ASKARI polisi zaidi ya 1,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini, wanatarajiwa kwenda masomoni Agosti mwaka huu, imefahamika.
Wanaokwenda kupata mafunzo zaidi, ni pamoja na shujaa aliyepambana na majambazi waliopora fedha za Benki ya NMB, Sajenti Solomon Mwangamilo.
“Watakwenda kusomea vyeo mbalimbali kulingana na viwango vya elimu walivyonavyo, lakini kwa Sajenti Solomon, yeye anatarajiwa kusomea u-meja,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Orodha ya majina ya askari waliobahatika kuingia katika mpango huo yalitarajiwa kutangazwa kuanzia jana jioni katika kila mkoa, ili hadi kufikia leo wahusika wawe na taarifa kwa ajili ya kujiandaa.
“Watapewa siku kama tano za kujiandaa, kwa kuwa katika siku hizo watakuwa wameshapata mishahara yao, hivyo siku hizo zinatosha kujiandaa.
“Kozi ni miezi mitatu, kwa hiyo baada ya kutangazwa wanatarajiwa kuripoti chuoni wiki moja baada ya kupata taarifa (wiki ya pili ya Agosti),” kilisema chanzo hicho.
Nafasi hii ya masomo inajumuisha askari waliopandishwa vyeo na Rais Jakaya Kikwete, baada ya kufanya kazi nzuri.
“Idadi hii ya askari ni kubwa na mpango huu ulikuwapo, lakini sasa wanakwenda baada ya Bunge kupitisha bajeti yetu,” chanzo hicho kilihitimisha.
Kumekuwapo mikakati mingi ya kuliboresha Jeshi la Polisi, kwa kuliongezea zana, na sasa inaonekana wanawekeza pia elimu kwa wahusika, ili wawe watendaji mahiri. Kulifanyika pia upanguaji wa makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya na maofisa wengine wa ngazi mbalimbali.