WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema kutokana na kutoimarika vyama vya siasa nchini, kumekosesha ushindani wa kweli wa kisiasa nchini.
Akifungua Mkutano wa 14 wa Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), katika Ukumbi wa Nkrumah, Dar es Salaam jana, Lowassa alisema licha ya vyama hivyo kushindwa kujipanua, pia vimekuwa vikikumbwa na migogoro inayovidhoofisha.
“Demokrasia yoyote duniani inayohusisha wananchi, inajengeka kwa kuwa na vyama imara vya siasa, kwani ndivyo vinavyoamsha watu kushiriki katika masuala ya siasa, huku vikilea na kufunza viongozi wa baadaye,” alisema Lowassa.
Alisema uchaguzi wa mwaka 1995, 2000 na 2005 chini ya mfumo wa vyama vingi, umetoa fundiso la kuhakikisha kunakuwapo upanuzi wa demokrasia ndani ya nchi na ndani ya vyama vyenyewe.
Alisema kwa kipindi cha miaka 14 tangu kurejeshwa kwa mfumo huo, utawala wa sheria umeendelea kuimarika, lakini bado kuna upungufu mdogo mdogo unaostahili kufanyiwa kazi haraka.
Aliutaja upungufu huo kuwa ni pamoja na wa vitendea kazi katika vyombo vya utoaji wa haki, na watumishi wenye sifa pamoja na vitendea kazi.
Lowassa alisema tatizo jingine linalowakumba wananchi wengi ni kutojua haki zao za msingi, jinsi ya kuzidai kisheria na gharama kubwa za kuendesha kesi.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hali ya ustawi wa vyama vya siasa bado ni ndogo kutokana na kukandamizwa na serikali.
“Sisi hatuwezi kupiga hatua kubwa kama wapinzani, kwani tumekuwa tukibanwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kila kunavyokucha na hili liangaliwe kwa makini,” alisema.
Naye, Profesa Horoub Othman, akiwasilisha mada yake iliyohusu Katiba, Sheria na Uchaguzi wa Tanzania, alisema Katiba ya nchi inapaswa kufanyiwa marekebisho ya haraka.
“Juu ya kwamba Katiba ya Muungano imetiwa ‘viraka vingi’ hata kukaribia kupoteza rangi yake ya mwanzo, bado haikidhi mfumo wa vyama vingi nchini, huku baadhi ya viraka hivyo vinapingana na makubaliano ya Muungano,” alisema Profesa Othman.
Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kufungwa leo.
Unahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, wabunge, wawakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, madiwani na wasomi mbalimbali.