishi na mapacha wenzake; umaskini na maradhi, na sasa rushwa na ufisadi.
TEA ni kifupi cha Tanzania Education Authority, au kwa Kiswahili Mamlaka ya Elimu Tanzania.
Ni mamlaka iliyoanzishwa kwa ajili ya kutafuta vyanzo zaidi vya fedha, kugharimia elimu nchini.
Mercy Sila, ni Mkurugenzi Mkuu wa TEA, na anasema kwamba, ilivyo sasa, kuna mzigo mkubwa wa kugharimia elimu nchini, kutokana na gharama zilizopo, wananchi kutoweza kuzimudu, na pia ufadhili kupungua.
Sila anasema kwamba, TEA imeanzishwa, ili kuwaleta pamoja watu wenye mapenzi mema wanaotaka kuchangia elimu, ikijulikana kwamba, awali hapakuwapo mfumo kama huo, hivyo hata waliotaka kuchangia iliwawia vigumu.
Upo Mfuko wa Elimu Tanzania, ambamo fedha hutolewa kwa njia tofauti, kusaidia Watanzania kupata elimu, iwe ni kwa msaada au kwa mkopo.
“TEA imeanzishwa kutokana na kuwapo watu wenye mapenzi mema kutaka kuchangia elimu, na hapakuwapo utaratibu au utaratibu wenyewe haukuwa mzuri,” anasema.
Anaongeza kwamba, mamlaka katika shughuli zake za siku kwa siku, inalenga kuboresha elimu, kuongeza nafasi za vijana katika elimu na kuleta usawa wa kijinsia, ili kuona kwamba wavulana na wasichana ambao wapo karibu sawa kwa wingi, wanakwenda sawa pia katika elimu.
Kwa maana nyingine, ni kuona watoto wa kike nao wanakuja juu, wanakwenda shule, wanafanya vizuri na kupata haki yao, kama ilivyozoeleka kwa wavulana. Ndiyo kusema, mamlaka inajenga mazingira mazuri ya kumwezesha mtoto wa kike kusoma.
Mazingira ambamo mtoto wa kike anaweza kusema haogopi, hatishwi wala hakwazwi kusoma, bali anafurahia na kuona fahari kwenda shule, akijua faida zake, kama ilivyo kwa wavulana.
Kadhalika, TEA inajaribu kujenga usawa kielimu kati ya watu wenye viungo kamili na wale wenye ulemavu kwa namna moja au nyingine. Mamlaka inataka kuondoa kipingamizi chochote kinachoweza kumfanya mwenye ulemavu asisome, eti kwa sababu tu ya upungufu katika viungo vyake.
Vivyo hivyo, Mamlaka hii ya elimu, inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwa na uwiano kwenye elimu kimikoa, isiwe kwamba mkoa fulani tu ndio unaopata elimu na watoto wa mikoa mingine wanabaki nyumbani na kugeuka kufanya kazi za kutumia musuli, huku wa mikoa mingine wanatumia akili kutokana na kwenda shule.
Kumbe basi, kazi ya TEA ni kujaribu kukusanya rasilimali fedha, kutoka maeneo mbalimbali, na kuitumia tena katika maeneo tofauti, lakini wakisaidiwa wale wasiokuwa na uwezo.
Ukweli ni kwamba, pato la taifa haligawanywi sawa, kuna wanaopata zaidi na wengine kidogo kutokana na sababu mbalimbali. Na kwa msingi huo huo, wale wenye nacho wana uwezo mkubwa wa kusomesha watoto wao, wakati wasio nacho wakiwa na nafasi finyu.
Ni kwa sababu hiyo, wananchi wanahamasishwa, kutoa kwa moyo wala si kwa sababu ya utajiri, kwa sababu wapo wenye nacho wasiotoa, lakini pia wapo wasiokuwa nacho, lakini hata kile kidogo walichonacho wanatoa kusaidia wengine.
Na wananchi wanaweza kutoa chochote; kwa hali na mali, ili kusaidia kukuza elimu. Sila anasema kwamba, wananchi wanaweza kutoa hata mahindi, maharage au chochote walichonacho, kinachoweza kugeuzwa katika fedha, na kisha kugharimia elimu.
Watoaji wanaweza pia kutoa fedha taslimu, ambazo zinawekwa kwenye mfuko, na kisha kugawanywa kwa watu au taasisi mbalimbali, chini ya utaratibu maalumu uliowekwa.
Lakini pia, wafadhili wanaweza kutoa vifaa vya elimu moja kwa moja. Wanaweza kutoa vitabu, madaftari, samani kama vile madawati, meza au hata kugharimia ujenzi wa majengo tofauti yanayohitajika kwenye shule au taasisi mbalimbali za elimu.
Ieleweke kwamba, TEA inashughulika na kuboresha elimu kuanzia shule za awali, shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi, taasisi, vyuo vya elimu ya juu na vyuo vikuu katika ukubwa wake wowote.
Kumbe TEA ni ya wote, na inalenga kusaidia wote katika namna yoyote ile, ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri kwa wanaohitaji, na kuona kwamba kuna ongezeko la udahili.
Sila anasema, kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo, upungufu mkubwa wa fedha na vifaa kwa ajili ya elimu, TEA inalazimika kujiuliza iende wapi na ifanye nini, kitakacholeta majibu na ufumbuzi wa matatizo yote hayo.
TEA ina kazi ya kufanya upembuzi yakinifu, na kwa kushirikiana na wadau katika nafasi husika, wanafunzi na taasisi mbalimbali ziweze kupata vifaa vya kufundishia, vitabu, maabara, vifaa kwa ajili ya teknolojia ya mawasiliano, ikitumika zama hizi za sayansi na teknolojia kama njia ya kujifunzia.
Ipo kazi pia ya kubadili mitaala ili iendane na mahitaji halisi ya wanafunzi watakapokuja kuhitimu, na si kusoma tu ilimradi, hata kama kitu hakiji kuonekana kwenye kazi atakazokuja kufanya baadaye.
Lakini pia, kazi nyingine kubwa ni kuwajengea uwezo zaidi walimu, ili wapande ngazi au madaraja, waongezeke ubora na wawe wazuri zaidi katika kuwafundisha wanafunzi, ili kusudi wanafunzi nao waelewe kwa urahisi zaidi. Kwa kifupi ni kulenga kuwa na walimu bora kabisa, na si kuwa na bora walimu