Na Oscar Mbuza, Dodoma
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Samwel Sitta, amewacharukia viongozi wa Serikali, wanaodharau wabunge na kukosoa mawazo na maoni wanayotoa katika mikusanyiko mbalimbali ya kijamii.
Katika hatua nyingine, Spika Sitta, amemwagiza Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa, kufuatilia na kutoa taarifa ya kiini cha ugomvi uliotokea hivi karibuni baina ya Mbunge wa Sumve, Bw. Richard Ndassa (CCM) na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Bw. Elias Maarugu.
Bw. Ndassa na Bw. Maarugu waliripotiwa na vyombo vya habari juzi na jana kuwa waligombana baada ya Mkuu huyo wa Wilaya, kumkatisha Bw. Ndassa, aliyekuwa akiwapa wananchi salamu za wabunge, wakati wa hafla ya kupokea Mwenge wa Uhuru katika jimbo hilo.
Spika Sita, alisema pamoja na kuwa bado haijajulikana kiini cha ugomvi huo, lakini kitendo hicho ni cha aibu kwa Serikali na ni vizuri kwa Waziri Mkuu, kufuatilia ili kujua chanzo na baadaye kutoa adhabu kwa mhusika.
Alisema katika siku za karibuni amekuwa akipokea malalamiko ya wabunge wakidai kunyanyaswa au kupuuzwa na baadhi ya viongozi wa Serikali wanapotoa mawazo au ushauri na alisema kumdharau mbunge ni sawa na kulidharau Bunge.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbunge ni kiongozi mwenye heshima na anapaswa kuheshimiwa na viongozi wote wa Serikali, ni marukufu na kosa kisheria, kwa kiongozi wa Serikali kumdharau mbunge kwa maneno au vitendo,” alisema Spika Sitta.
Alisema kuanzia sasa, Bunge halitakaa kimya pale litakapopata taarifa za mbunge kudharauliwa au kutendewa jambo lolote lisilo la kistaarabu na
kiongozi wa Serikali, na kuongeza kuwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa.
“Naomba kama kitatokea kitendo kama hicho na chanzo kikawa ni mbunge, basi taarifa zifikishwe kwangu mara moja ili mbunge huyo aweze kushughulikiwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maadili,” alisema Spika Sitta.