Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Meghji achongewa
Meghji achongewa
By Habari Tanzania | Published  07/24/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Na Pascal Mayalla, Nairobi

UMOJA wa Wafanyabiashara wa Viwanda vya Mafuta ya Kula wa Tanzania na Kenya, wamemshitaki Waziri wa Fedha wa Tanzania, Zakia Meghji, kwa Bunge la Afrika Mashariki.

Wafanyabiashara hao wamefikia hatua hiyo baada ya kuona imeshindikana kwa Meghji kubadilika “jiwe”, kwani amekataa katakata mbinu za kushusha ushuru wa bidhaa hiyo.

Wanadai kwamba, amekwamisha utekelezaji wa nia njema, wa ushuru wa pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki kuhusu mafuta ya kula.

Walisema kuwa, makubaliano yalikuwa kwamba malighafi ya mafuta hayo isitozwe kodi, yaani iwe sifuri.

Katika hotuba ya bajeti ya serikali ya mwaka 2006/2007 iliyosomwa na Meghji, ushuru wa malighafi hiyo ulipandishwa hadi asilimia 10; jambo ambalo linalalamikiwa mno na wafanyabiashara hao.

Mashitaka kwa Bunge la Afrika Mashariki yalitolewa mwishoni mwa wiki na Kiongozi wa Umoja wa Wafanyabiashara Wakuu wa Mafuta ya Kula, Sanjay Somani.

Somani ndiye mmiliki wa viwanda vya mafuta vya BIDCO vilivyopo Tanzania na Kenya.

Walitoa mashitaka mbele ya Kamati ya Biashara na Uwekezaji ya Bunge la Afrika Mashariki.

Kamati hiyo ilikuwa ikikusanya maoni kuhusu utekelezaji wa ushuru wa pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki, shughuli iliyofanyika katika Hoteli ya Safari Park jijini hapa.

Somani alisema Meghji, anatarajia kupeleka bungeni muswada mpya wa fedha wa mwaka 2006/2007; akipendekeza kutoza kodi ya asilimia 10 bidhaa zote za mafuta ya kula wakati ushuru wa pamoja unatamka kuwa malighafi zote hazitatozwa ushuru.

Somani alisema muswada huo umeandaliwa bila kukusanya maoni ya wadau muhimu.

Alisema umepuuza mapendekezo yaliyotolewa baada ya tafiti mbalimbali.

Baadhi ya ripoti za utafiti huo ni za Tume ya Profesa Wangwe ya mwaka 2002; Ripoti ya Chama cha Wenye Viwanda Tanzania (CTI) ya mwaka 2003; na Ripoti ya Tume ya Wataalamu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Februari, 2004.

Alisema ripoti zote zimeshauri ushuru wa asilimia sifuri kwa malighafi ya mafuta ya kula.

Somani alisema kupitishwa kwa muswada huo, si tu kutakwenda kinyume cha nia njema ya ushuru wa pamoja, bali pia kutasababisha hasara kubwa kwa viwanda vya mafuta.

Alisema kwa ushuru huo, havitaweza kushindana na mafuta yatakayotoka nje ya nchi, kwani gharama za uzalishaji ni kubwa.

Akijibu hoja hizo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Nangale, alisema wameyapokea malalamiko hayo na watayafanyia kazi.

Hata hivyo, alikiri kuwa suala la mafuta kwa muda mrefu limekuwa tata kutokana na wenye viwanda vya sabuni kutaka ushuru wa asilimia sifuri kwa mafuta ambayo ni malighafi ya bidhaa za sabuni.

Nangale alisema ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa zote za mafuta, unalenga kuwalinda wakulima wa ndani wa mazao kama vile mawese, alizeti, pamba, ufuta na mlonge.

Alisema kukosekana kwa ushuru kwa malighafi ya mafuta ya kula iingizwayo nchini, kuliwafanya wakulima wengi wasiendelee na kilimo, na hivyo kuathiri maisha yao.

Alisema utata katika suala zima la malighafi ya mafuta ya kula, unatokana na baadhi ya wenye viwanda vya mafuta ya kula kuwa ndiyo hao hao wenye viwanda vya sabuni.

Alisema wanaagiza malighafi kwa ushuru wa asilimia sifuri na kuuza bidhaa hizo hizo kwa viwanda vya sabuni kwa ushuru huo huo.

Ziara hiyo iliyodhaminiwa na Shirika la Friedrich Ebert Stiftung, leo inaingia siku yake ya saba kwa kutembelea Kampala, Uganda kabla ya kwenda Mutukula.

Itahitimishwa nchini Tanzania kwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na mpaka wa Namanga. 

Waziri Meghji, akizungumza na Tanzania Daima kwa simu mwishoni mwa wiki akiwa jijini Dar es Salaam, alipuuza madai ya wafanyabiashara hao, na kusema uamuzi wa kuweka kodi hiyo umezingatia zaidi maslahi ya wakulima na taifa.

“Najua wanataka kodi hiyo iondolewe, lakini lini tutatoka hapa tulipo? Viwanda vyetu, wakulima wetu lini watakuwa na hali nzuri?” alihoji.

Alisema kimsingi, kinachoingizwa na wafanyabiashara hao si malighafi, bali mafuta yaliyokwishapitia hatua mbalimbali za utengenezaji, hivyo wanastahili kulipa kodi hiyo.

Alisema kama ni suala la mawese, waombe ardhi, wapewe, walime na kisha waanze kuvuna baada ya miaka minne hadi mitano.

“Uganda wamefanya hivyo, kwa nini wasiombe ardhi wapewe, walime ili wapate malighafi hapa hapa, waweze kuwanufaisha pia wakulima wa Tanzania?” alihoji.

Meghji alisema kilimo, kama njia kuu ya ajira kwa mamilioni ya Watanzania, kinapaswa kuwekewa utaratibu mahususi ili kiweze kukua, na hivyo kutoa ajira zaidi kwa Watanzania.

Kwa kuhitimisha, Meghji alisema: “Hakuna namna, wanapaswa walipe ushuru huo, tayari wakulima wetu, ndani ya wiki hizi chache, wameanza kunufaika, hatuna namna isipokuwa walipe tu kodi hiyo.”


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.