*Jeshi la Polisi kuundwa upya, IGP kupunguziwa madaraka
*Madereva wa mabasi makubwa ya abiria kujaribiwa upya
*Vikosi maalumu kuanzishwa ili kulinda watalii na mabenki
*Sheria kutungwa kuzuia kuzungumza na simu ukiendesha
Na Oscar Mbuza, Dodoma
SERIKALI ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupambana na uhalifu, ajali za barabarani na kulijenga zaidi Jeshi la Polisi.
Waziri wa Usalama wa Raia, Bw. Bakari Mwapachu,
alitangaza mabadiliko zaidi katika kukabiliana na
vitendo hivyo, wakati alipowasilisha Makadirio ya
Matumizi ya Fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka
2006/2007, bungeni jana.
Waziri Mwapachu alisema baada ya muundo wa Wizara ya
Usalama wa Raia kuidhinishwa, hatua inayofuata sasa,
ni kuangalia upya muundo na mfumo wa Jeshi la Polisi
ili kuliwezesha kukabiliana na uhalifu.
Alisema upo mpango wa kupunguza zaidi watendaji
wanaoripoti moja kwa moja kwa Inspekta Jenerali wa
Polisi (IGP), ili kutawanya madaraka katika kanda kwa
ajili ya kupunguza urasimu, kuharakisha uamuzi na
kubwa zaidi kumpa IGP muda wa kutosha kufikiria maandalizi ya mipango ya mikakati ya kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi hasa katika kupambana na majambazi.
Waziri Mwapachu alisema Kanda Maalumu ya Polisi ya Dar
es Salaam, ni kama ya majaribio na kwamba itakapofanya vizuri, zitaanzishwa kanda nyingine na makamanda wa mikoa wa kanda husika wataripoti kwa Kamishna wa Kanda Maalumu, badala ya kuripoti kwa IGP kama ilivyo sasa.
Aidha, alisema wizara hiyo pia inakusudia kulifanyia
maboresho Jeshi la Polisi ili muundo na mfumo wake, uwe
imara kutoka ngazi ya makao makuu hadi ya kituo
cha Polisi, ikiwa ni pamoja na kugawa madaraka na
rasilimali husika mikoani, wilayani na vituoni.
“Baadhi ya sheria na kanuni za Jeshi la Polisi, zimepitwa na wakati na zinahitaji kufanyiwa marekebisho, kwani hazijazingatia kikamilifu haki za binadamu na hata askari wa kawaida ndani ya Jeshi lenyewe. Lengo ni kuziboresha ili ziendane na wakati na zisikwamishe utendaji wa Jeshi,” alisema Waziri Mwapachu.
Akizungumzia ongezeko la matukio ya ajali za barabarani, Waziri Mwapachu alisema Wizara ya Usalama wa Raia, inatarajia kupendekeza marekebisho ya baadhi ya Sheria za Usalama Barabarani, ikiwamo Sheria ya Leseni.
Alisema kuanzia sasa madereva wa magari makubwa, hasa
mabasi ya abiria, watalazimika kujaribiwa upya ili kupima uwezo wa kuendelea kubeba roho za watu na kwamba sifa zinazotakiwa ili mtu aruhusiwe kuendesha mabasi ya abiria zimepitiwa upya na leseni daraja la C inayoruhusu madereva kuendesha magari yote, sasa itatumika kwa kuendesha mabasi ya abiria tu.
Aidha, Waziri Mwapachu alisema Serikali itabadili
leseni za udereva, ili zifanane na za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
ambapo katika mabadiliko hayo, leseni mpya sasa
zitakuwa mfano wa kadi za benki ambazo si rahisi
kughushiwa na madereva hasa wa mabasi ya abiria.
Alisema Serikali pia itawasilisha sheria ya kushitaki wamiliki wa magari, madereva, makondakta na abiria wanaozidi kwenye mabasi, sheria ya kuwaadhibu madereva na makondakta wanaowanyanyasa wanafunzi na watu wasio na uwezo na sheria ya kuzuia magari kuwekwa vioo vya giza (tint).
Alisema sheria nyingine ni ya kuzuia madereva kuendesha magari wakati wanaongea na simu za mkononi na sheria ya kuruhusu taasisi za Serikali, kampuni binafsi na magereji yenye uwezo kukagua magari kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kudhibiti magari mabovu.
Alisema katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu na
uhamiaji haramu, Serikali sasa itakuwa na vikosi maalumu vya kudhibiti matukio hayo ambapo sasa, kitaanzishwa kikosi maalumu kwa ajili ya ulinzi wa watalii, kikosi maalumu kwa ajili ya ulinzi na usalama kwenye vituo vya kuingilia nchini na kikosi maalumu cha kupambana na majambazi katika benki na vyombo vya fedha.
Aidha, Waziri Mwapachu alisema ujambazi wa kutumia
silaha bado ni tatizo kubwa ambalo linachangiwa kwa
kiasi kikubwa na kuzagaa kwa silaha, hivyo Jeshi la Polisi litazikagua, kuziorodhesha na kuzisajili upya, silaha zote za kiraia nchini ili kuhakiki umiliki na matumizi yake.