Watu kumi wanaodhaniwa kuwa ni majambazi sugu wamejikuta wakitua mkononi mwa polisi kiulaini baada ya kupita kizuizini usiku usiku na ’zana zao za kijambazi’ bila kujua vijana wa kazi hawalali usingizi.
Watuhumiwa hao wapatao kumi wamedakwa wakiwa na magari mawili pamoja na silaha moja aina ya SMG yenye namba BD 354983 ikiwa na risasi 26 pamoja na ganda moja la risasi iliyotumika.
Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga, Isaya Mngulu amesema watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa kuamkia jana kwenye kizuizi cha Polisi Kituo cha Kabuku wilayani Handeni.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Hamza Athumani, 21, Ali Hamad,18, Bakari Shabani,35, waliokuwa wakitumia gari lenye nambari T 235 AJD aina ya Toyota Mark II iliyokuwa ikiendeshwa na Hamza Athumani.
Wengine wametajwa kuwa ni Fred Mchome, 24, Daud Emmanuel,36, Omari Rajabu,38, Kondo Ayubu,42, na Abbas Mwanamboka,38, waliokuwa kwenye gari lenye namba za usajili T 814 AGQ aina ya Toyota Corolla ikiendeshwa na Fred Mchome.
Kamanda Mngulu amesema magari ya watuhumiwa hao yalisimamishwa kwenye kizuizi hicho na baada ya kupekuliwa yakakutwa na silaha hiyo pamoja na risasi.
Pia amesema ndani ya magari hayo kulikuwa na nguo nyeupe pamoja na kofia yenye nembo isiyojulikana vyote vinavyofanana na sare za askari wa usalama wa barabarani.
Amesema katika upekuzi zaidi polisi waligundua kuwa katika shati hilo kuliandikwa namba D. 30156 ambazo kwa mbali zinaonekana kama ni za askari polisi.
Hata hivyo Kamanda Mngulu amesema makachero wa polisi wamebaini kuwa namba hizo hazijasajiliwa kwa askari yeyote wa majeshi ya ulinzi na usalama hapa nchini.
Aidha amesema watuhumiwa hao walipatikana na vibao viwili vya magari vinavyoonyesha namba ya chases ya gari jipya zinazofungwa kwenye gari ambalo halijasajiliwa vikionyesha namba AE 1003195915 pamoja na mkanda wa sare ya JWTZ, tochi moja pamoja na kisu.
Kamanda Mngulu amesema kuwa polisi wamebaini kuwa watuhumiwa hao ni miongoni mwa wale wanaotafutwa kwa tuhuma za utekaji nyara magari ya abiria na ya mizigo yakiwemo matanki ya mafuta yanayosafirishwa na kupora bidhaa na mali mbalimbali za abiria kwenye maeneo ya mikoa ya Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Aidha, amesema kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakitokea Jijini Dar es Salaam ambapo inaonekana walifanya matukio ama majaribio ya uhalifu kutokana na kupatikana na ganda moja la risasi ya silaha ya aina hiyo.
Amesema wanawasiliana na Interpol ili kuweza kujua kama nambari za magari hayo ni halali ama ni za bandia.
Amewaomba wahanga mbalimbali wa matukio ya ujambazi katika barabara kuu za Morogoro, Kilimanjaro na Pwani kuwasiliana na Polisi Mkoa wa Tanga ili kupata maelekezo zaidi na kwenda kuwatambua watuhumiwa na mali zilizoporwa.