Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Ugomvi wa DC, mbunge wakolea
Ugomvi wa DC, mbunge wakolea
By Habari Tanzania | Published  07/26/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Magu, Dk. Festus Limbu, amemwomba Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa, amsamehe Mkuu wa Wilaya (DC) ya Magu, Elias Maarugu, kwa kitendo chake cha kumdhalilisha mbele ya hadhara.

Dk. Limbu, akizungumza na Tanzania Daima kwa simu, alisema kwa miaka mitano ambayo amemjua DC huyo, hakushangaa kusikia amemtolea Ndassa maneno yasiyofaa.

“Namuomba Mheshimiwa Ndassa amsamehe, namjua DC huyo kwa miaka mitano, sikushangaa kusikia maneno aliyomtolea mheshimiwa mbunge,” alisema.

Mwishoni mwa wiki, asubuhi katika Kijiji cha Nyabore, Kata ya Nkungulu wilayani Magu, Ndassa anadaiwa kukorofishwa na DC huyo wakati viongozi na wananchi wa Wilaya ya Magu wakipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa viongozi wa Wilaya ya Kwimba.

Ndassa alipandwa hasira baada ya Maarugu kuingilia kati hotuba yake, na kutoa maneno yaliyomuudhi.

Wakati akiwashukuru wananchi, Ndassa alisema wabunge wa majimbo mawili yaliyopo wilayani Magu - Busega na Magu - hawakuhudhuria sherehe hizo kutokana na majukumu mengine ya kitaifa.

Kwa sababu hiyo, Ndassa alisema ametumwa na wabunge hao ili afikishe salamu kwa niaba yao.

Maarugu aliposikia hivyo, ndipo alipomkatiza kwa kusema: ‘Endelea bwana, hiyo ni kazi ya Spika na wewe siyo Spika.”

Maneno hayo yalimuudhi mno Ndassa. Akiwa amemwelekea Maarugu, akauliza: “Wewe ni nani unayeingilia mazungumzo yangu? Hivi kumbe huna adabu kiasi hiki! Chunga sana, mdomo wako utakuponza, huo mdomo endapo utaendelea kuutumia hovyo hovyo hivyo.”

Ndassa aliendelea kumtaka DC huyo kuwa na staha na adabu kwa kuheshimu itifaki wakati wa shughuli za kitaifa.

Maarugu alipoona mambo yanaelekea pabaya, alisema: “Samahani sana, mheshimiwa kama nimekukosea nisamehe, naomba.”

Aliomba msamaha huku akijishika tumboni na kuinama, kama dalili ya kuungama kosa alilotenda.

Kwa tukio hilo, Ndassa alipandisha hasira, akaamua kukatisha hotuba yake.

Baadaye alizungumza na waandishi wa habari na kusema: “Nimechukizwa na kuropoka kwa Maarugu, nimeamua nimpasulie kasoro yake mbele ya watu ili kama anaweza, ajirekebishe kwa sababu hawezi kuutumia vizuri mdomo wake.

“Mimi nimetoka bungeni jana, na nimeonana na wabunge wote wawili, wameniambia niwaletee wananchi wao salamu na kueleza sababu za kushindwa kwao kushiriki mbio za Mwenge, halafu ninaambiwa kuwa hiyo ni kazi ya Spika.”

Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alikuwa akitarajia kusafiri nje ya nchi kwa shughuli za kikazi.

Kwa upande wake, Ndassa alipohojiwa jana na Tanzania Daima kwa simu, alieleza kukerwa mno na kauli ya DC huyo.

“Aliniudhi sana, hana mamlaka ya kunidhalilisha mbele ya wananchi, amemdhalilisha hata Mheshimiwa Spika kwa sababu Spika hawezi kuzuru majimbo ya wabunge wanaokuwa hawapo majimboni kwao kutokana na majukumu mengine ya kitaifa au kimataifa.

“DC huyu ni jeuri, na lazima ajifunze kufunga mdomo wake,” alisema.

Kwa upande wake, Maarugu, alizungumza kwa simu na Tanzania Daima, jana asubuhi na jioni na kueleza kwamba hakutoa maneno yaliyoandikwa.

 “Hivi kweli sina akili? Mimi niseme maneno hayo kweli?” alihoji.

Hata hivyo, Maarugu ana kawaida ya kukanusha kila linalomsibu. Mwaka jana alikataa kupigwa na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kuwakuta barabarani wakiwa na sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baada ya kukanusha habari hizo, baadaye ilikuja bainika kuwa kweli ‘alikunjwa’, kwani alikwenda kufungua kesi mahakamani, akilalama kupigwa na wafuasi hao. Kesi hiyo inaendelea.

Kuna habari kwamba amepanga kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kuzungumzia sakata lake na Ndassa, katika kile kinachoonekana ni kutaka kujisafisha


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.