RAIS Robert Mugabe amekataa kumlipia ada ya shule mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa, Chatunga, akisema kuwa ada anayotakiwa kulipa ni kubwa mno.
Shule anayosoma mtoto huyo, pamoja na nyingine, zimelazimika kuongeza ada kwa kiwango kikubwa cha asilimia 400 kutokana na mfumuko wa bei uliofikia asilimia 1,200 ambao ni rekodi duniani.
Waziri wa Elimu, Aeneas Chigwedere ameitaka shule hiyo kupunguza ada hadi nusu ya kiwango cha sasa katika agizo linaloonekana kutokana na amri ya Rais Mugabe.
Shule hiyo binafsi ya msingi ya Hartman, kwa sasa inawataka wazazi wa watoto wasomao hapo kulipa ada ya dola milioni 109 za Zimbabwe.
Uongozi wa shule hiyo umesema kuwa, kiwango hicho hakina tofauti na ada zinazotozwa katika shule nyingine binafsi.
Hata hivyo, barua kutoka kwa Waziri Chigwedere ilitaka ada kwa kila muhula ipunguzwe hadi dola milioni 53 za Zimbabwe (sawa na sh laki saba).
Kwa mujibu wa Chigwedere sababu ya kutaka kupunguzwa kwa ada ni kwamba haziendani na msimamo wa bei kwa wateja.
Vyanzo vya habari vya serikali vilisema kuwa, Mugabe alimuagiza Chigwedere aandike barua kwa shule hiyo, kwa sababu anaamini kwamba ada hiyo ni kubwa mno.
Ada kwa mtoto mwingine wa kiume wa Mugabe, Robert mdogo, ni dola milioni 25 za Zimbabwe (sawa na karibu sh laki 3.5).
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, wazazi wa wanafunzi katika shule hiyo “wamenawa mikono” kwa kuwa wanaamini kwamba hakuna njia nyingine.
Baadhi ya wazazi wanasema kuwa iwapo Rais Mugabe hataki kulipa ada hiyo, amwondoe mtoto wake.
Wakati mhula wa shule ukitarajia kuisha kipindi cha wiki mbili zijazo, wazazi ambao hawawezi kukabiliana na makali ya ada wanatarajia kuwaondoa watoto wao shuleni.