SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imepiga marufuku wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwenda shuleni wakiwa na simu za mkononi kwa lengo la kudhibiti mmong’onyoko wa maadili.
Hayo yametangazwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman, wakati akifunga mjadala wa bajeti yake katika mwaka wa fedha 2006/07 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi.
Alisema kwamba vitendo hivyo vinaleta usumbufu kwa walimu wanapotekeleza majukumu yao darasani, lakini pia vinashawishi uvurugaji maadili katika maeneo ya shule.
Waziri alisema yeye mwenyewe binafsi amekwisha chukua hatua ya kuwakataza watoto wake kwenda na simu shuleni.
“Kuanzia sasa ni marufuku kwa wanafunzi kuchukua simu za mkononi wanapokwenda shule,” alisema Waziri Haroun.
Hatua hiyo ya serikali imefikiwa baada ya wajumbe wengi wa kambi ya upinzani kuzungumzia suala hilo na kuhoji wanafunzi hao wanapata wapi simu za thamani na kumudu kuzihudumia wakati hawana ajira.
Wawakilishi hao walisema inashangaza baadhi ya wanafunzi wanamiliki simu zenye laini mbili, ambapo moja kazi yake ni kupokea mawasiliano ya kifamilia na nyengine mambo ya mapenzi.
Mwakilishi wa Jimbo la Tumbe, Mohammed Bakar, alisema imefika wakati serikali lazima ichukue hatua juu ya jambo hilo kwa vile zinaweza kuwavuruga kisaikolojia wanafunzi na kuchangia maadili kuvurugika.
Aidha Waziri Haroun alisema wizara hiyo imeanza kushughulikia tatizo la nauli za walimu kuwa hazilingani na viwango vinavyotumiwa na wamiliki wa gari za abiria zikiwamo daladala.
Alisema wizara yake inakusudia kuwasilisha mapendekezo serikalini na kuwataka walimu wawe wastahamilivu juu ya suala hilo.
Waziri huyo alisema wizara yake itazifanyia ukaguzi shule zote binafasi ili kujua kiwango chake cha ubora na sifa za walimu kwa sababu baadhi ya shule hizo zinafunguliwa katika maeneo ambayo hayana sifa yakiwamo makazi binafsi.
Hata hivyo alisema sekta binafasi imeonesha mafanikio makubwa Zanzibar na inatoa mchango mkubwa kukuza elimu visiwani.
Akizungumzia suala la serikali kusitisha mkataba wa kazi na mtaalamu wa mambo ya historia, Dk. Abdulkadir Sherif, Waziri Haroun alisema serikali ilichukua hatua hiyo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wake wa kiutendaji.
Alisema serikali ilimpa notisi mtaalamu huyo kuondoka wakati serikali ikiwa inamuhitaji.
Wakati huo huo, Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai aliwataka wajumbe wa Baraza hilo kuacha tabia za kibaguzi zinazoweza kuvuruga umoja wa kitaifa.
Akichangia bajeti ya wizara hiyo ya elimu, Nahodha alisema inasikitisha baadhi ya wajumbe hawawezi kupita dakika mbili bila ya kuzungumzia kauli za umajimbo na maeneo