TANZANIA imetajwa kuwa moja ya nchi maskini zaidi duniani, kwa kuwa ukuaji wa uchumi wake upo chini ya asilimia saba.
Hizo si habari nzuri kwa Watanzania, kwa kuzingatia ukweli juu ya rasilimali tulizonazo, ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi hapa duniani, na hata katika Bara la Afrika.
Kenya imeponyoka kwenye kundi letu, na sasa inajidai ikiwa inaelekea kuzuri. Tunasema kwamba si habari nzuri kwa Watanzania kwa sababu, kwa miaka nenda rudi tumeimbiwa juu ya jitihada za kukuza uchumi.
Tangu Awamu ya Kwanza, kumekuwapo na maneno ya kutia moyo na kuburudisha, yote yakiegemea zaidi kukitegemea kilimo kutuondoa hapa tulipo. Lakini kwa bahati mbaya, hadi sasa hakuna kilichofanyika, zaidi ya kukalia rasilimali zetu.
Kilimo kimeendelea kuwa cha kutegemea jembe la mkono, hakuna anayesema ni kwa vipi mipango iliyowekwa sasa itakavyoliondoa taifa kwenye kilimo kidogo, wakati ikijulikana wazi hali ya mvua.
Wakulima wadogo wameambiwa kwamba sasa wapanue mashamba yao; wale wa chai, kahawa, korosho, mpunga na kadhalika wanatakiwa waongeze jitihada, lakini wanafanyaje hayo ikiwa zana zao bado ni duni?
Mapinduzi ya kilimo yanakuja vipi na kuwafikia wakulima ambao hadi sasa hawajakuwa na uhakika wa masoko ya kuuzia mazao yao, nguvu kazi itakayotumika mashambani, kwani vijana wamehamia mijini, au walau kujua ushirika wao uliowasaidia kupanga bei unakuzwa?
Mbaya zaidi ni kwamba nchi yetu imekumbwa na ukame wa kujitakia, kutokana na viongozi kukaa kimya kwa miaka yote, wananchi walipokuwa wakiharibu mazingira, wakikata miti na kuiuza nje ya nchi.
Leo kunageuka jangwa, ndiyo inatangazwa operesheni. Tunafungaje zizi wakati tayari ng’ombe wametoka zizini? Kiasi cha sh milioni 500 kwa kila mkoa kitaweza kweli kuondoa umaskini? Labda kama hatujui maana halisi ya umaskini.
Tanzania imebaki na nchi kama Zimbabwe, Zambia na Uganda, ambazo kwa kweli hazina rasilimali nyingi kama sisi. Ardhi yetu ni kubwa, yenye rutuba na mito mingi pamoja na mabonde mengi, lakini tunashindwa kuitumia.
Madini nayo yapo mengi, lakini simulizi ya jinsi yanavyochimbwa, kutumiwa na wananchi wanachopata, ni huzuni tupu. Wakati yamebaki mashimo makubwa kabisa yasiyojulikana yatajazwa vipi, ndipo tunafikiria kupitia upya mikataba.
Kwa kipato cha madini, tungeweza kabisa kuufufua uchumi wetu na kwenda mbali. Kumbe basi, ikiwezekana hata leseni zilizopo zingesitishwa ili uchunguzi ufanyike, badala ya kuahidi kuzipitia, huku madini yakihamishwa kila uchao.