KUNA hatari ya kuibuka mapigano makali baina ya wavuvi wa visiwa vya Bongoyo, Mbiji na Pangane na mwekezaji kutoka nchini Italia, kwa madai kuwa mwekezaji huyo anawanyanyasa kwa kuwakataza wasivue kwenye visiwa hivyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Wadogo Wadogo Msasani (CHAWAWAM), Mohamed Tana, aliiambia Tanzania Daima mwishoni mwa wiki kuwa, manyanyaso wanayopata kutoka kwa mwekezaji huyo yamefikia hatua mbaya.
“Sisi sasa tumechoshwa na vitendo vya kunyanyaswa na mwekezaji huyo, kama serikali haitaingilia kati hapa kunaweza kutokea mapigano baina ya wavuvi na mwekezaji huyu…tumechoshwa jamani tukimbilie wapi?” alisema Tana.
Alisema mwekezaji huyo anawakataza wasivue samaki katika visiwa hivyo akidai kuwa serikali imempatia yeye pekee kufanya kazi hiyo.
“Sisi tuna familia na watoto wanatutegemea kutokana na kazi yetu hii, sasa tunapozuiwa na mwekezaji huyo hatujui nini hatima yetu, ”alisema Tana.
Alisema licha ya kuzuiwa kuvua samaki katika eneo hilo, wavuvi wengi wamekuwa wakinyang’anywa zana zao za uvuvi kama vyavu, mitumbwi na walinzi wa mwekezaji huyo huku wakipigwa bila sababu.
Alisema miongoni mwa wavuvi waliopigwa mwishoni mwa wiki ni pamoja na Mussa Ali, Ndoga Mohamed Mussa, Hamis Abdallah na Mwindadi Msemwa.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo alisema kumeibuka mgogoro mkubwa katika soko la samaki Msasani kwa baadhi ya watu wajanja kutaka kulibinafsisha soko hilo bila kushirikisha viongozi wa soko hilo.
Alisema mbinu za kuuzwa kwa soko hilo zimekuwa zikifanywa na mmoja wa viongozi wa kata hiyo, jina limehifadhiwa.
Uongozi wa chama hicho umeitaka serikali kuchukua hatua za haraka dhidi ya kiongozi huyo ambaye wanasema kwa kipindi kirefu sasa amegoma kuidhinisha katiba ya chama hicho ambayo Tanzania Daima imepata nakala yake ili iweze kutambulika rasmi.