SERIKALI imeanza msako rasmi dhidi ya wafanyabiashara wa mafuta ambao wanadaiwa kuyaficha kwenye maghala na kufanya bei ya nishati hiyo iwe ya juu.
Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, alisema hayo bungeni jana alipokuwa akielezea matatizo mbalimbali ya nishati nchini.
Hata hivyo, katika kauli yake hiyo, Msabaha hakusema ni adhabu ipi hasa watapewa wale watakaokutwa wameficha mafuta hayo.
“Hivi ninavyozungumza hapa bungeni, tayari serikali imetuma timu ya watu wake kwenda kwenye maghala ya wafanyabiashara ambao tumepata taarifa kwamba wameyaficha mafuta ya taa,” alisema.
Dk. Msabaha alisema lengo la kuyaficha mafuta hayo ni kufanya yawe kidogo kuliko mahitaji kwenye soko na hivyo bei ipande.
“Hii ni tamaa tu ya wafanyabiashara kutaka kupata faida, na serikali haiwezi kuwaachia waendelee na mtindo wao huo,” alisema.
Wakati akifanya majumuisho ya hotuba ya bajeti ya wizara yake aliyoiwasilisha mwanzoni mwa wiki, Dk. Msabaha alitangaza vita dhidi ya wafanyabiashara ya mafuta wenye tamaa ya kujitajirisha.
Alitangaza kwamba serikali imeamua kuliruhusu Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuagiza mafuta ili kupunguza upandaji holela wa bei ya nishati hiyo.