JESHI la Israel limesema kuwa askari na vifaru vyake vimefanikiwa kuutwaa mji wa mpakani unaoaminika kuwa ngome ya kundi la Hezbollah na ambao umekuwa ukanda wa vita kali tangu jeshi la nchi hiyo lilipokitwaa kijiji cha Maroun al-Ras, Jumamosi iliyopita.
Baada ya mapambano makali hatimaye inaaminika idadi isiyojulikana ya wapiganaji wa Hezbollah wameukimbia mji huo.
Pamoja na jeshi la Israel kuendelea na operesheni nzito, wapiganaji wa Hezbollah wamekuwa wakiendelea kujibu mashambulizi kwa kurusha maroketi aina ya Katyusha katika miji ya kaskazini mwa Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice amefanya mazungunzo mjini Yerusalemu na Waziri Mkuu wa Israel, Ehud Olmert katika juhudi za kutafuta suluhu za mgogoro huo nchini hapa.
Wakati mazungumzo hayo yakianza, Olmert alisema kuwa hataachana na kampeni ya kutaka kuwatokomeza wapiganaji wa Hezbollah.
Olmert alisema kuwa amesikitishwa na kuguswa na hali mbaya ya kibinadamu inayowapata raia wa Lebanon, lakini alisisitiza kuwa inachofanya nchi yake ni kujilinda dhidi ya magaidi.
Wakati huo huo mji wa tatu kwa ukubwa wa Israel, Haifa, jana umeendelea kupigwa na maroketi kadhaa kutoka Lebanon na imeripotiwa watu 30 wamejeruhiwa kutokana na mashambulio hayo jana.
Watu saba wa familia moja nchini hapa wakiwamo watoto wawili waliuawa katika shambulio la anga la Israel lililoendeshwa usiku wa kuamkia jana kwenye mji wa Nabatiyeh.
Olmert alisema kuwa Israel haiko katika vita na watu wa Lebanon, bali na wapiganaji wa Hezbollah ambao aliwaeleza kuwa ni magaidi na alionya kwamba Israel itachukua hatua kali zaidi dhidi ya kundi hilo.
Wachambuzi wa mambo walisema kuwa Rice hakutegemewa kuishinikiza Israel iache operesheni yake nzito ya kijeshi wakati wa mazungumzo yake na kiongozi wa Israel.
Mhariri wa masuala ya kidunia wa Shirika la Habari la Uingereza, BBC, John Simpson, aliyeko hapa alisema kuwa ilishafahamika kwamba Rice angeiambia Israel kwamba Marekani inaruhusu muda zaidi wa kuendelea na operesheni za kijeshi.
Rice hata hivyo aliitaka Israel itambue mahitaji ya kibindamu ya watu wa Lebanon na Palestina.
“Watu wa eneo hili la Israel, Lebanon, na hususan Palestina kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi kwa hofu na shaka kubwa inayotokana na machafuko yasiyokwisha,” alisema na kutaka malengo ya muda mrefu kukomesha hali hiyo yachukuliwe.
Rice alitarajia kukutana na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas baadaye jana.
BBC