WAKAZI wa Dar es Salaam, wamewapongeza wakuregenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam kwa kubaki katika halmashauri zao bila ya kuhamishwa.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema serikali ina imani na wakurugenzi hao ndio maana wameachwa, hivyo wanapaswa kuchapa kazi zaidi.
“Wamejitahidi kupunguza kero za barabara za mitaa ya Dar es Salaam na masoko yanaridhisha kidogo,” alisema mfanyabiashara mmoja wa soko la Ilala, Boma.
Wafanyabiashara wengi wa masoko la Ilala Boma, Kariakoo, Kisutu na Tandale waliohojiwa, bado wanalalamikia hali ya uzoaji taka na usafi katika masoko hayo.
Walisema mitaa mingi ya Dar es Salaam sasa imefurika maji machafu yanayozagaa kila mahali kutokana na kuvuja kwa mifereji na mitaro ya kupitishia maji hayo.
“Wakurugenzi sasa waangalie zaidi swala la mitaro ya maji machafu kwani kwa kipindi kirefu wakati wa mvua bababara za katikati ya jiji hazipitiki,” alisema Abdallah Juma.
Hivi karibuni, serikali ilifanya mabadiliko ya vituo na kuteua wakurugenzi wapya katika halmashauri zote nchini, lakini wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, waliachwa bila kubadilishwa.
Wakurugenzi hao na halmashauri zao kwenye mabano ni Idd Nyundo (Temeke), Damian Lubuva (Ilala) na Hussein Katanga (Kinondoni).