BENKI ya National Microfinance (NMB), imeipa serikali sh bilioni 2.55, ambazo ni gawio la hisa za serikali kwa benki hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia 2005.
Hundi ya fedha hizo ilikabidhiwa jana kwa Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji. Aliyemkabidhi ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Misheck Ngatunga, katika hafla fupi iliyofanyika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, Dar es Salaam.
Kabla ya kukabidhi hundi hiyo, Ngatunga alimwambia Waziri Meghji kuwa benki hiyo ya makabwela imekuwa ikipata faida kwa muda wa miaka saba mfululizo, na kwamba amana za wateja zimekuwa zikiongezeka kwa wastani wa asilimia 27.
“Benki imetimiza adhima yake ya kuwahudumia wateja wa kipato kidogo ambao wamechangia ongezeko la amana ya benki.
“Hivi sasa tunaongoza kwa vigezo vya ufanisi ikiwa ni amana, rasilimali, mtandao wa matawi, wateja na kupata faida.
“Mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2005, NMB ilipata faida ya sh bilioni 36.44 baada ya kulipa kodi ya mapato ya sh bilioni 11.1; faida baada ya kodi ilikuwa sh bilioni 25.3,” alisema Misheck.
Alisema wanahisa waliamua kuchukua gawio la sh bilioni tano na faida iliyobaki walielekeza itumike kuboresha huduma za wateja kwa kuongeza wateja wapya, kukarabati majengo yaliyopo, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi, kuwekeza katika jamii na kuboresha mtandao wa kompyuta.
Misheck alisema NMB imejizatiti kupeleka huduma karibu na wateja nchi nzima; dhamira ikiwa ni kufikisha huduma hadi vijijini.
Alisema tangu Machi 2006, benki hiyo imejitahidi kufungua matawi kwenye maeneo yenye wateja wengi ili kupunguza msongamano katika matawi yaliyopo sasa.
“Tumeboresha mtandao wa kompyuta ili tuweze kutoa huduma kwa njia za kisasa zaidi, nzuri kwa wateja wetu. Hivi sasa tunafanya maandalizi ya kutoa huduma za kibenki kwa kutuma ujumbe kupitia simu za mikononi (SMS Banking).
“Pia tunatarajia kuanza kutumia mashine za kulipa na kuweka pesa (Automatic Teller Machines) kuanzia Oktoba, mwaka huu.
“Kwa upande wa mikopo, benki imepanua wigo wa mikopo yake kwa wafanyabiashara wadogo.
“Hadi Juni 30, mwaka huu, tumewapa sh bilioni 99 wakopaji 188,506, wakopaji wadogo, na tunafurahi kuwa mikopo hiyo inarejeshwa vizuri kwa kiwango cha asilimia 99, jambo linalotupa uwezo wa kuendelea kukopesha,” alieleza Misheck.
Mkurugenzi huyo alieleza kwamba NMB inatarajiwa kufanywa kuwa benki ya kiwango cha juu inayotoa bidhaa nzuri zenye mchanganyiko bora unaovutia.
Aliishukuru serikali kwa kuziunga mkono jitihada za benki hiyo tangu ilipoanzishwa na aliiomba isichoke kuipa msaada hasa katika mpango inaotarajia kuanzisha wa kuunganisha mtandao wa malipo ya serikali na huduma za benki za kompyuta.
Alisema mpango huo utawezesha malipo kufanyika kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Misheck alimhakikishia Waziri Meghji kuwa NMB itaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuongeza sehemu za upatikaji wa huduma zake na kufanya kazi kwa bidii ili benki hiyo iendelee kuwa taasisi endelevu na inayopata faida.
Kwa upande wake, Meghji aliipongeza benki hiyo kwa mafanikio makubwa yaliyokwishapatikana, na akataka iongeze kasi katika kuwahudumia wananchi.
Alisema benki hiyo inawahudumia watu wengi masikini, hivyo lazima nguvu zake na jitihada zake zielekezwe katika kuwakomboa wanyonge kiuchumi.
Alishauri mikopo mingi itolewe katika sekta ya uzalishaji, hasa kwa wazalishaji wadogo ambao alisema wanahitaji ukombozi.