Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wafanyabiashara Z’bar wataka wamilikishwe silaha
Wafanyabiashara Z’bar wataka wamilikishwe silaha
By Habari Tanzania | Published  07/24/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

WAFANYABIASHARA kadhaa mjini Zanzibar wamemweleza Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, kuwa wakati umefika kwa wao kuruhusiwa kumiliki silaha ili waweze kujihami wanapovamiwa na majambazi.

Walisema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao cha pamoja cha kujadili matukio ya uhalifu wa silaha yaliyoikumba Zanzibar katika siku za hivi karibuni.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Serena Inn, Mji Mkongwe, walisema kwamba ni jambo la kushangaza kuona wenzao Tanzania Bara wanaruhusiwa kumiliki silaha, lakini wao hawaruhusiwi.

Mfanyabiashara Mohammed Judda, alisema kwamba Wizara ya Usalama wa Raia ni moja, lakini wafanyabiashara wa Zanzibar bado sheria inawazuia kumiliki silaha.

“Mheshimiwa hatutaweza kupambana na uhalifu kwa kutegemea hirizi zinazoning’inia madukani, tunaomba maelezo zaidi kwa nini sisi tusiruhusiwe kumiliki silaha?” alihoji Judda.

Naye, mfanyabiashara, Bashir Golo, alisema: “Mheshimiwa utaratibu wa kuingia kwa pasipoti Zanzibar lazima uangaliwe upya, ili kuwatambua watu wanaoingia Zanzibar.”

Mfanyabiashara Mohammed Raza, ambaye wiki kadhaa zilizopita alivamiwa nyumbani kwake, alisema kwamba Polisi lazima ijipange upya katika kupambana na uhalifu wa silaha pamoja na biashara ya dawa za kulevya.

Alisema kwamba pamoja na Zanzibar kuwa  ndogo, biashara ya dawa za kulevya imeenea na kuwaathiri vijana wengi.

“Biashara ya dawa za kulevya inaonekana ina mtandao mkubwa Zanzibar, inakuwaje nchi ndogo kama hii inashindwa kudhibitiwa na kuwaacha vijana waathirike?” alihoji Raza.

Alishauri serikali iwapatie polisi vitendea kazi ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Kwa kuonyesha kuwa anachozungumza ni cha dhati, alichanga sh milioni mbili ili zitumike katika kampeni ya kupambana na uhalifu Zanzibar.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Saidi Mwema, alisema jeshi hilo linafanya utafiti juu ya suala la watu binafsi Zanzibar kumiliki silaha.

“Tunafanya utafiti kabla ya kuchukua uamuzi kwa sababu uzoefu unaonyesha wahalifu wanapovamia sehemu ambako mwenyewe anamiliki silaha, hutumia nguvu kubwa,” alisema IGP Mwema.

Pia alisema Polisi inafanya utafiti juu ya faida na hasara zilizopatikana kwa watu walioruhusiwa kumiliki silaha kwa upande wa

Tanzania Bara, kwa vile wengi wao wanashindwa kuzitumia.

Mkuu huyo wa Polisi alisema kwamba katika kupambana na uhalifu watendaji wa polisi watategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi na viongozi wa serikali za mitaa.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar wasisubiri kuwatumia viongozi wa Serikali za Mitaa (masheha) pale tu wanapokuwa na migogoro ya familia, bali wawatumie pia kwa shughuli za ulinzi na usalama wa raia kwa ushirikiano na polisi.

“Viongozi wa serikali za mitaa wanawajua watu wanaoingia na kutoka katika maeneo yao, na kama tutashirikiana, mpango wa polisi wa kufanya kazi kwa kushirikiana na jamii (Community Police) utaweza kufanikiwa,” alisema.

Naye, Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, alisema kwamba suala la usalama wa raia na mali zao si la polisi pekee, bali ni la wananchi wote.

Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Khalid Idd Nuizan; Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Ramadhan Kinyogo;  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Khatib Shaaban; na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mjini, Hassan Nassir.

Wengine ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar, Abdalla Abass Omar; na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Mgharibi, Abdalla Mwinyi


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.