HOJA ya mgombea binafsi inamkera sana Rais Jakaya Kikwete, baadhi ya watu wake wa karibu wamesema.
Habari kutoka kwa vyanzo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinasema:“Kati ya mambo ambayo rais hapendi kusikia ni mgombea binafsi.”
Kwa sababu hiyo, rais huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ameomba chama kimsaidie kuidhoofisha hoja hiyo kwa mbinu mbalimbali.
Mbinu ya kwanza iliyokubalika katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kilichofanyika Aprili mwaka huu, ni kukata rufaa mahakamani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyokubaliana na Mchungaji Christopher Mtikila kuhusu umuhimu wa mgombea binafsi mapema mwaka huu.
Mbinu ya pili ni kuwatumia baadhi ya vigogo ndani ya CCM kuzungumzia hoja hiyo kwa kuikataa, ili kupima hisia za wananchi.
Wa kwanza aliyetumwa kupima hisia hizo ni Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa, ambaye tayari ameshalizungumzia suala hilo, akisema wakati muafaka kwa Tanzania kuwa na mgombea binafsi haujawadia.
“Unadhani Mkapa alikuwa anatoa msimamo wake binafsi? Huo ndio msimamo wa chama chetu. Tulishajadili suala hili, tukasema hakuna haja ya kuliruhusu, kwa kuwa linaweza kutubomoa,” alisema kiongozi huyo mwandamizi ndani ya CCM.
Akizungumzia sababu za Rais Kikwete kuogopa mgombea binafsi, alisema si yeye pekee, bali wapo wengi wanaohisi kwamba likiruhusiwa, watu maarufu wenye uwezo wa kifedha ndani ya CCM wanaweza kukihama chama hicho na kukipa ushindani mkali.
“Mzee (Kikwete) angependa amalize ngwe yake ya miaka 10. Ukiruhusu ushindani mkali chama kitameguka, nguvu itapungua, tutapata wapinzani wenye nguvu…na huwezi kujua matokeo yake bwana,” alisema.
Hata hivyo, uchunguzi wa Tanzania Daima umeonyesha kwamba wabunge wengi wa CCM wanapenda wagombea binafsi waruhusiwe.
Baadhi ya wabunge wa CCM waliohojiwa wamekiri kwamba mgombea binafsi ni fursa kwa wana CCM wengi wanaoishi kwa hofu ndani ya chama hicho.
“Nakwambia, asilimia 90 ya wabunge wa CCM tunataka mgombea binafsi aruhusiwe katika ngazi zote. Chama kinatumia nguvu yake kutunyonya na kututesa, hasa wakati wa uchaguzi, kwani kama ni pesa, kila mgombea hutumia nguvu yake,” alisema mmoja wa wabunge wa muda mrefu ndani ya CCM.
Mbunge mwingine wa siku nyingi alisema: “Wakubwa wanaogopa mgombea binafsi kwa kuwa hawajiamini. Hata uamuzi wenyewe wa kulipinga suala hili ulivyofikiwa, kama unavyoelewa, haukuwa wa kidemokrasia. Hatukulijadili hasa…wakubwa waliamua wenyewe na kutuburuza sisi, basi.”
Mwingine alisema: “Sikutarajia kwamba hata JK angejiingiza katika biashara hii ya woga…hasa ukizingatia kwamba hapendi kuchukiwa au kulaumiwa na wananchi…lakini hili limepitishwa haraka haraka kumlinda yeye asipate upinzani mkubwa kutoka ndani au nje ya CCM.”
“Kumbe hujui! Viongozi wetu ni waoga sana… Rais halitaki suala hilo, linamkera, na tayari Mwanasheria Mkuu alishaagizwa alipinge mahakamani,” alisema mbunge mwingine jana na kuongeza:
“Si tu ndani ya chama. Unajua wapo watu ama kwenye vyama vya upinzani au wasio wanasiasa, wakubwa wanaona kwamba tukiruhusu suala hili wataibuka na kutumia uwezo wao kuushawishi umma uwaunge mkono. Na katika mazingira ya sasa, haitakuwa vigumu kwa wagombea binafsi kupita kule wanakokubalika, kwani hata katika uchaguzi wa sasa, wengi wanapita kwa mvuto na uwezo wao binafsi, chama kinawasaidia kidogo.”
Mwingine alisema: “JK hataki kuchafua rekodi yake ya kupendwa na wananchi, ndiyo maana amelainika haraka katika suala la kupinga takrima, lakini amegundua kwamba wananchi walio wengi wana uelewa mdogo kuhusu hoja hii ya mgombea binafsi, wengi hawaoni faida ya watu kugombea bila vyama, hivyo anajua hata CCM ikilipinga wananchi hawatakuja juu.”
Mara ya kwanza kwa Serikali na CCM kupingana na mahakama juu ya suala hili, ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya tisini, lakini Bunge, wakati huo likiwa la chama kimoja, lilitunga sheria kuzuia wasio na vyama kugombea nafasi za uongozi.
Mchungaji Mtikila, aliyekuwa ameshinda kesi hiyo, alifungua upya kesi dhidi ya serikali; na mapema mwaka huu, Mahakamu Kuu iliamua kwamba suala hilo ni la msingi katika kanuni za demokrasia na kwa mujibu wa haki za binadamu.
Wanaharakati wamekuwa wakishangaa nia ya serikali kukataa mgombea binafsi huku ikijua ni haki ya kidemokrasia kwa mtu kupiga au kupigiwa kura.
Hata hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kulizungumzia suala hili, akikilaumu chama chake na serikali kwa kung’ang’ania zama zilizopita, huku akisisitiza kuwa baadhi ya watu wana mvuto na nguvu binafsi kuliko chama.
Aliongeza kuwa hata CCM ingekubali wakati ule kuruhusu mgombea binafsi, ilikuwa bado na uwezo wa kuwashinda kwani wengi wao watagombea bila kuwa na nyenzo za kutosha; lakini akasisitiza kwamba ni haki yao, waruhusiwe.
Baadhi ya wana CCM wanaotaka mgombea binafsi, waliliambia gazeti hili kwamba jitihada hizi za serikali na chama chao kupinga mgombea binafsi, ni ushahidi mwingine kwamba “wakubwa hawamuenzi tena Baba wa Taifa kama wanavyosema kwenye hotuba zao.”
“Wanatumia mamlaka yao kuatamia nguvu na akili za wenzao, utadhani kuna kitu wanafanya…hakuna,” alisema.
Jitihada za kumpata Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kuzungumzia sababu za woga wa chama chao kupingana na msingi huu nyeti wa kidemokrasia hazikuzaa matunda jana. Simu yake ilipokewa na mtu mwingine ambaye hakujitambulisha, lakini akasema; “mzee yupo kikaoni.”