CHAMA cha Wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRAWU), kimelipongeza Baraza la Mawaziri kwa kuagiza kusitisha ubinafsishwaji wa TRC ili mkataba huo uweze kufanyiwa marekebisho.
Kaimu Katibu Mkuu wa TRAWU, Sylivester Rwegasila, alisema jana kuwa, ingawa hawajaarifiwa rasmi kuhusu suala hilo, lakini hawana budi kupongeza busara za Baraza la Mawaziri.
“Hatuna budi kupongeza uamuzi huu wa busara wa Baraza la Mawaziri kwani tuna imani sasa upungufu uliopo utarekebishwa,” alisema Rwegasila.
Alisema uamuzi huo si tu ni habari njema kwa TRAWU, bali pia kwa wafanyakazi wa shirika hilo na Watanzania kwa ujumla, kwani ndicho kilio chao kwamba mkataba wa LITES una upungufu.
Rwegasila, alisema mbali na kueleza serikali dosari zilizopo katika mkataba huo, pia TRAWU imekuwa ikisisitiza kutokuwapo kwa ulazima wa kukodishwa ama kubinafsishwa kwa TRC.
Alisema, TRAWU imekuwa ikisisitiza kwamba badala ya kuikodisha ama kuibinafsisha TRC, serikali inaweza kuliokoa shirika hilo kwa kuteua menejimenti mpya na kuongeza mtaji.
“Suluhisho la TRC si kuikodisha ama kuibinafsisha, bali ni kufanya mabadiliko ya menejimenti na kuiongezea mtaji, TRC haijafikia hali mbaya kiasi cha kukodishwa ama kubinafsishwa,” alisema.
Alisema, mkakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ni kuongeza ajira ili kuwaondolea umaskini wananchi, hivyo mpango wa kupunguza wafanyakazi 4,000 una athari kubwa.
“Iwapo serikali itaendelea na nia ya kuibinafsisha ama kuikodisha TRC, kutokana na mazingira ya usiri katika mkataba huu wa LITES, TRAWU tunaomba wafanyakazi wote walipwe haki zao,” alisema.
Mei mwaka huu, wafanyakazi hao walikutana jijini Dar es Salaam na kufikia azimio la kuwatuma viongozi wao kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili kufikisha kilio chao