VIONGOZI wakuu wa nchi 11 za eneo la Maziwa Makuu, wanatarajiwa kusaini itifaki ya kuanzishwa kwa Baraza la Habari la eneo hilo.
Hatua hiyo ya kihistoria inatarajiwa kufanyika Desemba, mwaka huu, wakati wa mkutano wa viongozi hao utakaofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania, Balozi Liberata Mulamula, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga umoja na kumaliza matatizo yanayolikabili eneo hilo.
Kuridhiwa uanzishwaji wa Baraza hilo ni moja ya mafanikio ya utendaji kazi wa Balozi Mulamula na wasaidizi wake ambao walipewa dhima hiyo.
Tayari wizara hiyo imeanza mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau wa habari, na jana alizungumza na baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Mkutano huo ulifanyika ofisini kwake, Dar es Salaam.
Kuanzishwa kwa Baraza hilo ambalo linapendekezwa liwe na wajumbe 11, ni matokeo ya mkutano wa wakuu wa nchi za eneo la Maziwa Makuu uliofanyika mwaka 2004 jijini Dar es Salaam.
Kila nchi itatoa mjumbe mmoja, na uwakilishi wao utakuwa wa kijinsia. Bado inatafutwa njia murua ya kuwa na uwiano huo.
Pamoja na mambo mengine, wakuu hao waliona umuhimu wa kushirikisha vyombo vya habari katika suala zima la kumalizwa kwa vurugu na mateso mengi yanayowakabili wananchi katika eneo hilo.
Mulamula alisema vyombo vya habari vina nafasi ya kuhimiza utawala bora, elimu ya uraia, mapambano dhidi ya umasikini ambao pia ni chanzo kikuu cha migogoro, kuhimiza suala zima la amani na maendeleo.
Katika itifaki hiyo, Kiswahili kinatajwa kuwa moja ya nyenzo muhimu za kujenga umoja katika eneo la Maziwa Makuu.
Mwaka 2004, wakuu wa nchi hizo walisaini makubaliano ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya eneo la nchi za Maziwa Makuu.
Mulamula alisema baadhi ya maudhui ya baraza linalotarajiwa kuundwa ni kupigia debe uhuru wa watu kutoa maoni na kubadilishana mawazo katika eneo la Maziwa Makuu, kutetea uhuru wa vyombo vya habari, kutetea wingi wa vyombo vya habari na teknolojia ya mawasiliano; na kuboresha taaluma ya habari.
Kazi nyingine ni kutoa elimu ya uraia kwa wananchi wa eneo hilo na kueneza Kiswahili kama moja ya nyenzo muhimu ya kuwaunganisha wananchi.