Na Oscar Mbuza, Dodoma
WABUNGE wa CCM na wa Kambi ya Upinzani, wameungana na kummwagia sifa kemkem, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, wakisema ni mwadilifu, mkakamavu na anayeweza kupambana na majambazi.
Maoni ya Wabunge kuhusiana na utendaji wa IGP Mwema, yalianza kutolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, iliyosomwa na Mbunge wa Namtumbo, Bw. Vitta Kawawa (CCM), ambaye alisema ni IGP Mwema mwenye uwezo mkubwa wa kubadili sura ya Jeshi la Polisi.
“Pongezi mahususi ni kwa IGP Mwema, kutokana na ujuzi na uzoefu wake wa muda mrefu katika Jeshi la Polisi ndani na nje ya nchi, kamati inaamini kuwa ataendelea kutekeleza majukumu ya Jeshi hili kikamilifu na kwa
uadilifu,” alisema Bw. Kawawa.
Alisema kamati hiyo ya Bunge inapongeza pia hatua ya Serikali ya kuanzisha kanda maalumu ya Polisi ya Dar es Salaam, ambayo imeongeza ufanisi katika kukabiliana na wimbi la uhalifu, hatua ambayo alisema imerejesha imani ya wananchi kwa polisi.
“Ni imani na matumaini ya Kamati yangu kuwa juhudi zitaongezwa zaidi hadi kuutokomeza kabisa uhalifu uliokuwa ukishamiri siku hadi siku, siku chache zilizopita,” alisema Bw. Vitta.
Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Usalama wa Raia, Bw. Muhammad Ibrahim Sanya, alisema uteuzi wa IGP Mwema ni wa busara kuwa na uliozingatia vigezo vyote ambavyo hutakiwa IGP kuwa
navyo.
Bw. Sanya ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mji Mkongwe kupitia CUF, alisema uteuzi wa IGP Mwema, umekuja wakati muafaka kutokana na haja ya kuwa na kiongozi wa Jeshi la Polisi wa aina hiyo.
“IGP tuliyenaye amejengeka vyema kitaaluma, kimafunzo,
kinidhamu sambamba na kazi zake yeye mwenyewe
anaonekana ni mkakamavu.
“Mheshimiwa Spika, mgema mara nyingi akisifiwa sote tunaelewa matokeo yake, hivyo mimi binafsi na kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, tunamtakia IGP Mwema, autumikie umma wa Watanzania kwa kheri na mafanikio
makubwa ili kurejesha matumaini mapya,” alisema Bw. Sanya.
Pamoja na mambo mengine, Bw. Sanya alisema suala la ulinzi na usalama kwa upande wa Zanzibar ni la utatanishi, kwa vile wimbi la ujambazi limepania kuhamia Zanzibar baada ya kuona kwaamba Jiji la Dar es Salaam lina ulinzi madhubuti na kuwanyima nafasi ya kufanya uhalifu.
Naye Waziri wa Usalama wa Raia, Bw. Bakari Mwapachu, alisema baada ya mabadiliko ya uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi, wananchi na wadau wengine wamejenga imani na kuwa na matarajio makubwa na Polisi, hatua ambayo alisema ni lazima IGP Mwema akaijua, ili kutowaangusha wananchi.
Alisema hatua hiyo inatoa changamoto kwa Jeshi, kuboresha huduma zake kwa kuwa karibu na wananchi, kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na Haki za Binadamu, kujiepusha na vitendo vya rushwa na askari kufika mapema kwenye eneo la tukio.