WIKI chache zijazo, mwaka utakamilika tangu nianze kuandika safu hii. Nadhani si mapema kuanza kuangalia nilikotoka na lengo langu lilikuwa ni nini hasa.
Nataka kujikumbusha lengo langu, ambalo ni kwalo nakuandikia wewe msomaji. Hapo mwanzoni nilitaka lengo langu liwe kujikumbusha juu ya maisha. Kwamba sisi ni kina nani, kwamba ni vema kujikumbusha na kufanya vile ambavyo tunatakiwa kufanya.
Kwangu, ni faraja kuwa wapo watu wanasoma kile ninachoandika. Baadhi yao tayari huwasiliana nami juu ya hisia zao katika mawazo yangu. Shukrani zangu za moyo ziwafikie popote walipo.
Mara nyingi natoa mifano ya kihistoria juu ya watu mbalimbali. Natoa nukuu kutoka kwa watu mbalimbali, wengine wao wakiwa maarufu. Naaangalia pia hadithi ambazo zinaweza kukifanya kile ninachokusudia kieleweke kwa urahisi. Nukuu ninazozitoa, lengo lake la kwanza si kusudi tuwaelewe wale waliozisema, (ni vema pia kuwaelewa) bali kusudi tujielewe zaidi sisi.
Wala lengo si kuangalia historia ya watu ambao mara nyingi nawatoa kama changamoto, bali lengo ni kujua kwamba na sisi tuna nafasi tunayotakiwa tuitumie. Naandika kwa ajili yetu, si kwa ajili yao, si kwa ajili ya hadithi, si kwa ajili ya mifano, bali kwa ajili yako, kwa ajili yangu. Naandika kusudi tujitafakarishe. Tena baadhi ya wale ninaowanukuu, sikubaliani na kila kitu katika maisha yao, ila nakubaliana na baadhi ya maelekezo yao.
Naandika kusudi tutumie mifano hii, na pengine na wewe ujikumbushe na mifano mingine ambayo kwako, labda inaweza kuwa na umuhimu kuliko hii ninayoitoa mara kwa mara. Mifano yangu, nukuu ninazozitoa, hadithi ninazotoa, si kitu kitakatifu ambacho lazima ukichukue, pengine una mifano ya maana zaidi kwako katika kukupa changamoto. La muhimu ni kuwa, mifano hiyo itakuchokoza kuwaza zaidi juu ya yale ambayo tayari una uzoefu nayo.
Naandika, kwa hiyo, si kama mwalimu, bali kama mtu ninayetaka kutafakari pamoja na wewe, na katika kutafakari tuweze kuona mbele zaidi. Si kama mamlaka elekezi, bali kama tunaotembea pamoja na ambao pia, kama maisha yalivyo, uwezekano wa kukosea upo kati yetu.
Naamini katika uwezo wa kila mmoja wetu kiakili. Naamini katika mipango inayowezekana ya kila mmoja wetu, ilimradi ni mipango isiyokinzana na maumbile, isiyokinzana na majaliwa yetu. Lakini nashawishika kuamini kuwa wengi wetu bado hatuyachukulii maisha kwa uzito unaotakiwa na kanuni zinazopaswa.
Hata kama tumekuwa wasikivu kwa kanuni ambazo ni sahihi, bado mara nyingi kanuni hizi hazitupi furaha, kwa kuwa hatutaki kujifunza au kutafakari kwa nini tuzifuate, na katika kutafakari, kanuni hizi ziwe sehemu ya maisha yetu. Wakati mwingine tumekuwa watumwa wa sheria badala ya kufurahia sheria hizo, taratibu hizo, kanuni hizo za maisha.
Naamini katika uwezo wetu ambao unapatikana kwa kuweka misingi mizuri kwa kila jambo. Tukikosa msingi mzuri ambao ndio utakuwa kiungo katika chochote chema tufanyacho, basi hata mengi tutakayofanya yatakuwa ya kubahatisha. Kuweka misingi imara kwa kurekebisha tuliyovuruga. Misingi itakayotuwezesha kusimama wenyewe. Misingi itakayotuwezesha kuelezea kile tunachofanya. Vinginevyo tutakuwa ‘fundamentalists’ - wenye misimamo mikali, ambao hutoa majibu kabla ya swali, kwa kuwa wanakurupuka kutetea kwa jazba bila kufikiri.
Kuna tofauti kubwa kati ya mashine inayomtii mwongozaji wake na mtu anayetii kanuni sahihi za maisha. Mashine haifanyi kazi kwa ufahamu wala kwa upendo. Sisi pia tunapofanya bila kufahamu, bila upendo, mara nyingi tunakuwa tumejishusha mno. Kuna haja ya kutafakari hata yale tunayoyajua kwamba ni sahihi, kwa sababu ni katika kufanya hivi, maisha yanakuwa mapya daima. Kitu kinapokuwa ni mazoea, maisha yanachosha, na hivyo tunatafuta burudani zisizofaa kusudi kuyapa maisha maana.
Tunafanya mambo mengi sana katika maisha. Ni kweli hatuwezi kuweka akili zetu na hisia zetu katika yote hayo, kwa kuwa mambo hayo ni mengi mno. Lakini ni muhimu kuwa katika yale ya msingi au ya maana zaidi. Kusoma na kuelewa ikiwa wewe ni mwanafunzi. Kusali na moyo wako kuwa katika sala ikiwa wewe ni muumini, kufanya chochote cha muhimu na akili yako iwe pale. Mwalimu wangu aliniambia kwamba, mambo ambayo tunaweza tukaacha kuweka akili yetu yote ni kama vile kupumua, isipokuwa labda kama wewe ni mwanafunzi wa kuimba, maana hapo itabidi kuongoza pumzi yako.
Na kukumbuka pia tulichofanya na kujikumbusha mbinu tulizotumia katika kushinda au kushindwa kwetu. Mwalimu akatoa tena mfano wa mchezaji mpira. Katika fainali anatumia mbinu nyingi na akili yake inafanya kazi kwa namna ya haraka ajabu, na wakati mwingine kwa usahihi.
Baada ya mpira, ana uwezo wa kuangalia taratibu mkanda wa mechi ile na kujifundisha tena mwenyewe mbinu zile alizotumia wakati wa mchezo, na kuzitolea maelezo ingawa wakati ule alikuwa haelewi. Huo ni mfano ambao nasi pia twaweza kuutumia kuangalia tulipotoka, kuangalia kwa taratibu na kuweza kuangalia mbinu tulizotumia na kuzidumisha, na ikiwa tulifeli, tukiri kufeli kwetu na kutaka kwenda tena kwa usahihi.
Na moja ya sababu zinazofanya maisha kuwa ya ovyo ni kwa kuwa hatutaki kuangalia tulikotoka. Haturekebishi udhaifu wetu wa nyuma. Kwa sababu hatuangalii nyuma, pia hatujifunzi mbinu sahihi zaidi ya zile za mwanzo. Hata kama tulifanya vizuri, nafasi yetu ya kufanya kwa usahihi zaidi inakuwa haba.
Alikuwa ni Socrates, aliyesema kuwa maisha bila tathmini hayana maana ya kuyaishi. Wakati mwingine inabidi kuangalia kwa uchungu jinsi tulivyokosea mahali fulani. Ni muhimu kuvuta kumbukumbu hizi chungu na kuzifanyia kazi, badala ya kuzifunika na kujidai kuwa hakuna lililotokea. Kisaikolojia, hata baadhi ya matatizo huponywa kwa njia hii.
vedamwema@yahoo.com
0784 77 40 69