Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali yabanwa mbavu
Serikali yabanwa mbavu
By Habari Tanzania | Published  07/22/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Martha Mtangoo, Dodoma

MBUNGE wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), amepinga ubaguzi unaodaiwa kufanywa na serikali katika elimu.

Ameitaka serikali ieleze iwapo fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya mikopo ni kwa wanafunzi wa vyuo vya serikali pekee au la.

Mkono alikuwa akichangia hoja iliyotolewa bungeni na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla, kwenye makadirio ya matumizi ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha wa 2006/2007.

Mbunge huyo aliitaka serikali kuweka bayana kuhusu mikopo hiyo kutokana na kauli ya waziri huyo aliyoitoa hivi karibuni kuwa mikopo itatolewa kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu vya serikali pekee.  

Alisema iwapo fedha hizo zitatolewa kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma vyuo vya serikali pekee ni ubaguzi ambao Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakataza, kwa kuwa binadamu wote ni sawa na wana haki.

“Mheshimiwa Spika, kabla sijaunga hoja mkono naomba waziri anieleze kuwa hizi sh bilioni 50 za mikopo ni kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma vyuo vya elimu ya juu vya serikali au kwa ajili ya wanafunzi wote, na kama ni kwa ajili ya wanafunzi wa serikali, mimi siungi hoja mkono,” alisema mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi.

Alisema sheria ya mikopo inaruhusu mtu yeyote mwenye umri wowote, alimradi awe na sifa ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu, anaruhusiwe kupata mkopo kwa ajili ya kusoma. Alisema iwapo fedha hizo zitalenga vyuo vya serikali, wanafunzi wa vyuo binafsi watakuwa hawakutendewa haki.

Alisema kubagua watu ni kukiuka katiba ya nchi kutokana na ubaguzi wa kuwapatia wale wa vyuo vya serikali na kuwanyima wale wa vyuo binafsi.  

Alisema suala la serikali kudai haina fedha si la kweli, kwa kuwa serikali ina vyanzo vingi vya fedha ambavyo vinaweza kutumiwa na kufadhili wanafunzi wa elimu ya juu.

“Serikali iuze dhahabu isomeshe wanafunzi, lakini suala la serikali kusema haina pesa si kweli,” alisema mbunge huyo ambaye alikataa kuunga mkono hoja hiyo.

Juzi, Profesa Msolla, alinukuliwa akisema kuwa mikopo ni kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya umma pekee.

Kauli hiyo ilizua malalamiko mengi miongoni mwa wadau, wakisema uamuzi huo ulikuwa wa kibaguzi. Kwa kuondoa msimamo huo, serikali itakuwa imejiweka katika mazingira mazuri ya kuepusha mgogoro ambao chanzo chake kilionekana kuwa ni ubaguzi.

Naye, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Fatma Fereji, aliitaka serikali kuvunja Bodi ya Mikopo na kuanzisha upya bodi hiyo kwa kuweka watendaji wengine.  

Alisema kutokana na utaratibu wa bodi hiyo kutoridhisha, ingekuwa vyema ikavunjwa na kuanza upya, kwa kuweka watendaji wengine.  

“Mheshimiwa Spika, mimi naona bodi hii ingevunjwa na kuanza upya kwa kuweka watendaji wengine, kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake sawasawa…kila siku wanafunzi wanaandamana kwenye ofisi zao,” alisema mbunge huyo.

Aliitaka serikali itoe maelezo kuwa ni hasara gani imepatikana tangu bodi ilipoanzishwa kutokana na utaratibu mbaya uliowekwa na bodi hiyo.

Naye, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Nyawazwa (CCM), aliitaka wizara hiyo kurekebisha utaratibu uliopo sasa wa kuwataka watu kuomba mikopo kabla ya udahili.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.