MBUNGE wa Sumve, Richard Ndassa, amegombana na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Magu, Elias Maarugu.
Ugomvi huo ulitokea juzi asubuhi katika Kijiji cha Nyabore, Kata ya Nkungulu, wilayani Magu, wakati viongozi wa wilaya hiyo wakipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa viongozi wa Wilaya ya Kwimba.
Ndassa alipandwa hasira baada ya Maarugu kuingilia kati hotuba yake, na kutoa maneno yaliyomuudhi mbunge huyo.
Wakati akiwashukuru wananchi, Ndassa alisema wabunge wa majimbo mawili yaliyopo wilayani Magu - Busega na Magu - hawakuhudhuria sherehe hizo kutokana na majukumu mengine ya kitaifa.
Kwa sababu hiyo, Ndassa alisema ametumwa na wabunge hao ili afikishe salamu kwa niaba yao.
Maarugu aliposikia hivyo, ndipo alipomkatiza kwa kusema: “Endelea bwana, hiyo ni kazi ya spika na wewe siyo spika.”
Maneno hayo yalimuudhi mno Ndassa. Akiwa amemwelekea Maarugu, akauliza: “Wewe ni nani unayeingilia mazungumzo yangu? Hivi kumbe huna adabu kiasi hiki! Chunga sana, mdomo wako utakuponza, endapo utaendelea kuutumia ovyo ovyo hivyo.”
Ndassa aliendelea kumtaka DC huyo kuwa na staha na adabu kwa kuheshimu itifaki wakati wa shughuli za kitaifa.
Maarugu alipoona mambo yanaelekea pabaya, alisema: “Samahani sana, mheshimiwa kama nimekukosea nisamehe, naomba.”
Aliomba msamaha huku akijishika tumboni na kuinama, kama dalili ya kuungama kosa alilotenda.
Kwa tukio hilo, Ndassa alipandisha hasira, akaamua kukatisha hotuba yake.
Baadaye alizungumza na waandishi wa habari na kusema: “Nimechukizwa na kuropoka kwa Maarugu, nimeamua nimpasulie kasoro yake mbele ya watu ili kama anaweza, ajirekebishe kwa sababu hawezi kuutumia vizuri mdomo wake.
“Mimi nimetoka bungeni jana, na nimeonana na wabunge wote wawili, wameniambia niwaletee wananchi wao salamu na kueleza sababu za kushindwa kwao kushiriki mbio za Mwenge, halafu ninaambiwa kuwa hiyo ni kazi ya spika.”
Tukio hilo lilitawala mazungumzo miongoni mwa viongozi na wananchi wa kawaida. Wapo waliomuunga mkono Ndassa, na wengine Maarugu.
Awali, Ndassa aliwasalimu wananchi wa Wilaya ya Magu na kusema kwamba amewapelekea salamu kutoka kwa wabunge wao.
Salamu za kwanza zilitoka kwa Mbunge wa Magu, Dk. Festus Limbu, ambaye hakufika kwa vile alikuwa na majukumu mengine ya kiserikali.
Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alikuwa akitarajia kusafiri nje ya nchi kwa shughuli za kikazi.