Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Maofisa mpaka wa Mtukula wadaiwa kufukuza raia
Maofisa mpaka wa Mtukula wadaiwa kufukuza raia
By Habari Tanzania | Published  07/31/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Baadhi ya maofisa wa taasisi mbalimbali za Serikali waliopo Mtukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda, wamelalamikiwa kwa vitendo vya unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi.

Hali kadhalika, maofisa hao wamedaiwa kuwafukuza nchini baadhi ya wananchi kwa madai kwamba si raia.

Madai hayo yalitolewa na Bi. Ndasoro Haule mbele ya Kamati ya Biashara, Uwekezaji na Mawasiliano ya Bunge la Afrika Mashariki.

Kamati hiyo inatembelea vituo vya ushuru wa forodha vya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa Ushuru wa Pamoja ulioanza kutumika Januari, mwaka jana.

Akielezea mkasa huo wake, Ndasoro Haule ambaye mama yake ni Mtanzania na baba Mganda.

Hata hivyo, alilelewa na mama yake baada ya baba yake kuitelekeza familia hiyo ambapo baadaye yeye aliolewa na Mtanzania, Bw Joseph Haule.

Bi. Haule alisema kwa sasa ametimuliwa nchini na maofisa hao wa serikali kwa maelezo kuwa si raia wa Tanzania.

Akielezea kwa masikitiko juu ya mkasa huo mbele ya Kamati hiyo, Bi. Haule alisema chanzo cha yeye kutimuliwa kilitokana na mtoto wake wa kiume kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mmoja ambaye pia alikuwa na uhusiano kama huo na mmoja wa maofisa hao wa serikali.

Alidai kuwa, baada ya ofisa huyo kubaini hilo, ndipo alipomfuata nyumbani kwake na kumpa vitisho kuwa watakiona cha mtema kuni.

Alidai kuwa, baada ya kupita siku nne, alifuatwa nyumbani kwake na polisi wakiwa katika gari aina ya Defender na kupelekwa kituo cha polisi cha Rusumo.

Kwa mujibu wa Bi. Haule, akiwa kituoni hapo, askari wa kiume walimfanyia upekuzi sehemu zote za mwili, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Alisema baadaye alilazimishwa kusaini karatasi ambayo hakujua kilichokuwa kimeandikwa kwa kuwa hajui kusoma wala kuandika.

”Hata nilipowahoji wanieleze kilichoandikwa, niliambulia kipigo na ndipo nilipolazimika kusaini hivyo hivyo,” alidai.

Aliongeza kuwa, siku iliyofuata, yeye na motto wake walichukuliwa na gari ya polisi wa Tanzania na kwenda kukabidhiwa kituo cha polisi cha Uganda eneo la Mutukula na kuelezwa kuwa karatasi aliyosaini ilikuwa ni ya kupigwa marufuku kuishi nchini kwa kuwa siyo raia.

Hata hivyo, alisema hata nchini Uganda pia walikataa kumpokea kwa kuwa hana ndugu yeyote.

Mwanamke huyo ameliomba Bunge la Afrika Mashariki, kufikishia kilio chake na cha mamia wengine ambao hawajapata pa kusemea.

Mwenyekiti wa Kamati ya Biashara, Uwekezaji na Mawasiliano ya Bunge la Afrika Mashariki, Bw George Nangale, (Tanzania),alisema, ingawa mkasa huo hauhusiani na ziara yao, lakini kutokana na uzito wa shutuma na tuhuma mbalimbali za unyanyasaji zinazodaiwa kufanywa na maofisa wa Forodha, Uhamiaji na Polisi, watayafikisha malalamiko hayo katika ngazi zinazohusika ili yafanyiwe kazi.

Ziara hiyo ya Kamati ya Biashara, Uwekezaji na Mawasiliano ya Bunge la Afrika Mashariki, iliyodhaminiwa na Shirika la Friedrich Ebert Stiftung, mwishoni mwa wiki ilitarajia kutembelea mpaka ya Tanzania na Kenya eneo la Namanga.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.