DAR ES SALAAM inaye Mkuu wa Mkoa (RC) mpya, Abbas Kandoro, ambaye awali alikuwa RC wa Tabora kabla ya kuhamishiwa Arusha alikokaa kwa muda mfupi.
Kama ilivyotarajiwa, kwa wateule wapya, Kandoro ameanza kwa kugusa suala muhimu na ambalo limekuwa likilalamikiwa na watu, kutokana na kero yake na kumomonyoka kwa maadili.
Hilo ni kuagiza kufungwa biashara ya ukahaba inayofanywa katika eneo la Uwanja wa Fisi, Manzese jijini Dar es Salaam. Ameagiza pia kuchukuliwa kwa hatua wote watakaokwenda kinyume cha agizo hilo.
Kandoro kama RC, anatekeleza majukumu yake ya kazi, na sisi tunataka asimamie uamuzi wake na ahakikishe maagizo yote yanatekelezwa haraka, biashara inafungwa mara moja na moja kwa moja.
Watoto wamekuwa wakidhalilishwa katika eneo hilo, biashara ya ngono chafu inafanywa kana kwamba hakuna viongozi katika eneo husika, wakati kila baada ya miaka mitano wanapiga kampeni na kisha kuchaguliwa, hatimaye kusherehekea ushindi wa kishindo.
Kero hiyo imepigiwa kelele na wananchi kwa muda mrefu, viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa wanaishi na wananchi hao hao, lakini hawachukui hatua, labda wakiogopa kukosa kura chache za eneo husika, au wakiona si wajibu wao.
Sisi tunasema kwamba, waliopewa uongozi waelewe kwamba hiyo ni dhamana kubwa, waliudai kama haki, sasa watekeleze wajibu, bila kujali kwamba nyumba za kulala wageni (gesti bubu) za Uwanja wa Fisi ni za rafiki au ndugu zao.
Agizo la Kandoro liwazindue wengine pia, na yeye mwenyewe anatakiwa kuangaza macho maeneo tofauti katika mkoa huu, ahakikishe hali inarejea kuwa shwari, matendo machafu yanayotia aibu yanaachwa na watu wanafanya kazi au biashara halali ya kuwaingizia kipato.
Wimbi la wanaouza miili yao limekuwa kubwa, kasi ya wanaorubuni wasichana na hata watoto kufanya nao ngono ni ya kutisha na kila jitihada zinatakiwa kufanywa kuzuia na kuwachukulia hatua wahusika.
Wenyewe wanajulikana walipo, viongozi wanafahamu fika uchafu huo unapofanyikia, kuanzia Buguruni, Ohio, Kinondoni Makaburini, Tunisia Road na maeneo mengine mengi, lakini imekuwa tabu kuwashughulikia.
RC aliyepita, Luteni Yusuf Makamba, alijaribu kidogo akaacha, kana kwamba alikosolewa au kuzuiwa na wakubwa. Hatuamini hivyo, lakini tunataka kuona, moto aliouwasha Kandoro, unaendelea kuwaka, mithili ya ule wa petroli.
Tusisikie hata kidogo kwamba umezimika, isipokuwa pale ambako utakapokuwa umeteketeza uchafu wote, mkaa na majivu yake visombwe na kutupwa mbali kusikofikika, kisha watu waishi kwa usafi. Kandoro kaza uzi, tutafika.