Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wabunge wamjaribu Kikwete
Wabunge wamjaribu Kikwete
By Habari Tanzania | Published  07/28/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Oscar Mbuza, Dodoma

WABUNGE wamemwomba Rais Jakaya Kikwete, kuwaachia mara moja wafungwa waliohukumiwa kunyongwa ambao
wamekaa muda mrefu Magereza bila hukumu zao
kutekelezwa.

Katika hatua nyingine, Wabunge wa Upinzani, wamemtaka
Rais kuwafikisha mahakamani viongozi waliohusika katika kashfa ya wizi wa sh. bilioni 2, katika Ubalozi wa Tanzania, nchini Italia.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala, kuhusu utekelezaji wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2005/2006 na makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007,
Mjumbe wa Kamati hiyo, Bi. Pindi Chana, alisema Kamati
hiyo imemwomba Rais kuwaachia wafungwa hao.

“Kamati imepokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri wa
Kamati uliotolewa katika kipindi cha mwaka 2005/2006,
ushauri huu ulikuwa ukiiomba Serikali ifuatilie tatizo la wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo na ikiwezekana imshauri Rais atoe msamaha kwa watu waliokaa muda mrefu gerezani badala ya kuwaacha waishi katika hali hiyo,” alisema Bi. Chana.

Alisema pamoja na ushauri huo, Kamati hiyo ilitoa
mapendekezo pia kwa Serikali, kutafuta ufumbuzi wa
kudumu wa tatizo la ukosefu wa usafiri kwa mahakimu na
ikiwezekana kutafuta wakopeshaji wenye masharti nafuu
ili iwakopeshe vyombo vya usafiri na pia Serikali
iboreshe maslahi yao.

Awali akisoma hotuba yake, Waziri wa Sheria na Katiba,
Dkt. Mary Nagu, alisema Serikali imedhamiria kuboresha
sekta ya sheria na katiba kwa kuwa na Sera ya Mahakama
inayolenga kusogeza huduma za mahakama karibu na
wananchi.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, Serikali inakusudia
kuwa na Jengo la Mahakama Kuu katika kila mkoa,
kujenga Mahakama ya Hakimu Mkazi katika kila mkoa,
kuwa na Jengo la Mahakama ya Wilaya katika kila wilaya
na ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo katika kila tarafa.

Aidha, Dkt. Nagu alisema Serikali inakusudia kuwasilisha bungeni hivi karibuni, Muswada wa Sheria ya kumfanya
Mtanzania kuwa na haki ya kuwa na uraia wa nchi mbili.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2005/2006, Mahakama
Kuu, ilitoa uamuzi kuhusiana na matukio mbalimbali kama kufuta vifungu vya Katiba, vyenye masharti yanayoelekeza kwamba wagombea wa kiti cha urais na ubunge wawe wanachama na wawe wamependekezwa na chama cha siasa.

Alisema Mahakama hiyo pia imefuta vipengele katika Sheria ya Uchaguzi, vilivyokuwa vinaruhusu matumizi ya
takrima katika kampeni za uchaguzi na ilifuta kipengele katika Sheria ya Uchaguzi kilichokuwa kinaruhusu uchaguzi mdogo kufanyika baada ya miaka miwili.

Alisema hata hivyo, Serikali imechukua hatua ya kukata
rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kufuta
masharti ya mgombea kuwa mwanachama na
aliyependekezwa na chama cha siasa na utaratibu wa
kuendesha uchaguzi mdogo.

Dkt. Nagu alisema aidha Serikali inafanya uchambuzi
ili kuwa na mapendekezo ya Sheria inayoweka utaratibu
wa kisheria juu ya kugharimia kampeni za uchaguzi,
ambao hautapingana na Sheria ya Rushwa, ili kutekeleza
uamuzi huo wa Mahakama.

Alisema ili kuongeza ufanisi katika Sekta ya Sheria na
hivyo kuboresha utoaji huduma kwa wateja na wananchi
kwa ujumla, Wizara ya Sheria na Katiba, imetenga
bajeti kwa ajili ya kuteuliwa majaji 20 katika mwaka
huu wa fedha.

Alisema ongezeko hilo la majaji pamoja na mikakati
mingine, vitasaidia kupunguza kesi zilizopo Mahakama Kuu zinazosubiri kusikilizwa.

Naye Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba, Bi. Fatma Maghimbi, alisema ni lazima Serikali itoe maelezo kutokana na taarifa za kutokea kwa wizi wa kughushi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia wa sh. bilioni 2.

Alisema wizi wa kughushi kwa lugha ya kisheria ni
‘forgery’ na si ‘corruption’ na alisema kambi ya
Upinzani inataka ufafanuzi ili kufahamu ni kwa nini
tuhuma za wizi huo zimepelekwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) badala ya kufikishwa mahakamani.

“Kambi ya Upinzani pia inataka Serikali iwaeleze
Watanzania majina ya wahusika kutoka katika Wizara za
Fedha, Miundombinu, Mambo ya Nje na mtu aliyekwenda
kupatana ili kufanya ununuzi wa nyumba nchini Italia.

Wakati huo huo, Waziri Nagu, aliliomba Bunge kuidhinisha
jumla ya sh. 66,849,887,000 kwa ajili ya utekelezaji
wa majukumu ya wizara hiyo kwa kipindi cha mwaka wa
fedha wa 2006/2007, na kwamba kati ya fedha hizo, za
matumizi ya kawaida ni sh. 50,027,746,000 na za
maendeleo ni sh. 16, 822,141,000.


Wakati huo huo, Eliya Mbonea anaripoti kuwa Jaji Augustine Shangwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, amepangwa kusikiliza kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Professa Costa Mahalu, dhidi ya Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Bw. Reginald Mengi, akidai magazeti yake yalichapisha habari za uongo dhidi yake.

Kesi hiyo namba 104 ya mwaka huu, ilifunguliwa hivi karibuni, ambapo Profesa Mahalu anaiomba Mahakama Kuu imwamuru Bw. Mengi amlipe fidia ya sh. bilioni 12 kwa madai ya kumchafulia jina na rekodi yake safi katika utumishi.

Katika kesi hiyo anayowakilishwa na Kampuni ya Uwakili ya Adili, mdai anataka Mahakama pia imwamuru mshitakiwa akanushe habari hizo zilizochapishwa kwenye magazeti na kutangazwa kwenye vituo vya redio na televisheni vinavyomilikiwa na Bw. Mengi.

Pamoja na mshitakiwa huyo wa kwanza, Profesa Mahalu amewaunganisha pia waandishi wa habari, Bi. Furaha Thonya, Bw. Mbaraka Islam, wahariri wa magazeti ya This Day na Kulikoni na Kampuni ya The Gurdian Limited na Media Solution ambao ndio wachapishaji.

Profesa Mahalu, anadai kulipwa kiasi hicho kutokana na habari zilizochapishwa na magazeti hayo katika matoleo tofauti zikidai alifuja sh. bilioni mbili mali ya Serikali ya Tanzania na kuziweka kwenye akaunti binafsi Ufaransa.

Katika hati ya madai aliyoiwasilisha mahakamani hapo, Prof. Mahalu ameeleza jinsi ununuzi wa jengo la ubalozi ulivyoanza mwaka 2001, baada ya kuombwa kufanya hivyo na Serikali.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana mahakamani hapo zilidai tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo itapangwa na

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.