RAIS Jakaya Kikwete amebeza utengenezwaji na usambazaji wa filamu inayoipaka matope Tanzania na kulenga kuhujumu biashara ya samaki katika Ziwa Victoria.
Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Mwanza katika Ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mjini Mwanza jana jioni, Rais alisema filamu hiyo iitwayo ‘Darwin’s nightmare’, iliyotengenezwa na Hubert Sauper, raia wa Ufaransa, inaeleza mambo ya uongo.
Alizitaja tuhuma zilizo kwenye picha hiyo; kwamba ndege zinazokuja kuchukua samaki zinaleta silaha ambazo husambazwa katika nchi za Maziwa Makuu, minofu yote ya samaki inauzwa nje na wananchi wanaachiwa kula vichwa vya samaki vilivyooza (mapanki), na kwamba mji wa Mwanza umejaa makahaba, mambo aliyosema ni ya uongo.
Rais alikiita kitendo cha Sauper kuwa ni cha uzandiki, na kwamba filamu hiyo ilionyeshwa mara ya kwanza Oktoba mwaka jana mjini Paris, Ufaransa, ambapo Ubalozi wa Tanzania huko, ulitoa tamko la kushutumu, lakini, Sauper aliendelea kueneza uongo Uingereza kisha Ujerumani.
“Moja ya uongo wa wazi uliomo kwenye filamu hiyo ni yale madai kwamba ndege zinazokuja kuchukua minofu ya samaki hapa Mwanza eti huleta silaha ambazo hutumika kuchochea migogoro katika nchi za Maziwa Makuu.
“Wazee wangu, huu ni uongo na uzushi mtupu ambao hauna hata chembe moja ya ukweli. Isitoshe hakuna popote katika filamu hiyo anapothibitisha madai hayo zaidi ya simulizi za watu wanafiki. Kwa bahati nzuri Mwezi Mei mwaka huu nilikutana na mtengenezaji wa filamu hii, Bwana Hubert Sauper, mjini Paris, Ufaransa…nilimuomba anipatie ushahidi wa madai yake kuhusu uingizaji wa silaha nchini. Alishindwa kabisa kufanya hivyo. Badala yake aliona aibu, akakimbia bila hata ya kuaga.
“Baada ya filamu hiyo kutoka, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimefuatilia tuhuma hizo na hakuna ukweli wowote uliothibitika. Nimewataka wafanye tena ili kama kuna mahali popote hawakugusa au kupaona, na kazi inaendelea. Lakini, hata kabla ya filamu hiyo kulikuwepo na madai ya namna hiyo ambayo yalishafuatiliwa.
“Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote inayothibitisha kuwapo kwa vitendo hivyo viovu hapa Mwanza. Labda katika uchunguzi wa marejeo, kama itabainika ni kweli. Napenda kuwahakikishia wana - Mwanza, Watanzania wenzangu na jumuiya ya kimataifa kwamba habari za kuwapo biashara ya silaha katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza si kweli. Ni habari za uongo zinazozushwa na kuenezwa na watu wasioitakia mema Tanzania,” Rais alisisitiza.
Alisema kwamba, Tanzania haitaruhusu ardhi yake itumike kuleta machafuko nchi jirani, na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vipo makini kuhusu uingizaji na usafirishaji wa silaha nchini, akasema yaelekea filamu hiyo imefadhiliwa na watu wasioitakia mema Tanzania.
Kuhusu makahaba, alisema katika nchi za Ulaya, ukahaba ni biashara, tena inakatiwa leseni, kwa hiyo akashangaa kuona kwamba inaelezwa kuwa Mwanza kuna ukahaba, jambo alilosema pia si la kweli.
Katika hatua nyingine, Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Maura Mwingira, alisema jana katika taarifa yake kwamba, mgeni rasmi katika maadhimisho ya sherehe za wakulima za Nanenane, ni Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, na si Rais Kikwete, kama taarifa yake ya jana ilivyokuwa imesema. Rais ana mapumziko Mwanza hadi Agosti 6.