MAMIA ya wananchi jijini Dar es Salaam, jana walijitokeza katika viwanja vya Mnazi Mmoja, kushuhudia maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa waliopigana vita kwa ajili ya kutetea uhuru wa taifa hili.
Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Rais huyo alikuwa mgeni rasmi kutokana na Rais Jakaya Kikwete kuwa ziarani nchini Ujerumani, Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuwa bungeni mjini Dodoma wakati Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Shein, yupo nchini Uingereza kwa matibabu.
Rais Karume alianza kwa kuweka mkuki na mshale katika mnara wa mashujaa kama ishara ya silaha za jadi zilizokuwa zikitumika wakati wa vita ya ukombozi.
Naye Mkuu wa Majeshi, George Waitara aliweka sime katika mnara huo, Mwenyekiti wa chama cha Askari Wastaafu (Tanzania Legion), naye aliweka shoka.
Balozi wa Libya nchini, Bashiri Bashiri alifuata kwa kuweka shada la maua kama ishara ya kumbukumbu kwa mashujaa waliokufa, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa pia alipata fursa ya kuweka upinde na mshale.
Katika kumbukumbu hiyo, askari walipiga mizinga miwili kama heshima na kumbukumbu kwa mashujaa waliokufa kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inakuwa huru.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta; Naibu Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Ali Juma Shamuhuna; Rais mstaafu Benjamin Mkapa; Spika wa Bunge wa zamani, Pius Msekwa, Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba; Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wa dini.