Waziri Mkuu Bw Edward Lowassa, amesema Serikali imeongeza bajeti ya mbolea ya ruzuku kutoka Sh. bilioni saba mwaka jana hadi kufikia Sh. billioni 21 mwaka huu kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula.
Bw. Lowassa amesisitiza kwamba, Serikali itahakikisha kwamba, mbolea hiyo inafikishwa vijijini na kuwafikia wakulima bila vikwazo vya aina yoyote.
Aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Matai, Wilaya ya Sumbawanga akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Rukwa ya kukagua shughuli za maendeleo.
Aidha, Waziri Mkuu aliwaambia wananchi hao Serikali msimu huu itaongeza akiba ya chakula katika hifadhi ya Taifa (SGR) kutoka kiwango cha tani 150,000 cha sasa na kwamba kuanzia Agosti Mosi SGR itaanza kununua mazao kwa wakulima ili kupata chakula cha kutosha katika akiba yake.
Bw. Lowassa alisema hatua hii ya Serikali ni moja ya mikakati ya kupambana na nguvu ya soko hivyo ametoa wito kwa wananchi kuacha kuuza mazao yakiwa bado shambani.
Katika ziara yake hiyo kijiji cha Matai, Waziri Mkuu alizindua barabara ya kutoka Matai, Kalalasi hadi Itekesha yenye urefu wa kilomita 26.5 iliyojengwa na Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya masoko ya mazao ya kilimo (AMSDP) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Pia Waziri Mkuu alizindua mfumo wa stakabadhi ghalani ambao utaiwezesha SACCOS ya Matai kununua mazao kutoka kwa wakulima kwa kutumia stakabadhi hizo ambazo ili kutekeleza mfumo huo Benki ya CRDB ilitoa mkopo wa Tsh. Milioni 25 kwa ajili ya SACCOS hiyo.
Waziri Mkuu pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko la kisasa lenye uwezo wa kuchukua tani 35 kwa siku za nafaka linalojengwa na programu hiyo ya AMSDP lenye thamani ya Sh. 127.9.
Bw. Lowassa katika hotuba yake hiyo alisisitiza kuwa, sera ya CCM inataka wananchi wajenge tabia ya kujitegemea na kwamba kazi kubwa ya Serikali ya awamu ya nne ni kutekeleza kwa vitendo, ufanisi na figa ilani hiyo hili wananchi waishi maisha bora apate huduma mbalimbali za kijamii zilizo bora