MBUNGE wa Viti Maalumu, Margareth Mkanga (CCM), ameitaka serikali kueleza ni kwa kiasi gani imewashirikisha watu wenye ulemavu katika ushiriki wa nchi katika mchakato unaoendelea kimataifa kuandaa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu.
Mbunge huyo pia amehoji kama serikali ina habari juu ya mchakato huo.
Akijibu maswali hayo bungeni mjini hapa jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alisema kuwa, serikali inayo habari kuhusu mchakato wa mkataba wa kimataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu.
“Kamati ya Umoja wa Mataifa ilianza kukutana mwaka 2002 na imeendelea kukutana mara moja au mbili kila mwaka. Kikao cha karibuni kilifanyika Februari mwaka huu mjini New York ambapo nchi yetu iliwakilishwa na ubalozi wetu uliopo New York.
“Vikao hivi ni muhimu, na serikali inapaswa kuhudhuria, ili kuchangia maoni yetu katika mchakato mzima kwa niaba ya wananchi wetu wenye ulemavu. Kutokana na ukosefu wa fedha, serikali haijapeleka ujumbe kwenye vikao hivi,” alisema.
Waziri alisema katika kikao cha mwisho cha mchakato huu na ambacho kitatoa maamuzi kuhusu mkataba kitakachofanyika Agosti mwaka huu, serikali inakusudia kutuma ujumbe.
Alisema ana imani kuwa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo utashirikisha watu wenye ulemavu.
Profesa Mwakyusa alisema matayarisho yamekamilika kwa Tanzania kuridhia kanuni hizo