WATU wawili wamefariki dunia juzi na wengine kumi na saba wamejeruhiwa katika ajali ya basi lenye namba za usajili T. 826 AHK, lililomgonga mwendesha baiskeli kabla ya kupinduka na kumuua utingo, Ibrahimu Kibwana.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Masendoki Masendoki, amewaambia waandishi wa habari jana kuwa, ajali hiyo ilitokea saa saba na nusu mchana maeneo ya Kigogo Fresh, Wilaya ya Ilala.
Kaimu Kamanda huyo alisema kuwa basi hilo lilikuwa linatokea jijini Dar es Salaam kuelekea Kisarawe, Pwani na lilipofika maeneo ya Pugu Kajiungeni ndipo lilipomgonga David Benson (20) aliyekuwa akiendesha baiskeli.
Masendoki alisema watu kumi na saba walijeruhiwa katika ajali hiyo, na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo wanane kati yao waliruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu na wengine saba waliojeruhiwa vibaya wanaendela na matibabu.
Aliwataja waliolazwa kuwa ni Miliza Bwake (30), Aishi Ally (20), Hadida Juma (12) na Ruth Mlaki (30). Wengine ni Shaaban Rajabu (30), Salima Pampe (30) na Sauda Moshi (18).
Katika tukio jingine, jeshi hilo linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kukamatwa na puli mbili na kete 200 za bangi.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Temeke, Emmanuel Kandihabi, alisema kuwa watu hao walikamatwa baada ya jeshi hilo kufanya doria maeneo ya Yombo Vituka.
Wanaoshikiliwa ni Abasi Salum (23), Said Alfan (25) na Shabani Ulimwengu (28). Wengine ni Juma Khatib (22), Kangresi Charles (25) na Mashuku Dasai (26).