Na Solomon Mwansele, Mbarali
UHABA mkubwa wa madawati uliokuwa ukiikabili shule ya msingi Mahango Ruiwa iliyopo wilayani Mbarali na kusababisha wanafunzi wa darasa la tatu kukaa chini sasa umepatiwa ufumbuzi kufuatia madawati mapya 20 kutengenezwa.
Taarifa za shule hiyo kukumbwa na upungufu wa walimu wanane na madawati 57 uliopelekea wanafunzi hao kusomea chini ziliripotiwa na gazeti hili miezi miwili iliyopita.
Ilielezwa kuwa hali hiyo ya wanafunzi hao kukaa chini ilichangiwa zaidi na shule hiyo kuandikisha wanafunzi wengi waliojiunga na darasa la kwanza mwaka huu.
Akiongea na mwandishi wa habari hii Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Samwel Sheshambo, alisema madawati hayo 20 yametengenezwa na serikali ya kijiji cha Mahango Ruiwa kufuatia michango iliyotolewa na wananchi wa kijiji hicho.
Sheshambo alisema madawati mengine (hakutaja idadi), yamefanyiwa ukarabati na pia wamebuni utaratibu wa muda kwa wanafunzi wanne kukaa katika dawati moja wakati juhudi za kukamilisha madawati mengine 27 yanayohitajika zikiendelea kufanywa.
"Hadi sasa hakuna mwanafunzi anayekaa chini na madawati hayo mengine 27 yanayohitajika yatakuwa tayari yametengenezwa kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, mwaka huu," alisema Sheshambo.
Kuhusu upungufu wa walimu shuleni hapo, Sheshambo alisema tatizo hilo nalo limeanza kupatiwa ufumbuzi kufuatia Ofisa Elimu wa wilaya hiyo kuwaongezea mwalimu mmoja na hivyo kufanya walimu waliopo shuleni hapo kufikia 7.
Alibainisha kuwa ofisa elimu huyo ameahidi kuwaongezea walimu wengine wanaohitajika ili kuondokana na upungufu wa walimu wanane hadi sasa unaoikabili shule hiyo.
Shule ya msingi Mahango Ruiwa yenye wanafunzi 530 na walimu 6 ilikuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati 57 kufuatia kuandikisha wanafunzi wengi waliojiunga na darasa la kwanza mwaka huu.
Katika shule hiyo kulikuwa na upungufu wa walimu wanane hali iliyopelekea walimu sita waliokuwepo kufanya kazi zaidi ili kuziba pengo hilo la upungufu wa walimu hao waliokuwa wanahitajika.