Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kashfa nzito CCM
Kashfa nzito CCM
By Habari Tanzania | Published  08/1/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Charles Mullinda

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza wanadaiwa kuhujumu mapato ya chama hicho na kujihusisha na vitendo vya mauaji.


Wanadaiwa kutumia vibaya mamilioni ya fedha za chama hicho, kabla na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni wa mwaka jana.


Pia wanadaiwa kuhusika na kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa kijana wa kikundi cha ulinzi wa chama hicho kijulikanacho kama Green Guard, Babangida.


Vyanzo vya habari kutoka ndani ya uongozi wa CCM Mkoa wa Mwanza, vimelieleza Tanzania Daima kuwa Katibu wa Chama wa Mkoa, Mujuni Kataraia, anaongoza na watu ambao hawasaidii ipasavyo kulinda mali za chama.


Vimeeleza kwamba tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, utaratibu wa kawaida wa utoaji taarifa za fedha za chama ulibadilika, kwa kubadili ratiba za vikao vya kamati ya siasa ya mkoa, na kupunguza muda wa kamati hiyo kukutana.


Taarifa zaidi zimedai kuwa, Kataraia kwa kushirikiana na wasaidizi wake, wamekuwa wakitumia fedha za vitega uchumi vya chama hicho kwa masilahi yao binafsi na kwamba wanamiliki biashara mbalimbali katika majengo ya chama hicho.


Imedaiwa kuwa, sehemu kubwa ya mapato ya Uwanja wa CCM Kirumba na yale yanayopatikana kutoka katika ofisi zilizopangishwa za jengo la makao makuu ya chama hicho mkoani Mwanza, zinatumiwa na viongozi hao kinyume cha taratibu.


Aidha, Kataraia anadaiwa alipangisha wafanyabiashara wa mbao katika eneo linalozunguka Uwanja wa CCM Kirumba waliokuwa wakimlipa kodi ya kufanya biashara katika eneo hilo. Hata hivyo, inasemekana kwamba, kodi hiyo haikuwa ikifika katika hazina ya chama.


Taarifa zinaeleza kuwa, wafanyabiashara hao walikwishaondolewa eneo hilo kwa amri ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kupelekwa eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya kufanyia biashara ya mbao.


Kataraia pia anadaiwa kukiuka taratibu za ununuzi zilizowekwa na CCM katika ununuzi wa magari mawili ya chama wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.


Inadaiwa kuwa alichukua fungu kubwa la fedha lililochangwa na wafadhili katika harambee iliyoendeshwa na Rais Jakaya Kikwete na kwenda nje ya nchi ambako alinunua magari mawili aina ya Land Cruiser, bila kupata kibali cha vikao husika cha kufanya ununuzi huo.


Kataraia, pia anatajwa kuwa mmoja wa viongozi wa chama hicho aliyesababisha kupotea na baadaye kuibuka madai ya kuuawa kwa Babangida.


Baadhi wa vijana wa chama hicho, wameliambia gazeti hili kuwa Babangida alitumwa na Kataraia kutoka Makao Makuu ya CCM Mwanza kwenda Wilaya ya Ukerewe kupeleka barua.


Kwamba, alipoondoka hakuonekana tena na baadaye zilipatikana taarifa kuwa amefariki dunia, hata hivyo mpaka sasa mwili wake haujapatikana, na baba yake mzazi amekuwa akihangaika kwa mashirika ya misaada na haki za binadamu bila mafanikio yoyote hadi sasa.


Taarifa zaidi zinadai kuwa, siku chache kabla ya kutumwa wilayani Ukerewe, Babangida alikuwa na msuguano na baadhi ya viongozi wa mkoa, hivyo kupotea kwake kunaweza kuwa kulipangwa.


Akizungumza kwa simu kutoka Mwanza, Kataraia alisema hawezi kuzungumzia tuhuma za ubadhirifu wa mali za chama zinazomkabili katika vyombo vya habari.


“Malalamiko hayo yapo, lakini siwezi kuyazungumzia katika vyombo vya habari, nikifanya hivyo nitakuwa ninawajibika sehemu mbili, jambo linaloweza kuniletea matatizo.


“Tuhuma zote hizo nilikwishazitolewa ufafanuzi katika kamati ya siasa ya mkoa, tulikuwa na kikao Juni 5, mwaka huu, nilitoa taarifa na tunafanya kingine Agosti 3, kama kuna jambo la kutolea maelezo nitatoa huko, sifanyii kazi kwenye magazeti,” alisema Kataraia.


Alisema kubadilika kwa ratiba kwa vikao vya chama vya mkoa kunategemea na majukumu waliyonayo viongozi, na kuongeza kuwa kamati ya siasa ya mkoa imekuwa ikikutana kwa muda mfupi, kutokana na mpangilio mzuri wa ajenda na maandalizi mazuri ya ripoti zinazojadiliwa na kamati hiyo.


“Kamati ya Siasa ya Mkoa inakutana kwa muda mfupi kwa sababu ajenda zinakuwa zimepangiliwa barabara, ripoti zinazowasilishwa zinakuwa za kitaalamu na zimepangiliwa vizuri, hapo kwa nini wajumbe wakae muda mrefu?” alihoji Kataraia.


Kuhusu madai ya kuhusishwa kwake na kifo cha Babangida, alikiri kumtuma kijana huyo kupeleka barua wilayani Ukerewe, lakini zaidi ya hapo alisema hajui.


“Nilimtuma kiofisi, kilichotokea baada ya yeye kuondoka sijui, na hili jambo nalo siwezi kulizungumzia kwa sababu liko polisi, waulizeni hao kwa nini limechukua miaka yote hii bila kutolewa taarifa.


Kataraia alisema madai ya kuwapo mgawanyiko au wanachama kutishana kwa silaha za moto au kutishiwa kuuawa hayapo na hayajawahi kutokea, akasisitiza kwamba CCM Mwanza ni shwari.
Kauli hiyo ya Kataraia inapingana na taarifa za migogoro ya mara ya mara inayoambatana na vitisho ambayo imekuwa ikiibuka ndani ya chama hicho mkoani Mwanza.


Mwaka jana wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Katibu Mwenezi wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Simon Mangelepa, alidai kutishiwa kwa bastola na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Joseph Yared.


Hivi karibuni Mweka Hazina wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Samson Maganga, naye alilalamika kutishiwa kuuawa na watu wasiofahamika


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.